KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 19, 2013

YANGA NG'ARING'ARI


TIMU ya soka ya Yanga jana iliichapa Simba mabao 2-0 katika mechi ya mwisho ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Wauaji wa Simba katika mechi hiyo walikuwa washambuliaji Didie Kavumbagu na Hamisi Kiiza, bao moja katika kila kipindi.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kumaliza ligi hiyo ikiwa na pointi 60 baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 55 na Simba yenye poinri 45.

Kavumbagu aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya tano ya mchezo baada ya kuuwahi mpira wa juu, kufuatia kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima.

Simba ilipata nafasi ya kusawazisha dakika ya 27 baada ya Mrisho Ngassa kuangushwa kwenye eneo la hatari na mabeki Nadir Cannavaro na Kevin Yondan, lakini mkwaju wa Mussa Mudde ulipanguliwa na Ally Mustafa ‘Barthez’ kabla ya kipa huyo kuuchupia na kuudaka.

Kiiza aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 62 baada ya kuunganisha wavuni kwa shuti la kinyumenyume mpira wa krosi uliopigwa na Simon Msuva kutoka pembeni ya uwanja.

Mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro alijikuta akijeruhiwa dakika ya 87 wakati akiwa anaamua ugomvi kati ya beki Masoud Nassor Chollo wa Simba na mshambuliaji Didier Kavumbagu wa Yanga na kutibiwa kwa dakika mbili.

No comments:

Post a Comment