'
Wednesday, May 1, 2013
KOCHA MOROKO ALIPUA BOMU
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Coastal Union ya Tanga, Hemed Moroko amewataka wachezaji wa timu hiyo kujitambua na kucheza soka kwa malengo.
Akizungumza na Burudani mjini hapa mwanzoni mwa wiki hii, Moroko alisema wachezaji wanapaswa kutambua kuwa, kucheza soka ni ajira kwao, hivyo wajiepushe na vishawishi vya kuihujumu timu yao.
Moroko alisema inashangaza kuona kuwa, baadhi ya wachezaji wamekuwa wakikubali kucheza chini ya kiwango katika baadhi ya mechi kutokana na kushawishiwa kufanya hivyo na viongozi wa timu pinzani.
"Hili ni kosa kubwa kwa mchezaji kwa sababu hilo siyo lengo lake katika kucheza soka,"alisema kocha huyo, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Zanzibar.
"Mchezaji anaposajiliwa, anakuwa na kiwango bora kinachomshawishi kocha kumpa namba kwenye kikosi cha kwanza, lakini unapofika wakati wa ligi, anakubali kununuliwa na timu pinzani," alilalamika kocha huyo.
Moroko alisema kufanya vibaya kwa timu katika ligi husababisha makocha kubebeshwa lawama wakati wanaosababisha hali hiyo ni baadhi ya wachezaji.
Kocha huyo alisema wachezaji wengi wanaojihusisha na vitendo hivyo ni wale walioachwa na klabu kubwa na ndio chanzo cha kuporomoka kwa timu wanazozichezea.
“Mtatuhukumu makocha kila mara, lakini tatizo kubwa katika klabu za Tanzania ni kwamba, wanaoharibu mchezo ni wachezaji wanaokubali kuzihujumu timu zao,"alisisitiza.
Moroko alisema mdudu anayezitafuna klabu za mikoani, ni wachezaji wanaokubali kuhongwa na timu pinzani kwa maslahi yao binafsi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment