'
Wednesday, May 1, 2013
KASSIM DEWJI: NIPO TAYARI KUREJEA SIMBA
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage wiki iliyopita alikaririwa akisema kuwa, anatarajia kuisuka upya kamati ya usajili kwa kuwarejesha kundini baadhi ya wanachama waliotoa mchango mkubwa kwa klabu hiyo. Miongoni mwa wanachama wanaotajwa kurejeshwa Simba ni katibu mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Kassim Dewji. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, kiongozi huyo wa zamani wa Simba anaelezea msimamo wake kuhusu taarifa hizo.
SWALI: Kwa muda mrefu sasa umekuwa kimya kuhusu masuala ya soka, hasa katika klabu yako ya Simba. Unaweza kueleza ni kwa sababu gani umejiweka pembeni na Simba?
JIBU: Ni kweli nipo kimya kuhusu Simba, lakini sababu kubwa ni kwamba sina nafasi yoyote katika uongozi. Nimebaki kuwa mwanachama wa kawaida wa Simba nikiangalia mambo yanavyokwenda.
SWALI: Je, umebaini kuwepo kwa kasoro yoyote ndani ya Simba iliyosababisha timu ifanye vibaya katika msimu huu wa ligi?
JIBU: Sio siri kwamba kikosi chetu msimu huu hakikusajiliwa vizuri. Kinapaswa kufumuliwa na kusukwa upya ili kiweze kutoa ushindani na kufanya vizuri msimu ujao. Tusipokuwa makini katika hili, hatuwezi kufika mbali katika ligi.
SWALI: Mbali na usajili kutokuwa mzuri, unadhani ni sababu zipi zingine zilizosababisha timu ivurunde msimu huu?
JIBU: Baadhi ya wachezaji, uwezo wao ni mdogo na wengine wamejenga kiburi kwa viongozi na benchi la ufundi. Wanapopewa maelekezo na kocha, wanakuwa wabishi kutekeleza na kujiona mastaa. Wachezaji wa aina hii hawapaswi kuendelea kuwemo ndani ya Simba.
Tatizo lingine lililoigharimu Simba ni wachezaji kushindwa kucheza kwa kujituma uwanjani, hasa inapotokea malipo yao ya mishahara yamechelewa. Hili ni tatizo sugu. Sidhani kama yupo kiongozi anayependa kuchelewesha mishahara ya wachezaji kwa makusudi. Kila kiongozi anapenda kuona mchezaji anapata haki zake anazostahili.
SWALI: Hivi karibuni ulitokea mvurugano ndani ya Simba na kudaiwa kwamba, baadhi ya viongozi wa zamani, ukiwemo wewe wamekuwa wakihujumu timu. Je, kuna ukweli wowote kuhusu tuhuma hizi?
JIBU: Kwa watu wanaonifahamu vyema, hakuna anayeweza kupinga kwamba mimi ni Simba damu. Naipenda Simba kwa moyo wangu wote. Kamwe siwezi kuihujumu kwa njia yoyote. Nimepata umaarufu kwa sababu ya Simba.
Nimeshawahi kuiongoza Simba miaka ya nyuma na kuiletea mafanikio makubwa, hivyo kuisaliti ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa kwangu. Kama ni kugombea uongozi, ninao uwezo wa kufanya hivyo na wanachama ndio watakaoamua.
Hao wanaodai kwamba nimekuwa nikiihujumu Simba, nadhani wamekosa la kuzungumza na wanataka kuficha udhaifu wao. Lengo lao ni kunichafua. Kamwe siwezi kuwa na mawazo ya kuihujumu Simba ili ifungwe. Pia sina mawazo ya kutaka uongozi kwa sasa kwa vile tunao viongozi waliochaguliwa kikatiba.
Nawaomba watu wanaonihusisha na vitendo hivyo waache mara moja kwa sababu huko ni kurudisha nyuma maendeleo ya klabu yetu, ambayo ina historia kubwa barani Afrika.
SWALI: Uliupokeaje uamuzi wa makamu mwenyekiti wa zamani, Geofrey Nyange 'Kaburu' na mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope kujiuzulu?
JIBU: Siwezi kusema lolote kwa sasa kuhusu uamuzi wao huo zaidi ya kuwataka wanachama wa Simba kuwa watulivu. Wanapaswa kuivumilia timu yao, ambayo inaundwa na vijana wengi wachanga. Nina hakika vijana hawa wakikaa pamoja kwa miaka miwili, Simba itakuwa na timu tishio sana katika ligi.
Nina hakika baada ya ligi ya msimu huu kumalizika, uongozi utachukua hatua za kukiimarisha zaidi kikosi hicho na kukifanya kitishe msimu ujao. Ni suala la kukipa muda tu.
SWALI: Hivi karibuni, Rage alikaririwa akisema kuwa, anafikiria kuunda upya kamati ya usajili na upo uwezekano mkubwa wa wewe kurejeshwa kwenye kamati hiyo. Unasemaje kuhusu taarifa hizi?
JIBU: Sijapata taarifa zozote kuhusu jambo hilo, lakini nipo tayari kuitumikia Simba wakati wowote. Na iwapo itakuwa hivyo, naahidi kwamba nitafanyakazi hiyo kwa moyo wangu wote kwa lengo la kuhakikisha kuwa, Simba inarejesha hadhi yake na kupata mafanikio makubwa zaidi.
SWALI: Ungependa kutoa ushauri gani kwa wanachama wa Simba, ambao wamekuwa wakitaka uongozi wa sasa uondoke madarakani?
JIBU: Nawaomba wawe na subira na uvumilivu. Wasubiri kuona hatua zitakazochukuliwa na uongozi katika kurekebisha matatizo yaliyojitokeza msimu huu.
Kama wana mawazo, maoni ama ushauri kwa uongozi, wasubiri mkutano ulioitishwa Julai mwaka huu. Hakuna sababu ya kushinikiza kufanyika mambo, ambayo hayawezekani.
SWALI: Ligi kuu inatarajiwa kumalizika Mei 18 kwa mechi saba, ikiwemo ya Simba na Yanga. Nini mtazamo wako kuhusu mechi hii?
JIBU: Kama tutaendelea kuwa watulivu na wenye umoja kama ilivyo sasa, sioni kipi kinachoweza kutukwamisha kuifunga Yanga. Ni lazima tulinde heshima yetu kwa Yanga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment