KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 10, 2013

SIMBA, YANGA KUKUTANA DARFUR

TIMU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame, inayotarajiwa kufanyika katika Jimbo la Darfur nchini Sudan.

Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye alisema kwa njia ya simu jana kutoka Nairobi, Kenya kuwa, maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo yanakwenda vizuri.

Musonye alisema Yanga itashiriki michuano hiyo ikiwa bingwa mtetezi wakati Simba itashiriki ikiwa bingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita.

Yanga imetwaa kombe hilo mara mbili mfululizo, mwaka jana na mwaka juzi wakati mashindano hayo yalipofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Musonye amezihakikishia nchi wanachama wa baraza hilo kuwepo kwa usalama wa kutosha katika Jimbo la Darfur nchini Sudan.

Musonye alisema jana kuwa, alifanya ziara katika jimbo hilo hivi karibuni na kuridhishwa na hali ya usalama.

CECAFA imepanga michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame ifanyike katika jimbo hilo kwa lengo kulisaidia kimaendeleo na pia kuimarisha amani.

"Tumechukua tahadhari zote kuhakikisha kuwa, wakati wote wa mashindano hayo kutakuwa na usalama wa kutosha kwa ajili ya timu zote,"alisema Musonye.

"Tumekutana na viongozi wa jimbo hilo na viongozi wa serikali ya Sudan na wote wametuhakikishia kuwa, maandalizi yanakwenda vizuri na usalama upo wa kutosha,"aliongeza.

Kwa mujibu wa Musonye, baraza lake linatarajia kutangaza majina ya timu zitakazoshiriki katika mashindano hayo baada ya kuwasiliana na vyama vya soka vya nchi wanachama.

No comments:

Post a Comment