KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 9, 2013

KAVUMBAGU KUFUNGASHIWA VIRAGO YANGA, BAHANUZI AKALIA KUTI KAVU




KLABU ya Yanga imepanga kuwaacha wachezaji wake kadhaa nyota kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kutokana na kushuka kwa viwango vyao vya soka.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, mpango wa kuwaacha nyota hao pia utawahusu baadhi ya wachezaji wa kigeni.

Kwa mujibu wa habari hizo, miongoni mwa nyota wa kigeni watakaoachwa msimu ujao ni pamoja na mshambuliaji Didier Kavumbagu kutoka Burundi.

Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, tayari benchi la ufundi la Yanga limeshaanza kuandaa ripoti ya ushiriki wa kila mchezaji katika msimu huu kabla ya kuikabidhi kwa uongozi.

Tayari baadhi ya wachezaji nyota wa Yanga wameshaanza kupatwa na hofu baada ya kuwepo kwa tetesi kuhusu kuachwa kwao.

Kavumbagu alisajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Vital'O ya Burundi na alikuwa mmoja wa washambuliaji wa kutegemewa kabla ya kiwango chake kuonekana kushuka katika mzunguko wa pili.

Mshambuliaji huyo mrefu na mwenye umbo lililojaa, alimudu kumweka benchi Jerry Tegete katika mzunguko wa kwanza kabla ya kibao kugeuka mwishoni mwa mzunguko wa pili.

Hivi karibuni, Kavumbagu alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akilalamika kuwa, baadhi ya wachezaji wenzake wamempiga 'juju' kwa lengo la kushusha kiwango chake.

"Uongozi unataka timu iwe na washambuliaji wenye uwezo wa kufunga mabao katika michuano ya Kombe la Kagame na klabu bingwa Afrika,"kilisema chanzo cha habari kutoka ndani ya Yanga.

Wachezaji wengine wanaotajwa kukalia kuti kavu ni pamoja na mshambuliaji Saidi Bahanuzi, ambaye alisajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Mtibwa Sugar.

Bahanuzi alionekana kuwakera mashabiki wa Yanga wakati timu hiyo ilipomenyana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana na kukosa mabao mengi.

No comments:

Post a Comment