'
Wednesday, May 1, 2013
MTANZANIA AOMBEWA ITC NORWAY
SHIRIKISHO la Soka la Norway (NFF) limetuma maombi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ya kupatiwa hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) mchezaji Godfrey Mlowoka wa Tanzania.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, NFF inamuombea hati hiyo Mlowoka ili aweze kujiunga na klabu ya Ekne IL ya nchini humo akiwa mchezaji wa ridhaa, ambapo klabu yake ya zamani imetajwa kuwa ni Sadani.
Wambura alisema TFF inayafanyia kazi maombi hayo na baada ya taratibu zote kukamilika, hati hiyo ya uhamisho itatumwa nchini Norway.
Wakati huo huo, Wambura amesema mikoa 18 kati ya 27 ya kimpira imeshapata mabingwa kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa itakayoanza Mei 12 mwaka huu chini ya usimamizi wa TFF.
Wambura alisema jana kuwa, timu tatu za juu katika Ligi hiyo ya mabingwa zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014).
Alisema ligi ya FDL inazo jumla ya timu 24, ambapo tatu katika ligi hiyo ni zile zilizoshuka daraja msimu huu. Timu hizo ni Moro United ya Dar es Salaam, Small Kids ya Rukwa na Morani FC ya Manyara.
Aliwataja mabingwa waliopatikana hadi sasa, mikoa yao kwenye mabano kuwa ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).
Wengine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).
Wambura alisema kila klabu inatakiwa kulipa ada ya ushiriki, ambayo ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika ligi ya mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho.
"TFF inapenda kusisitiza kuwa, hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo,"alisema Wambura.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment