KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, November 26, 2012

SHARO MILIONEA AFARIKI DUNIA KWA AJALI





MSANII nyota wa vichekesho na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Ramadhani, maarufu kwa jina la Sharo Milionea amefariki dunia.
Sharo alifariki dunia kwa ajali ya gari jana saa mbili usiku katika barabara ya
Segera-Muheza wakati alipokuwa akitoka Dar es Salaam kwenda Muheza.
Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Constantine Massawe amesema kwa njia ya simu kuwa, Sharo alipata ajali katika eneo la Maguzonizoga wilayani Muheza baada ya gari alilokuwa akiendesha kuanja barabara na kupinduka mara kadhaa.
Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, marehemu Sharo alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR na kwamba alikuwa peke yake kwenye gari.
Kamanda alisema hakukuwa na kona kali sana wala ubovu wa barabara kwenye sehemu aliyopata ajali Sharo Milionea na kwamba gari hilo limehifadhiwa mahali salama kwa sababu halitembei.
Kamanda Massawe alisema mwili wa marehemu Sharo umehifadhiwa katika hospitali teule ya wilaya ya Muheza.
Marehemu Sharo alianza kujipatia umaarufu baada ya kushiriki kwenye filamu za vichekesho zilizokuwa zikitayarishwa na msanii mkongwe wa fani hiyo, Amri Athumani maarufu kwa jina la King Majuto.
Baadaye alijitosa kwenye fani ya muziki wa kizazi kipya, ambapo alifanikiwa kuteka soko la muziki huo baada ya kuibuka na kibao cha Chuki za nini.
Hivi karibuni, Sharo alijiongezea umaarufu zaidi baada ya kushiriki kutengeneza matangazo ya Kampuni ya Simu ya Airtel akiwa na King Majuto.
Blogu ya liwazozito inatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Sharo.

No comments:

Post a Comment