'
Friday, November 30, 2012
UGANDA YAUA
UGANDA imefuzu kwa asilimia 100 hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge baada ya kushinda mechi zake zote za Kundi A, ikiwemo ya leo waliyoshinda 4-0 dhidi ya Sudan Kusini.
Hakuna mjadala, Sudan Kusini inaondoka katika mashindano haya, bila kuingiza hata pointi moja, wakifungwa mechi zote tatu.Uganda na Kenya wamefuzu moja kwa moja, wakati Ethiopia walioshika nafasi ya tatu watasubiri hatima yao kufuzu kama mmoja wa washindi wa watatu bora kutoka makundi yote, A, B na C.
Katika mchezo wa leo, mabao ya Uganda ambao pia ni mabingwa watetezi yalifungwa na Brian Umony mawili katika dakika za 23 na 39, Robert Ssentongo dakika ya 47 na Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 79.
Katika mechi ya kwanza, Kenya ilishinda 3-1 dhidi ya Ethiopia, mabao ya Ramadhan Mohamed Salim, Clifton Miheso na David Ochieng, wakati la Ethiopia lilifungwa na Gatech Panom Yietch.
Michuano hiyo, itaendelea kesho kwa mechi za Kundi B na C, saa 8:00 mchana, Tanzania Bara watamenyana na Somalia Uwanja wa Lugogo na baadaye saa 10:00, Rwanda itacheza na Eritrea wakati Sudan itaanza na Burundi saa 8:00 mchana Uwanja wa Wankulunkulu na baadaye saa 10:00 jioni Malawi watamenyana na Zanzibar Wankulunkulu.
Kikosi cha Uganda kilikuwa; Ali Kimera, Robert Ssentongo, Joseph Ochaya, Kweyune Said, Henry Kalungi, Isaac isinde, Manco Kaweesa/Joseph Mpande, Geoffrey Kizito, Nico Wakiro Wadada, Brian Umony/Brian Majwega na Hamisi Kiiza.
FIFA YAWATEUA RONALDO, INIESTA, MESSI KUWANIA TUZO YA MWANASOKA BORA WA DUNIA
The contenders for the FIFA Ballon d’Or for the best player of 2012 and the FIFA Women’s World Player of the Year 2012 awards have been announced at a press conference held at the Anhembi Convention Center in Sao Paulo.
It was attended by FIFA President Joseph S. Blatter, FIFA Secretary General Jérôme Valcke, L’Equipe and France Football CEO François Morinière, and legendary Brazilian players Ronaldo and Marta, who won the FIFA World Player of the Year and FIFA Women's World Player of the Year awards three and five times respectively.
In alphabetical order, the FIFA Ballon d’Or nominees are Cristiano RONALDO, Portugal, Andres INIESTA, Spain and Lionel MESSI, Argentina, while MARTA, Brazil, Alex MORGAN, USA and Abby WAMBACH, USA will contest the women’s award.
The candidates for the FIFA World Coach of the Year for Men’s Football and FIFA World Coach of the Year for Women’s Football awards were also announced. In alphabetical order, the contenders are: Vicente DEL BOSQUE, Spain (Spain), Pep GUARDIOLA, Spain (FC Barcelona) and Jose MOURINHO, Portugal (Real Madrid) for the FIFA World Coach of the Year for Men’s Football award, and Bruno BINI, France (France), Norio SASAKI, Japan (Japan) and Pia SUNDHAGE, Sweden (USA) for the FIFA World Coach of the Year for Women’s Football award.
All the nominees were confirmed after a poll in which the captains and head coaches of the men’s and women’s national teams, as well as international media representatives selected by France Football, voted for candidates.
The shortlist of 15 forwards for the FIFA FIFPro World XI was also announced, completing the final shortlist of 55 players featuring five goalkeepers, 20 defenders and 15 midfielders. See the full list by clicking on the link to the right.
In addition, the three nominees for the FIFA Puskás award for the most beautiful goal of the year were announced. They are: FALCAO (América de Cali-Atletico Madrid, 19 May 2012), NEYMAR (Santos-Internacional, 7 March 2012) and Miroslav STOCH (Fenerbahçe-Gençlerbirliği, 3 March 2012).
All the awards will be presented at the FIFA Ballon d’Or Gala at the Kongresshaus in Zurich on 7 January 2013 during a televised show to be streamed live on FIFA.com and FIFA on YouTube.
In addition to the above awards, the recipient of the FIFA Presidential Award and the FIFA Fair Play award will also be revealed during the gala.
ZANZIBAR HEROES YAICHEZESHA KWATA RWANDA
MABAO mawili ya kiungo wa Azam FC, Khamis Mcha ‘Vialli’ usiku huu yameipa Zanzibar ushindi wa 2-1 dhidi ya Rwanda, katika mchezo wa Kundi C, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge uliofanyika kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala.
Kwa ushindi huo, Zanzibar Heroes imefufua matumaini ya kwenda Robo Fainali ya michuano hii, ikipanda kileleni mwa Kundi hilo, kwa pointi zake nne, Rwanda ikishuka nafasi ya pili kwa pointi zake tatu, sawa na Malawi, wakati Eritrea inashika mkia kwa pointi yake moja.
Vialli alifunga mabao yake moja kila kipindi, la kwanza dakika ya sita na la pili dakika ya 61, yote akionyesha yeye ni fundi na mwenye akili na maarifa ya soka kutokana na kutulia na kumtungua kipa hodari kabisa katika ukanda huu, Jean Claude Ndoli.
Rwanda ilipata bao lake kupitia kwa Dadi Birori dakika ya 79, ambaye aliingia uwanjani dakika ya 66 kuchukua nafasi ya Tumaine Ntamuhanga.
Mchezo wa leo kama ulivyokuwa mchezo wa kwanza kati ya Malawi na Eritrea ulitibuliwa na mvua iliyoharibu mandhari ya Uwanja wa Mandela, hivyo haikuwa wa ufundi zaidi ya ‘butua butua’.
Nahodha wa Zanzibar, Nadir Heroub ‘Cannavaro’ alisema baada ya mechi hiyo kwamba wamefuta makosa yao ya mchezo wa kwanza na sasa Wazanzibari wasubiri Kombe, wakati Haruna Niyonzima wa Rwanda, alilalamikia Uwanja mbovu leo kuwasababisha kucheza ovyo.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Zanzibar kilikuwa; Mwadini Ally, Nassor Masoud ‘Cholo’, Samir Hajji Nuhu, Aggrey Morris, Nadir Haroub Ali 'Canavaro, Sabri Ali, Khamis Mcha 'Vialli', Abdulaghan Gulam, Jaku Juma, Seif Abdallah/Adeyom Saleh Ahmed dk88 na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
Rwanda; Jean Claude Ndoli, Emery Bayisenge, Hamdani Bariyanga, Ismail Nshutiyamagara, Mwemere Ngirishuti/Jean Claude Iranzi dk46, Jean Baptiste Mugiraneza, Haruna Niyonzima, Jimmy Mbagara, Jerome Sina, Jean D’Amour Uwimana/Fabrice Twagizimana dk24 na Tumaine Ntamuhanga/Dadi Birori dk66.
Katika mchezo mwingine wa kundi hilo uliochezwa leo, Malawi iliichapa Eritrea mabao 2-0 na kufufua matumaini ya kucheza robo faibali.
(HABARI, PICHA KWA HISANI YA BLOGU YA BIN ZUBEIRY)
Thursday, November 29, 2012
WASHIRIKI WA MISS EAST AFRICA 2012 HAWA HAPA
MISS UNIVERSE TANZANIA 2012 AKABIDHIWA BENDERA
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa nchini(BASATA) Ghonche Materego(kushoto picha ya juu) akimkabidhi bendera ya Taifa Mrembo wa Tanzania anayeshikilia taji la Miss Universe 2012, Winfrida Dominic, kwenye ofisi za Baraza hilo jijini Dar es Salaam jana. Mrembo huyo anaiwakilisha Tanzania kwenye fainali za mashindano hayo nchini Marekani yanayotarajiwa kufanyika Desemba 19 mwaka huu. Picha ya chini, Materego akizungumza na mrembo huyo kabla ya kumkabidhi bendera.
Wednesday, November 28, 2012
KILIMANJARO STARS YACHEMSHA KWA BURUNDI
TIMU ya soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars jana ilijiweka katika mazingira magumu ya kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji baada ya kuchapwa bao 1-0 na Burundi.
Katika mechi hiyo ya kundi B iliyochezwa kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala, Uganda, Burundi ilijipatia bao la pekee dakika ya 52 lililofungwa kwa njia ya penalti na mshambuliaji Selemani Ndikumana.
Penalti hiyo ilitokana na kosa lililofanywa na beki Shomari Kapombe kumkwatua Ndikumana ndani ya eneo la hatari. Kapombe alionyeshwa kadi ya njano na alishindwa kuendelea na mchezo kutokana na kuumia.
Kutokana na kipigo hicho, Kilimanjaro Stars sasa italazimika iishinde Somalia katika mechi yake ya mwisho ya kundi hilo itakayochezwa keshokutwa. Iwapo itashinda mechi hiyo, inaweza kushika nafasi ya pili ama kuwa 'best looser'.
Kwa ushindi huo, Burundi imefuzu kucheza robo fainali kutokana na kuwa na pointi sita baada ya kushinda mechi mbili. Itahitimisha mechi za kundi hilo kwa kumenyana na Sudan.
Kilimanjaro Stars ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya nane wakati Mrisho Ngasa alipotoa pasi ndefu kwa Salum Abubakar, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango la Burundi.
Ngasa angeweza kufunga bao dakika ya 30 baada ya gonga safi kati ya Frank Domayo, Simon Msuva na John Boco, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya lango.
Burundi ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 39 wakati Hamisi Tambwe alipopiga mpira wa adhabu, kipa Juma Kaseja akautema, lakini mabeki wake walitokea na kuondosha hatari.
Amri Kiemba aliyeingia kipindi cha kwanza badala ya Msuva alichangamsha mashambulizi kwa Kilimanjaro Stars na nusura afunge bao dakika ya 41 baada ya kufumua shuti kali, ambalo kipa wa Burundi alilitema na kuudaka tena mpira. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Kilimanjaro Stars ilikianza kipindi cha pili kwa kasi na kupata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao dakika ya 47 na 49 na 88 lakini zilipotezwa na Ngasa, Mwinyi Kazimoto na Boco.
Kilimanjaro Stars iliwakilishwa na Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomari Kapombe/Idrisa Rashid, Kevin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, Mwinyi Kazimoto/Shaaban Nditi, John Boco, Simon Msuva/Amri Kiemba.
Katika mechi ya kwanza ya kundi hilo iliyochezwa kuanzia saa 10 jioni, Sudan ilifufua matumaini ya kusonga mbele baada ya kuichapa Somalia bao 1-0.
SAFARI YA MWISHO YA SHARO MILIONEA
Na Sophia Wakati, Muheza
MAMIA ya watu wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa na wasanii wa fani mbalimbali jana walishiriki katika mazishi ya msanii nyota wa maigizo na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Ramadhani, maarufu kwa jina la Sharo Milionea.
Marehemu Sharo Milionea, ambaye alifariki dunia Jumatatu iliyopita kwa ajali ya gari katika eneo la Makuzoni, alizikwa jana saa saba mchana katika kijiji cha Lusanga, Muheza mkoani Tanga.
Miongoni mwa wanasiasa waliohudhuria mazishi ya msanii huyo nyota ni Katibu wa NEC-CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi
Mbali na viongozi hao wa siasa, mazishi hayo pia yalihudhuriwa na wasanii zaidi ya 450 wa fani za filamu, vichekesho na muziki wa kizazi kipya, wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba, Jacob Steven 'JB' na Vicent Kigosi 'Ray'.
Msiba huo uligubikwa na simanzi zito kutoka kwa waombolezaji, ambao walishindwa kujizuia kuangua kilio, hasa baada ya mwili wa marehemu kuwasili nyumbani kwao kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali teule ya Muheza.
Wasanii waliokuwa karibu na msanii huyo kama vile Mussa Yussuf 'Kitale' pamoja na Amri Athumani 'King Majuto' waliishiwa nguvu kutokana na majonzi waliyokuwa nayo na ilibidi wapate msaada kutoka kwa watu wengine.
Waombolezaji walianza kumiminika kijijini Lusanga tangu juzi
jioni na idadi iliongezeka na kuwa kubwa kuanzia jana asubuhi. Kamati ya mazishi iliongozwa na mkuu wa wilaya ya Muheza,Subira.
Sala ya jeneza iliongozwa na Sheikh Twaha Juma na baada ya sala hiyo, waombolezaji walijipanga mistari miwili kwa ajili ya kubeba jeneza hadi makaburini, umbali wa mita 100.
Akitoa salamu kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi, Nape alisema, Mwenyekiti wa Chama, Rais Jakaya Kikwete amestushwa na kifo cha msanii huyo, na kwamba anatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wapenzi wote wa tasnia ya filamu na muziki wa bongo fleva.
"Napenda kuwapeni pole wote kutokana na msiba huu wa kipenzi chetu Sharo Milionea. Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amenituma nifkishe salam hizi za pole kwenu na amesema amestushwa sana na kifo cha msanii huyu," alisema Nape.
"Tunashukuru Mungu kwamba muda mfupi tuliyeishi naye, Sharo Milionea amefanya mambo yatakayotufanya tumkumbuke daima," alisema Nape na kuongeza:
"Licha ya umri wake mdogo, wingi huu wa watu waliohudhuria hapa kumzika, ni uthibitisho kwamba Sharo Milionea ameacha alama nzuri, hivyo ni vizuri tuliobaki kuiga mfano wake na kuyaenzi aliyofanya," alisema.
Nnauye alisema umefika wakati sasa kwa wasanii kuungana na kuhakikisha jasho lao halipotei wala kunyonywa na wajanja wengine, ambao wamekuwa wakinufaika huku wasanii wakiendelea kubaki masikini.
Nape amevitaka vyombo vinavyohusika kusimamia kazi litaka ihakikishwe kwamba haki za kazi za kisanii za Sharo Milionea alizoacha zisitapanywe, badala yake zilindwe kwa mujibu wa sheria ili ziinufaishe familia ya marehemu.
Katibu huyo wa NEC Itikadi na Uenezi pia alilaani kidendo cha watu waliovamia eneo la ajali na kupora vitu mbalimbali vya marehemu Sharo Milionea ikiwa ni pamoja na kumvua nguo zake. Aliitaka serikali kuhakikisha inawasaka wahusika na kuwatia mbaroni.
Akizungumzia uporaji huo, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, alisema, serikali wilayani humo itahakikisha inawasaka popote walipo, waliohusika na unyama huo wa kumpora marehemu Sharo Milionea wakati wa ajali hiyo.
WAGOMBEA DRFA WAONYWA
MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Juma Simba 'Ghadafi' amewaonya wagombea waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho kuepuka kutoa rushwa.
Simba alitoa onyo hilo juzi wakati alipokuwa akitangaza majina ya wagombea 23 waliopitishwa kuwania uongozi wa chama hicho katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 8 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Alisema kamati yake itakuwa makini kufuatilia nyendo za wagombea katika uchaguzi huo na wale watakaobainika kutoa rushwa kwa wapiga kura, watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Simba amewataka wajumbe wa mkutano huo kuwatendea haki watu wa Dar es Salaam kwa kuwachagulia viongozi wenye sifa na uwezo wa kuendeleza soka katika mkoa huo.
Mwenyekiti huyo alisema yeye na kamati yake wanaamini kuwa, wawakilishi wa vyama vya soka vya wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni watafanyakazi nzuri kwa kuchagua viongozi wenye uchungu wa soka.
"Tumeshaaanza kusikia tetesi kwamba baadhi ya wagombea waliopitishwa kuwania uongozi katika uchaguzi huo wameanza kuwarubuni wapiga kura. Binafsi siamini kama wajumbe wa DRFA watakubali kurubuniwa na kuuza haki yao,"alisema.
Kwa mujibu wa Simba, wameandaa vitambulisho maalumu kwa ajili ya wapiga kura, vitakavyokuwa na picha zao ili waweze kutambulika kirahisi. Pia alisema wameandaa vitambulisho kwa ajili ya waandishi wa habari, ambao watatengewa eneo maalumu la kukaa.
JB MPIANA KUANZA MAKAMUZI LEO MWANZA
MWANAMUZIKI JB Mpiana na kundi lake la Wenge Musica (BCBG) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, anatarajiwa kuanza makamuzi yake leo kwa kufanya onyesho mjini Arusha.
Mkurugenzi wa Kampuni ya QS Muhonda, inayoratibu ziara ya mwanamuziki huyo, Joseph Muhonda alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, JB Mpiana na kundi lake wanatarajiwa kufanya maonyesho matatu nchini.
Muhonda alisema JB Mpiana atafanya onyesho lake la pili kesho kwenye viwanja vya Leaders Club vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, akishirikiana na bendi ya Mashujaa.
Kwa mujibu wa Muhonda, onyesho hilo litakuwa maalumyu kwa ajili ya kusindikiza uzinduzi wa albamu mpya ya Mashujaa, inayokwenda kwa jina la Risasi Kidole.
Alisema onyesho la tatu la mwanamuziki huyo na kundi lake limepangwa kufanyika Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Kwa upande wake, JB Mpiana aliwaambia waandishi wa habari kwenye hoteli ya Double Tree mjini Dar es Salaam juzi kuwa, amekuja kukonga nyoyo za mashabiki wa muziki wa Tanzania.
"Nina imani waandaaji wamefanya maandalizi ya kutosha, nimekuja na wanamuziki wangi wote 25, nimekuja na vifaa vyangu vyote ili kuwapa burudani ya kutosha,"alisema mwanamuziki huyo.
JB Mpiana aliwataka mashabiki wa muziki nchini wajiandae kupata uhondo wa nyimbo zake mpya zilizomo kwenye albamu ya Biloko.
TAIFA STARS KAMBINI BAADA YA CHALENJI
TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars inatarajiwa kuingia kambini baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Chalenjji, inayoendelea nchini Uganda.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kambi hiyo itakuwa kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia.
Michuano ya Kombe la Chalenji, iliyoanza kutimua vumbi Novemba 24 kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala, Uganda, inatarajiwa kufikia tamati Desemba 8 mwaka huu.
Taifa Stars inatarajiwa kumenyana na Zambia katika mechi ya kirafiki itakayopigwa Desemba 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kim alisema baada ya pambano hilo dhidi ya Zambia, wachezaji wa Taifa Stars watapewa mapumziko ya wiki mbili kabla ya kuingia tena kambini Januari 6 hadi 20 mwakani kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi nyingine ya kirafiki.
Kwa mujibu wa Kim, mechi hizo mbili zimelenga kuiandaa Taifa Stars kwa pambano lake la michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 dhidi ya Morocco.
Kocha huyo alisema amepanga kuongeza kipa mmoja kwenye kikosi chake ili kuwasaidia makipa wa sasa, Juma Kaseja na Deogratius Munish pamoja na chipukizi kadhaa kutoka timu za vijana wa chini ya miaka 17 na 20 kwa lengo la kuwapa uzoefu.
Kim alisema kwa sasa anafuatilia vipaji vya wachezaji wa Zanzibar, Zanzibar Heroes wanaoshiriki katika michuano ya Kombe la Chalenji nchini Uganda. Zanzibar imepangwa kundi moja na timu za Eritrea, Malawi na Rwanda.
BURIANI SHARO MILIONEA
Sharo alifariki dunia kwa ajali ya gari Jumatatu iliyopita saa mbili usiku katika barabara ya Segera-Muheza wakati alipokuwa akitoka Dar es Salaam kwenda Muheza.
Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alisema kwa njia ya simu kuwa, Sharo alipata ajali katika eneo la Maguzonizoga wilayani Muheza baada ya gari alilokuwa akiendesha kuacha barabara na kupinduka mara kadhaa.
Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, marehemu Sharo alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR na kwamba alikuwa peke yake kwenye gari.
Kamanda alisema hakukuwa na kona kali sana wala ubovu wa barabara kwenye sehemu aliyopata ajali Sharo Milionea.
WASEMAVYO WASANII
Kifo cha marehemu Sharo kilipokelewa kwa mshtuko mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa ndio kwanza anaanza kuchipukia katika fani ya vichekesho na muziki wa kizazi kipya.
Baadhi ya wasanii wenzake walipopata taarifa hizo, walihisi ni za uzushi tu, uliolenga kuwashtua watu na kuwafanya wataharuki. Kwa waliokuwa karibu naye, walitamani taarifa hizo ziwe za kuzusha, wakiamini kuwa, Sharo hawezi kuondoka duniani mapema kiasi hiki.
Wasanii wengine wamemwelezea Sharo kwamba ameiaga dunia akiwa bado mdogo huku akiwa na ndoto nyingi na malengo mengi. Wamekifananisha kifo cha Sharo kuwa ni sawa na kipaji kilichoyeyuka mithili ya mshumaa uliowaka na kuzimwa na upepo wa kifo!
Lakini hivyo ndivyo kifo kilivyo. Hakina taarifa. Humtokea binadamu wakati na muda wowote. Tunatembea nacho. Hakuna anayeweza kufahamu ni lini ataondoka duniani. Ni siri kubwa, ambayo Mwenyezi Mungu amewaficha viumbe wake.
Marehemu Sharo alianza kujipatia umaarufu baada ya kushiriki kwenye filamu za vichekesho zilizokuwa zikitayarishwa na msanii mkongwe wa fani hiyo, Amri Athumani maarufu kwa jina la King Majuto.
Baadaye alijitosa kwenye fani ya muziki wa kizazi kipya, ambapo alifanikiwa kuteka soko la muziki huo baada ya kuibuka na kibao cha Chuki za nini.
Hivi karibuni, Sharo alijiongezea umaarufu zaidi baada ya kushiriki kutengeneza matangazo ya Kampuni ya Simu ya Airtel akiwa na King Majuto.
MAHOJIANO YA MWISHO
Katika mahojiano na gazeti la Burudani yaliyochapishwa mapema mwaka huu, Sharo alielezea kwa kirefu kuhusu alikotoka, malengo na matarajia yake ya baadaye katika fani ya vichekesho na muziki wa kizazi kipya.
Msanii huyo aliyekuwa na mvuto wa aina yake alisema alibuni staili ya usharobaro kwa lengo la kujitofautisha na wasanii wengine. Alisema ubunifu wake huo ulimwezesha kupata mashabiki wengi katika fani zote mbili.
Sharo alisema licha ya kuwepo kwa tabia ya watu wanaojikweza kwa muda mrefu, wakiwa maarufu kwa jina la ‘mabradha meni’, staili aliyoibuni ya watu wa aina hiyo imekuwa na mvuto zaidi.
Alivitaja vitu vingine alivyovibuni kwa lengo la kuupa mvuto ‘ubradha meni’ kuwa ni pamoja na uzungumzaji wake kwa kupinda mdomo, uvaaji, utembeaji, unyoaji nywele na kubandika plasta usoni.
“Staili ya mabradha meni asili yake hasa ni Wamarekani. Kila wakisema neno, lazima wamalizie kwa kusema ‘you know man’. Nami nimeiiga, lakini nimeongezea vionjo vingine zaidi,”alisema.
Hussein alisema alianza kujihusisha na uigizaji tangu akiwa shule ya sekondari na kwamba amewahi kucheza filamu moja na baadhi ya wasanii maarufu kama vile Masanja Mkandamizaji na McReagan wa kundi la Orijino Komedi.
Aliongeza kuwa, fani ya uchekeshaji ni asili yake tangu akiwa mdogo kutokana na kuwafurahisha vijana wenzake kila walipokuwa wakikutana kwa mazungumzo vijiweni kwa kubuni maneno yenye mvuto.
“Kila nilipokuwa nikikaa na kuzungumza na wenzangu, niliposema maneno fulani, walikuwa wakivutiwa nayo sana na kuniona mtu wa ajabu, yaani mchekeshaji,”alisema.
KIPAJI CHA MUZIKI
Hussein alisema aliamua kujitosa kwenye fani ya muziki baada ya kujibaini kwamba, anacho kipaji cha fani hiyo na hadi sasa amesharekodi nyimbo nne. Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Tusigombane, Chuki bure aliomshirikisha Dully Sykes, Nawazamisha aliomshirikisha Nukta na Hawataki alioimba kwa kushirikiana na Kanali Top na Richard Mavoko.
Kwa mujibu wa Hussein, aliweza kurekodi nyimbo hizo kwa msaada mkubwa wa promota maarufu wa muziki nchini, Ustaadh Juma Namusoma, ambaye kwa sasa anamiliki kundi la Watanashati.
Hussein alisema kwa sasa ameshampata mdhamini, atakayekuwa akigharamia kurekodi nyimbo zake pamoja na kurekodi kanda za video, lakini hakuwa tayari kumtaja.
Alisema kwa kumtumia mdhamini huyo, ameanza kuandaa nyimbo zake mpya, ambazo atazirekodi kwa kushirikiana na msanii mwenzake nyota wa vichekesho, anayejulikana zaidi kwa jina la Kitale.
Alikiri kuwa, licha ya kurekodi nyimbo nne hadi sasa, bado hajaweza kupata mafanikio makubwa kimuziki kutokana na fani hiyo kukumbwa na vikwazo vingi. Alisema mafanikio pekee aliyoyapata ni kujulikana na mashabiki wengi wa muziki na pia kupata marafiki wapya kila kukicha.
“Kwa sasa nitaendelea kurekodi wimbo mmoja mmoja hadi hapo mambo yatakapokuwa mazuri ndipo nitakaporekodi albamu,”alisema msanii huyo.
Alipoulizwa madai kuwa, amekuwa akipenda kujifagilia katika vichekesho anavyocheza pamoja na nyimbo zake, Hussein alisema huo ni uigizaji, lakini sivyo alivyo.
AMTAJA KIWEWE
Hussein alikiri kuwa, miongoni mwa watu waliomwonyesha njia katika fani ya uigizaji ni msanii Kiwewe wa kundi la Ze Comedy. Lakini alikanusha madai kwamba, amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mcheza filamu, Shilole.
“Shilole ni rafiki yangu na ni kama dada yangu. Vivyo hivyo kwa Mzee Majuto, namuheshimu, nampenda na kumuheshimu kama baba yangu," alisema.
Msanii huyo pia alikanusha madai kuwa, aliwahi kugombania jina la Sharobaro na msanii Bob Junior. Alisema jina la kiusanii analotumia ni Sharo Milionea na siyo Sharobaro.
Hussein amekiri kuwa, katika wimbo wa Ferouz wa Starehe gharama, alikubali kuvua nguo zake kwenye picha ya video baada ya kulipwa kitita cha sh. milioni moja na nusu, ambacho alikielezea kuwa kwake ni kikubwa.
AKI, UKWA WAWATEMBELEA WAATHIRIKA WA MAFURIKO DELTA
LAGOS, Nigeria
WACHEZA filamu machachari wa Nigeria, Chinedu Ikedieze 'Aki' na Osita Iheme 'Ukwa' wiki hii walitembelea katika jimbo la Delta lililopo Kusini mwa Nigeria na kuwafariji waathirika wa mafuriko.
Aki na Ukwa walitembelea katika jimbo hilo kwa mwaliko wa Gavana Emmanuel Uduaghan kwa ajili ya kutoa misaada kwa waathirika.
Wacheza filamu hao walipokewa kwa furaha kubwa na wakazi wa jimbo hilo, ambao walionyesha furaha yao kuwaona nyota hao wakifika kuwafariji wakati wa matatizo.
Wakiwa katika jimbo hilo, Aki na Ukwa walipiga picha na wakazi wa jimbo hilo, hasa watoto wadogo, ambao walionekana kufurahia kupata nafasi hiyo.
Aki na Ukwa walikabidhi misaada mbalimbali kwa waathirika wa mafuriko hayo, waliokuwa wamehifadhiwa katika kambi maalumu.
MR IBU: FAMILIA YANGU ILIKUWA MASIKINI KULIKO ZOTE KIJIJINI
LAGOS, Nigeria
BAADHI ya watu huzaliwa katika familia tajiri, lakini wengine huzaliwa katika familia za kimaskini. Kwa mcheza filamu wa Kinigeria, John Okafor, maarufu kwa jina la Mr. Ibu, anakumbuka wakati wa ujana wake, hakuwahi hata kumiliki kijiko cha kulia chakula.
Akihojiwa na mtandao wa naijerules wiki hii, Mr. Ibu alisema kabla ya kuwa maarufu, aliishi maisha ya dhiki na mateso makubwa.
Mr. Ibu alisema familia yake ilikuwa maskini kuliko zote katika kijiji alichokuwa akiishi cha Umunekwu kilichoko Ezeokwe katika Jimbo la Enugu.
"Baada ya baba yangu kufariki, katapila lilibomoa nyumba yetu, tukawa sawa na wakimbizi katika kijiji chetu,"alisema Mr. Ibu.
"Tulizaliwa wanane, wanaume watano na wanawake watatu.Tulipewa chumba kimoja, ambamo tulilala sote usiku kama vile tupo selo. Mguu mmoja hapa mwingine kule," alisema mcheza filamu huyo huku akiangua kicheko.
"Ukiwa masikini, ni masikini tu. Utalazimika kutazama vitu vingi kutoka upande mwingine. Baba yangu aliacha kunisomesha wakati nilipokuwa bado mdogo. Alifariki mwaka 1975,"alisema.
Mr. Ibu alisema kifo cha baba yake kilisababisha watoto wote wafanyekazi ya kujilisha na pia kumlisha mama yao. Pia alisema alilazimika kufanyakazi za aina mbalimbali ili aweze kupata fedha za kujikimu.
Alizitaja baadhi ya kazi hizo kuwa ni pamoja na kuuza kuni, kunyoa watu nywele, kutengeneza kreti za vinywaji kwa kutumia mbao na pia kupiga picha za mitaani. Alisema pesa alizopata alizitumia kujisomesha elimu ya sekondari.
Mr. Ibu alisema pia kuwa, kuna wakati alilazimika kufanyakazi ya kuuza bucha. Kwamba yeyote aliyekuwa akihitaji kuchinjiwa mbuzi, ng'ombe na nguruwe, alikuwa tayari kwa kazi hiyo.
"Hivyo ndivyo nilivyoweza kuendesha maisha yangu. Ni kupitia katika kazi hizo, niliweza kupata pesa za kujisomesha. Baadaye niliongezewa pesa za shule na kaka yangu,"alisema Mr. Ibu.
Kwa mujibu wa Mr. Ibu, baada ya kuteuliwa kujiunga na Taasisi ya Teknolojia na Utawala ya Enugu, kaka yake alimshauri asome kwa muda mfupi kwa vile isingekuwa rahisi kupata fedha za kulipa mihula yote ya masomo.
"Hakukuwa na muda wa kupumzika kwa sababu yalikuwa ni mapambano wakati wote. Mapambano ya kwenda shule na mapambano ya kuilisha familia yetu na mama yetu,"alisema
Mr. Ibu alisema wakati wa mapambano hayo, waliwapoteza ndugu wawili katika familia yao na kwamba umaskini waliokuwa nao ulimwezesha kujifunza mambo mengi.
"Hivi sasa namshukuru Mungu kwa miujiza yake," alisema Mr. Ibu ambaye ni miongoni mwa wacheza filamu wenye uwezo mkubwa kipesa, akiwa na mke na watoto wawili.
WILFRIED ZAHA, KINDA ANAYEVITOA UDENDA VIGOGO VYA ENGLAND
LONDON, England
KOCHA Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha nia yake ya kutaka kumsajili winga wa klabu ya Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Wilfried Zaha.
Wenger amepanga kumsajili kinda huyo anayekadiriwa kuwa na thamani ya pauni milioni 20 za Uingereza wakati wa usajili wa dirisha dogo Januari mwakani.
Kocha Msaidizi wa zamani wa Arsenal, Pat Rice, ambaye bado anafanyakazi katika klabu hiyo pamoja na mvumbuzi mkuu wa wachezaji, Steve Rowley ndiyo waliompatia Wenger taarifa kuhusu kinda huyo, ambaye walimshuhudia akicheza hivi karibuni.
Arsenal imepanga kuwasilisha ofa ya kumsajili Zaha kwa klabu ya Crystal Palace kwa malipo ya pauni milioni tisa wakati usajili wa dirisha dogo utakapoanza.
Hata hivyo, kuna habari kuwa Mwenyekiti wa Crystal Palace, Steve Parish hataweza kukubali kinda huyo aondoke ndani ya klabu yake kwa kiasi hicho cha pesa.
Alipoulizwa Jumanne iliyopita iwapo ni kweli anamuhitaji mchezaji huyo, Wenger alisema: "Tunatafuta kila mchezaji, atakayeweza kukiongezea nguvu kikosi chetu, lakini kwa sasa hayumo kwenye orodha yangu."
Mbali na Arsenal, klabu zingine zilizoonyesha nia ya kumsajili Zaha ni pamoja na Liverpool, Manchester City na Manchester United.
Zaha (20) amezikuna klabu nyingi za England baada ya kuonyesha kiwango cha juu wakati timu ya taifa ya nchi hiyo ilipomenyana na Sweden katika mechi ya kirafiki ya kimataifa mapema mwezi huu, ikiwa ni mechi yake ya kwanza.
Kinda huyo alianza kuichezea Crystal Palace akiwa na umri wa miaka 17, Mei 2012 na hadi sasa ameshaichezea timu hiyo katika mechi 112 na kuifungia mabao 14.
Wenger anaamini kuwa, Arsenal ni lazima ijenge na kukiimarisha kikosi chake kwa kuwatumia wachezaji vijana waliopo England kama ilivyo kwa Jack Wilshere.
Zaha alirejea uwanjani hivi karibuni baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu na kwa sasa yupo kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya kati yake na viongozi wa Crystal Palace.
Wenger anaamini kuwa, iwapo Zaha ataungana na nyota wengine wa England kama vile Kieran Gibbs, Wilshere na Alex Oxlade Chamberlaini, kikosi cha Arsenal kitakuwa tishio katika ligi kuu ya England na michuano ya kimataifa.
Zaha amesaliwa na miaka miwili na nusu kumaliza mkataba kati yake na Crystal Palace na Wenger amekiri kuwa ni muda mrefu, lakini hawezi kukata tamaa ya kumpata.
Wenger alisema anataka kinda huyo pamoja na wachezaji wengine wa zamani kama vile Theo Walcott na Aaron Ramsey wacheze kwenye kikosi chake kwa muda mrefu.
Msimu uliopita, nahodha wa zamani wa timu hiyo, Robin van Persie aligoma kuongeza mkataba mpya na Arsenal, badala yake aliamua kutua Manchester United kwa uhamisho uliogharimu pauni milioni 24.
Kwa sasa, Arsenal inafurahia uamuzi wake wa kutoa kipaumbele kuwasajili wachezaji chipukizi wa England, ambao wamefanikiwa kuunda kikosi imara.
Kocha huyo anaamini kuwa, kusajiliwa kwa chipukizi wa England kutawafanya wachezaji hao kuichezea timu hiyo kwa kipindi kirefu kuliko ilivyo kwa wachezaji wa kigeni.
Hata hivyo, Wenger alisisitiza kuwa, katika kutekeleza mpango wao huo, watazingatia zaidi uwezo na viwango vya wachezaji.
Zaha ameripotiwa kuwa shabiki mkubwa wa Arsenal tangu akiwa mdogo na hilo linamfanya Wenger awe na uhakika mkubwa wa kumpata wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Kuna habari kuwa, tayari Manchester City imeshaanza kufanya mipango ya awali ya kumsajili kinda huyo huku Liverpool na Tottenham nazo zikionyesha nia ya kufanya hivyo.
Zaha alizaliwa Novemba 10, 1992 katika mji wa Abidjan nchini Ivory Coast. Majina yake kamili ni Dazet Wilfried Armel Zaha. Anatumia jezi yenye namba 16. Alijiunga na Crystal Palace kuanzia 2002 hadi 2009 akiwa katika timu ya vijana kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2010.
Amewahi kuzichezea timu za taifa za vijana wa chini ya miaka 19 na 21 za England kabla ya kuvaa uzi wa timu ya taifa ya wakubwa kwa mara ya kwanza katika mechi dhidi ya Sweden iliyochezwa mapema mwezi huu.
Zaha alihamia England akiwa na familia yake wakati akiwa na umri wa miaka minne. Alisoma katika shule ya Whitehorse Manor Junior, Thornton Heath na Selsdon.
Tuesday, November 27, 2012
SHARO MILIONEA ALIPORWA SH. MILIONI SITA KATIKA ENEO LA AJALI
SWAHIBA wa aliyekuwa msanii nyota wa vichekesho na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Ramadhani, maarufu kwa jina la Sharo Milionea, amesema marehemu alikuwa na sh. milioni sita kabla ya ajali.
Akihojiwa na kituo cha redio cha Clouds FM leo usiku, swahia huyo wa Sharo Milionea, Mussa Yussuf maarufu kwa jina la Kitale amesema alizungumza kwa simu na rafiki yake huyo na kumueleza kwamba alikuwa safari kwenda Tanga kumpelekea mama yake sh. milioni sita.
Kwa mujibu wa Kitale, alipata nafasi ya kuzungumza na Sharo Milionea muda mfupi kabla ya ajali hiyo na kupanga kwenda naye katika mazishi ya msanii mwenzao wa filamu, marehemu John Maganga aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita na kuzikwa jana.
Kitale alisema alifanya mazungumzo hayo na Sharo Milionea wakati alipokuwa safarini akirejea Dar es Salaam kutoka Iringa, ambako alikwenda kushiriki kwenye tamasha la Asante Tanzania, lililoandaliwa na msanii Sajuki na mkewe Stara.
Lakini wakati akikaribia kufika Dar es Salaam, Kitale alisema alishangaa alipompigia simu Sharo Milionea na kumueleza kwamba alikuwa safarini kwenda Tanga kumtembelea mama yake.
"Aliniambia hataweza kwenda kwenye mazishi ya Maganga kwa sababu alikuwa na mzigo muhimu aliokuwa akimpelekea mama yake Tanga. Aliniambia alikuwa akimpelekea mama yake shilingi milioni sita kwa ajili ya kazi muhimu,"alisema.
Kabla ya tukio hilo, Kitale alisema marehemu Sharo Milionea alimkaribisha katika nyumba mpya aliyopanga katika maeneo ya Magomeni, Dar es Salaam, ambapo alikuwa akilipa kodi ya shilingi laki mbili kwa mwezi.
Kitale alisema Sharo aliamua kuhamia kwenye nyumba hiyo mpya kwa lengo la kubadili hali ya maisha kwa vile mambo yalishaanza kumuendea vizuri, tofauti na alivyokuwa akiishi miaka ya nyuma.
Swahiba huyo wa Sharo Milionea alieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha watu wa kwanza waliofika katika eneo la ajali kumvua marehemu nguo zote alizokuwa amezivaa na kumuacha akiwa na nguo ya ndani.
"Kwa kweli hawa watu wamefanya kitendi kibaya sana," alisema Kitale kwa sauti iliyojaa majonzi makubwa kutokana na msiba huo mzito wa swahiba wake.
Akizungumzia jinsi alivyopata taarifa hizo, Kitale alisema alipigiwa simu na mmoja wa rafiki zake na alishindwa kuziamini hadi alipowasiliana na King Majuto, hali iliyosababisha aishiwe nguvu.
Kitale alisema amempoteza mtu muhimu katika maisha yake na hajui ataendeleaje kushiriki katika fani ya vichekesho na muziki wa kizazi kipya bila ya Kitale.
CCM YATUMA RAMBIRAMBI VIFO VYA MAGANGA, SHARO MILIONEA
Chama Cha Mapinduzi kimetuma salamu za rambirambi na pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, mashabiki wa wasanii wawili wa sanaa za maigizo na vichekesho Marehemu John Maganga aliyefariki Novemba 24, 2012 jijini Dar es Salaam na Hussein Mkiety aliyejulikana sana kwa jina la usanii ( Sharo Milionea) aliyefariki Novemba 26,2012 kwa ajali ya gari mkoani Tanga.
Katika salamu za Chama, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Itikadi na Uenezi Ndugu Nape Moses Nnauye ametoa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa namna yeye binafsi na CCM kwa ujumla walivyoguswa na Msiba huo mkubwa uliohusisha wasanii wawili vijana kabisa, kwa wakati Mfupi.
Katika salamu zake, Ndugu Nape amesema: “Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa habari za kutokea kwa ajali ya barabarani katika kijiji cha Lusanga Wilayani Muheza mkoani Tanga, iliyosababisha kifo cha kijana Hussein Mkiety.”
Ameongeza Ndugu Nape "Pia nimepokea kwa masikitiko Makubwa Taarifa za kifo cha Msanii we Sanaa ya maigizo Marehemu John Maganga kilichotokea katika hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kuugua kwa muda mfupi."
Ameongeza kuwa Vifo vya vijana hao wawili vilivyotokea katika Umri mdogo Kabisa, ni pigo kwa familia, tasnia ya filamu za maigizo na tasnia ya Sanaa, pamoja na Taifa kwa ujumla, kwani kazi zao zilikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya Sanaa, na Taifa kwa ujumla.
AJALI YA SHARO MILIONEA PICHANI
HIVI ndivyo gari alilokuwa akiendesha msanii Sharo Milionea lilivyopata ajali katika barabara ya Segera-Muheza mjini Tanga jana saa mbili usiku. (Picha kwa hisani ya gazeti la Uhuru).
Monday, November 26, 2012
JB MPIANA ATUA DAR
MWANAMUZIKI JB Mpiana kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
JB Mpiana akisindikizwa kutoka nje ya uwanja wa ndege na baadhi ya wenyeji wake. Mwanamuziki huyo anatarajia kupamba onyesho la uzinduzi wa albamu ya bendi ya Mashujaa.
SHARO MILIONEA AFARIKI DUNIA KWA AJALI
MSANII nyota wa vichekesho na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Ramadhani, maarufu kwa jina la Sharo Milionea amefariki dunia.
Sharo alifariki dunia kwa ajali ya gari jana saa mbili usiku katika barabara ya
Segera-Muheza wakati alipokuwa akitoka Dar es Salaam kwenda Muheza.
Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Constantine Massawe amesema kwa njia ya simu kuwa, Sharo alipata ajali katika eneo la Maguzonizoga wilayani Muheza baada ya gari alilokuwa akiendesha kuanja barabara na kupinduka mara kadhaa.
Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, marehemu Sharo alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR na kwamba alikuwa peke yake kwenye gari.
Kamanda alisema hakukuwa na kona kali sana wala ubovu wa barabara kwenye sehemu aliyopata ajali Sharo Milionea na kwamba gari hilo limehifadhiwa mahali salama kwa sababu halitembei.
Kamanda Massawe alisema mwili wa marehemu Sharo umehifadhiwa katika hospitali teule ya wilaya ya Muheza.
Marehemu Sharo alianza kujipatia umaarufu baada ya kushiriki kwenye filamu za vichekesho zilizokuwa zikitayarishwa na msanii mkongwe wa fani hiyo, Amri Athumani maarufu kwa jina la King Majuto.
Baadaye alijitosa kwenye fani ya muziki wa kizazi kipya, ambapo alifanikiwa kuteka soko la muziki huo baada ya kuibuka na kibao cha Chuki za nini.
Hivi karibuni, Sharo alijiongezea umaarufu zaidi baada ya kushiriki kutengeneza matangazo ya Kampuni ya Simu ya Airtel akiwa na King Majuto.
Blogu ya liwazozito inatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Sharo.
ZANZIBAR HEROES YABANWA, RWANDA YASHINDA
TIMU ya soka ya Zanzibar, Zanzibar Heroes leo imeshindwa kutamba mbele ya Eritrea baada ya kulazimishwa kutoka nayo suluhu katika mechi ya kundi C iliyopigwa kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala, Uganda.
Katika mechi hiyo, tatizo kubwa la Zanzibar Heroes lilikuwa umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake, ambao walishindwa kumalizia mipira ya mwisho.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa leo, Rwanda iliichapa Malawi mabao 2-0.
Matokeo hayo yameiwezesha Rwanda kuongoza kundi hilo ikiwa na pointi tatu baada ya kucheza mechi moja, ikifuatiwa na Eritrea na Zanzibar zenye pointi moja kila moja.
Mabao ya Rwanda yalifungwa na Jean Baptiste Mugiraneza na Haruna Niyonzima dakika ya 37 na 79.
YANGA KUWEKA KAMBI UTURUKI
UONGOZI wa klabu ya Yanga umepanga kuipeleka timu hiyo kambini nchini Uturuki kwa wiki mbili na kwamba ziara hiyo itafanyika mapema mwakani.
Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Yanga, Abdalla Bin Kleb amesema leo kuwa, timu hiyo itakwenda huko kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Bin Kleb alisema ziara hiyo imepangwa kufanyika kati ya Desemba mwaka huu na Februari mwakani.
Alisema kocha mkuu wa timu hiyo, Ernie Brandts ndiye aliyewasilisha pendekezo la timu hiyo kwenda kuweka kambi katika nchi hiyo kutokana na uzoefu wake.
Kwa mujibu wa Bin Kleb, ikiwa Uturuki, timu hiyo inatarajiwa kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya timu za nchi hiyo.
Katika hatua nyingine, Brandts ameamua kuwapandisha daraja wachezaji watatu kutoka katika kikosi cha pili cha timu hiyo, kinachoundwa na wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 20.
Aliwataja wachezaji hao kuwa ni kipa Yussuf Abdalla, George Banda na Rehan Kibinga.
Sunday, November 25, 2012
BOCCO AIBEBA KILIMANJARO STARS, YAITUNGUA SUDAN 2-0
Timu ya soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars leo imeanza vyema michuano ya soka ya Kombe la Chalenji baada ya kuichapa Sudan mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala, Uganda.
Mshambuliaji John Bocco ndiye aliyeibeba Kilimanjaro Stars baada ya kuifungia mabao hayo mawili katika kipindi cha kwanza baada ya kuunganisha wavuni pasi maridhawa kutoka kwa Mrisho Ngasa. Katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa leo, Burundi imeipiga Somalia mabao 5-1 na hivyo kushika usukani wa kundi hilo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na Kilimanjaro Stars. Michuano hio inatarajiwa kuendelea leo wakati Zanzibar itakapomenyana na Eritrea.
Saturday, November 24, 2012
UGANDA YAICHAFUA KENYA
WENYEJI Uganda, The Cranes wameanza vema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge baada ya kuilaza Kenya, Harambee Stars bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mandela, uliopo Namboole, Kampala, Uganda.
Shukrani kwake, mshambuliaji wa Saigon Xuan Thanh ya Vietnam, Geoffrey Kizito aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 74, akiunganisha krosi ya Iguma Dennis.
Kwa ushindi huo, Korongo wa Kampala anafungana na Ethiopia kuongoza Kundi A, kwa pointi zake tatu kila timu. Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na timu zote zilishambuliana kwa zamu.
Kenya walianza kwa kasi kwa dakika tano wakicheza soka iliyowasisimua mashabiki wake wachache waliokuwapo uwanjani, lakini Uganda wakazinduka nao na kuanza kuwapa raha mashabiki wao kwa soka safi. Mchezo uliendelea kuwa hivyo kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu, kila upande wakicheza kwa kujiamini. Lakini sifa ziende kwa safu zote mbili za ulinzi kutokana na kucheza kwa umakini wa hali ya juu.
Kipindi cha pili timu hizo ziliporejea uwanjani, zililazimika kusimama kwa takriban dakika saba baada ya taa za uwanjani kuzimika na baada ya mafundi kutatua tatizo hilo, ndipo kabumbu likaanza tena.
Michuno hiyo itaendelea kesho kwa mechi mbili, Burundi na Somalia saa 10:00 jioni na baadaye Tanzania Bara na Sudan saa 12:00 jioni.
Uganda; Abel Dhaira/Hamza Muwonge, Iguma Dennis, Godfrey Walusimbi,Henry kalungi, Isaac isinde, Hassan Wasswa, Geoffrey Kizito, Moses Oloya, Emmanuel Okwi, Hamisi Kiiza na Brian Umony.
Kenya; Duncan Ochieng, Anthony Kimani, Abdallah Juma, Jockins Atudo, David Owino, David Ochieng, Lama Salim Mohamed, Bernard Wanyama, Humphrey Mieno, Anthony ‘Muki’ Kimani/Enock Obiero na Clifton Miheso/Paul Were.
(HABARI, PICHA KWA HISANI YA BINZUBEIRY)
MUUMIN ATIMKA TWANGA PEPETA, AANZISHA BENDI MPYA
MWIMBAJI nyota na mwenye makeke katika muziki wa dansi, Muumin Mwinjuma amejiengua katika bendi ya Twanga Pepeta International na kuanzisha bendi mpya ya Victoria Sound.
Mwinjuma alitangaza uamuzi wake huo jana alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam.
Kiongozi huyo wa zamani wa bendi ya Double M alisema amepanga kuisuka vyema bendi yake hiyo mpya ili iwe tishio hapa nchini.
Mwanamuziki huyo alisema amepanga kwenda nchini Kenya kwa ajili ya kusaka wanamuziki nyota na mahiri watakaounda bendi hiyo.
Alisema ameamua kufuata wanamuziki Kenya kwa vile anafahamu vyema kuwa, nchi hiyo imejaliwa kuwa na wanamuziki wengi wa Kitanzania wenye vipaji vya muziki, lakini hawafahamiki hapa nchini.
Alisema aliwahi kufanya hivyo miaka ya nyuma kwa kuwarejesha nchini Badi Bakule, Amina Ngaluma, Rashidi Mwezingo, Rashid Sumuni, Mohamed Mbale wakati alipounda bendi ya Tamtam.
“Hakuna mtu aliyekuwa anawajua kina Ngaluma, lakini walipotua Bongo kila mtu alikubali moto wao, nitafanya hivyo hivyo katika Victoria Sound,” alisema Muumin.
“Kama ilivyo kawaida yangu kwani muziki ni kazi yangu, hivyo nawaomba mashabiki wasubiri kuona yale waliyoyamisi kutoka kwangu nikiwa na bendi hii mpya, na wala haitachukua muda mrefu nitakuwa nimekamilisha kikosi kazi changu na kuwapa raha mashabiki wa muziki wa dansi nchini. Naamini nitafanikiwa kuipandisha chati bendi hii ya Victoria pamoja na kulinda jina na kipaji changu katika tasnia hii ya muziki,” alisema Muumin.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Daniel Denga alisema wanajivunia kumpata mwimbaji nyota na mwenye uwezo wa juu katika anga za muziki wa dansi hapa nchini.
“Bendi yetu ilianzishwa tangu mwaka 2007, lakini hatukuweza kufikia muafaka, hivyo naamini sasa malengo yetu yamefanikiwa na yatatimia kwa kutambua uwezo wa Muumini ni mkubwa na hana mpinzani hapa nchini,” alisema Denga.
Muumin amesema atakwenda Nairobi kwa awamu mbili, ya kwanza ni kufanya usajili na ya pili ni kwenda kuwafanyia uhamisho rasmi wanamuziki kutoka Nairobi kuja jijini Dar es Salaam.
Subscribe to:
Posts (Atom)