KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 1, 2013

MR. NICE AVUNJA UKIMYA, AJA NA CHARLIE WA KIBERA



WASWAHILI wanasema, ukimuona kobe yuko kimya, ujue anatunga sheria na kwamba kimya kingi kina mshindo mkuu.

Hivyo ndivyo anavyotaka kudhihirisha msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Nice Lucas Nkenda, maarufu kwa jina la Mr. Nice.

Msanii huyo, ambaye kwa sasa ameamua kuhamishia maskani yake nchini Kenya, anatarajia kuzindua albamu yake mpya ya Charlie wa Kibera hivi karibuni nchini humo.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha East Africa wiki hii, Mr. Nice alisema uzinduzi wa albamu hiyo unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao.

Mr. Nice alisema ameamua kuibuka na albamu hiyo kwa lengo la kuwadhihirishia mashabiki wake kwamba hajafulia ama kufilisika kama watu wengi wanavyompakazia.

Kwa mujibu wa Mr. Nice, asilimia 20 ya mapato yatakayopatikana katika onyesho la uzinduzi wa albamu hiyo, atayatoa kwa serikali ya Kenya ili yawasaidie watoto yatima na wenye matatizo nchini humo.

Msanii huyo aliyewahi kutamba katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati miaka ya mwanzoni mwa 2000, alisema si kweli kwamba amefilisika kimuziki.

Alisema madai hayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya maadui zake kwa lengo la kumdhoofisha kimuziki na kumkatisha tamaa.

"Wanaotoa madai hayo wamekuwa wakitumiwa na adui zangu. Ni vichaa. Kichaa anapokuibia nguo zake na wewe ukaamua kumkimbiza, wewe ndiye utakayeonekana kichaa,"alisema.

"Pesa kazi yake ni matumizi. Nafanyakazi kutafuta pesa, natoka jasho, nakata viuno stejini kwa ajili ya kutafuta pesa. Na hata kama nimeishiwa, sijawahi kumgongea mtu mlango kumuomba pesa," aliongeza.

Mr. Nice alisema maadui zake hao wanashindwa kumchafua kimuziki kwa sababu wanafahamu wazi kwamba muziki upo kwenye damu yake na ni kipaji alichobarikiwa na Mungu.

Msanii huyo pia alikanusha madai kwamba, amekuwa akijihusisha na uvutaji bangi na dawa za kulevya. Alisema katika maisha yake yote, hajawahi kutumia vitu hivyo au sigara.

Mr. Nice alijizolea umaarufu mkubwa alipoibuka na vibao vyake vilivyotamba kama vile ‘Kidali po’, ‘Kila mtu na demu wake’, ‘Kikulacho’, ‘Fagilia’, ‘Mbona umeniacha’, ‘Rafiki’ na ‘First Lady’.

No comments:

Post a Comment