KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, May 6, 2013

SIMBA YAVUTA KASI



SIMBA jana ilizinduka katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 3-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameiwezesha Simba kuchupa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 42 baada ya kucheza mechi 26 na hivyo kuiondoa kwenye nafasi hiyo, Kagera Sugar.

Mshambuliaji Amri Kiemba aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 14 baada ya kumalizia mpira uliopigwa na Felix Sunzu, aliyemtoka beki, Ernest wa Ruvu Shooting.

Ruvu Shooting nusura isawazishe dakika ya 26 wakati Saidi Madega alipoingia na mpira ndani ya 18 na kufumua shuti lililowababatiza mabeki wa Simba.

Abdalla Seseme nusura aifungie Simba bao dakika ya 36 baada ya kupewa pasi akiwa ndani ya eneo la hatari la Ruvu Shooting, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango.

Ruvu Shooting ilisawazisha dakika ya 52 kwa bao lililofungwa na Abdulrahman Mussa kwa shuti lililomshinda kipa Abel Dhaira wa Simba.

Bao la pili la Simba lilifungwa na Christopher Alex baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Ruvu Shooting kabla ya Ismail Mkoko kuongeza la tatu dakika ya 89.

No comments:

Post a Comment