'
Thursday, May 2, 2013
YANGA KWA RAHA ZAO
YANGA jana ililazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pamoja na kulazimishwa sare hiyo, Yanga bado inaongoza ligi hiyo huku ikiwa imeshatwaa ubingwa, ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 26. Yanga imesaliwa na mechi moja dhidi ya Simba itakayochezwa Mei 18 mwaka huu.
Coastal Union ililianza pambano hilo kwa kasi na kulishambulia lango la Yanga mara kwa mara. Kutokana na mashambulizi hayo, kipa Saidi Mohamed wa Yanga alilazimika kufanyakazi ya ziada dakika ya 10 kupangua shuti la Pius Kisambale.
Dakika mbili baadaye, Yanga ilijibu shambulizi hilo kupitia kwa Jerry Tegete, ambaye alifunga bao la kwanza kwa shuti kali. Tegete alifunga bao hilo kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Nizar Khalfan.
Coastal nusura isawazishe wakati Selemani Kassim Selembe alipopewa pasi akiwa ndani ya 18, lakini shuti lake lilipaa sentimita chache kwenye lango la Yanga.
Abdi Banda aliisawazishia Coastal Union dakika ya 15 kwa mpira wa adhabu baada ya beki mmoja wa Yanga kucheza rafu karibu na eneo la hatari.
Joseph Mahundi nusura aiongezee Coastal bao la pili dakika ya 43 baada ya kufyatua kiki kali kwenye lango la Yanga, lakini kipa Saidi aliiona na kuipangua.
Katika kipindi cha pili, timu zote mbili zilishambuliana kwa zamu, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake ulikuwa kikwazo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment