KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 1, 2013

YANGA YAPANIA REKODI DARFUR



KLABU ya Yanga imetamba kuweka rekodi nyingine ya kutwaa ubingwa wa michuano ya soka ya Kombe la Kagame ugenini.

Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Abdalla Bin Kleb alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, tayari Kocha Ernest Brands ameshaandaa programu kwa ajili ya michuano hiyo.

"Tumepania kuweka rekodi ya kutwaa kombe la Kagame ugenini kwa mara ya tatu ndio sababu tunataka kuanza maandalizi mapema,"alisema Bin Kleb.

Aliongeza kuwa, kikosi cha Yanga kina uwezo mkubwa wa kuweka rekodi hiyo kutokana na kufanya vizuri katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.

"Tunafanya mambo yetu kwa umakini mkubwa ili tuweze kuendelea kutisha na hilo halina mjadala. Baada ya ligi kuu kumalizika tu, tutakwenda kuweka kambi mahali kwa ajili ya kujiandaa kwa Kombe la Kagame,"alisema.

Mabingwa hao wa ligi kuu msimu huu, wameweka rekodi ya kutwaa taji hilo kabla haijamalizika kutokana na kuwa na idadi kubwa ya pointi, ambazo haziwezi kufikiwa na timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo.

Yanga ilitwaa kombe la Kagame ugenini kwa mara ya kwanza 1993 nchini Uganda kabla ya kulitwaa tena 1999 nchini humo. Pia ilitwaa kombe hilo mara mbili mfululizo 2011 na 2012.

Michuano ya kombe hilo imepangwa kufanyika Juni mwaka huu katika Jimbo la Darfur nchini Sudan.

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeamua kupeleka michuano hiyo katika Jimbo la Darfur kwa lengo la kulisaidia kupata maendeleo.

CECAFA inaamini kuwa, kwa kuendesha michuano hiyo na kufanikiwa, utakuwa uthibitisho wa kurejea kwa amani katika jimbo hilo, ambalo lilikuwa likikabiliwa na vita vya mara kwa mara.

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alitembelea jimbo hilo wiki iliyopita kwa ajili ya kukagua maandalizi ya michuano hiyo, ikiwa ni pamoja na kukagua viwanja na hoteli.

Michuano hiyo imepangwa kufanyika Darfur Kaskazini na Kordofan Kusini na itadhaminiwa na Gavana wa Darfur Kaskazini, Osman Mohamed Yousef.

No comments:

Post a Comment