'
Sunday, November 18, 2012
SERENGETI BOYS YASHINDA, LAKINI...
TIMU ya soka ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 17, Serengeti Boys leo imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2013 baada ya kuichapa Congo Brazaville bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pamoja na kupata ushindi huo, Serengeti Boys inakabiliwa na kazi ngumu kutokana na kushindwa kuonyesha soka ya kuvutia na pia wachezaji kutoonyesha vipaji binafsi.
Iwapo Congo Brazaville wangekuwa makini, wangeweza kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao, kwa sababu walipata nafasi nyingi nzuri za kufunga mabao, lakini washambuliaji wake walishindwa kuzitumia vyema/
Bao pekee na la ushindi la Serengeti Boys lilifungwa na Mudathir Yahya Abbas kwa shuti la mpita wa adhabu la umbali wa mita zipatazo 20 lililombabatiza bezi mmoja wa Congo na kumzubaisha kipa na mpira kutinga wavuni.
Baadhi ya mashabiki waliohudhuria mechi hiyo walisema kuna tatizo kubwa katika uteuzi wa wachezaji wa Serengeti Boys kwa sababu baadhi ya wachezaji walionyesha kiwango duni cha soka.
Mashabiki hao walisema lingekuwa jambo la busara iwapo timu hiyo ingeongezewa nguvu na baadhi ya wachezaji kutoka timu za vijana wa umri huo za Simba, Azam na Yanga kwa vile zinaundwa na wachezaji wengi wazuri na wenye vipaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment