'
Friday, May 10, 2013
MSIBA MZITO MAN UNITED
LONDON, England
KLABU ya Manchester United ya England imethibitisha kuwa, Kocha wake mkuu, Sir Alex Ferguson atastaafu mwishoni mwa msimu huu.
Fergie mwenye umri wa miaka 71, anaondoka Old Trafford akiwa na rekodi ya kutwaa mataji 13 ya ligi kuu ya England.
Kocha huyo raia wa Scotland alisema jana kuwa, uamuzi wake wa kustaafu ni kati ya mambo aliyokuwa akiyafikiria na haikuwa rahisi.
“Ilikuwa muhimu kwangu kuiacha taasisi ipo imara na muonekano mzuri na naamini nimefanya hivyo,"alisema kocha huyo kipenzi cha mashabiki wa Manchester United.
"Ubora wa kikosi kilichotwaa ubingwa wa ligi hii na uwiano wa umri uliopo, wapo fiti kuendeleza mafanikio katika kiwango cha juu na kuzingatia mpango wa muda mrefu wa kukuza vijana," aliongeza kocha huyo na kusisitiza kuwa, klabu itazidi kuendelea kung'ara.
“Vifaa vyetu vya mazoezi ni kati ya vilivyo bora katika ulimwengu wa michezo na nyumbani kwetu Old Trafford panapendeza na kuchukuliwa kati ya viwanja bora duniani.
“Kwa upande mwingine, nina furaha kupewa majukumu yote ya mkurugenzi na balozi wa klabu. Kwa shughuli hizi, pamoja na manufaa yangu mengine mengi, natazama mbele kwa baadaye," alisema.
Ferguson alisema anaishukuru familia yake kwa upendo wao kwake na kumuunga mkono kwa kipindi chote alichokuwa akiitumikia Manchester United akiwa kocha.
"Mke wangu Cathy amekuwa ufunguo muhimu katika kazi yangu kwa uvumilivu na kunipa moyo. Maneno hayatoshi kuelezea hii ina maana gani kwangu,"alisema kocha huyo anayependa kutafuna 'bazoka' muda wote wa mchezo.
“ Kwa wachezaji wangu na wafanyakazi, waliopita na waliopo, napenda kuwashukuru wote kwa kucheza katika kiwango cha juu na juhudi zilizosaidia kutwaa mataji mengi ya kukumbukwa. Bila ya mchango wao, historia ya klabu hii isingefika ilipo,"alisema.
“Katika miaka yangu ya mwanzo, nikisaidiwa na bodi na hasa Sir Bobby Charlton, walinifanya nijiamini na kupata muda wa kuijenga klabu ya soka, kuliko kuwa timu ya mpira.
“Zaidi ya muongo mmoja uliopita, familia ya Glazer ilinipa ofa za kuweza kuiongoza Manchester United kwa uwezo wangu bora na nilibahatika kufanya kazi na mtendaji mkuu mwenye kipaji na kuaminika, David Gill. Ukweli wote wamenifurahisha.
“Nawashukuru mashabiki kwa kutuunga mkono kwa miaka mingi, kumekuwa na msisimko wa kina. Imekuwa heshima kubwa kupata bahati ya kuongoza klabu yenu na kuwa kipenzi cha Manchester United.”
Mbali ya kutwaa mataji 13 ya ligi, Sir Ferguson pia aliiongoza Manchester United kutwaa vikombe viwili vya Ulaya, mataji matano ya FA na vikombe vinne vya Kombe la Ligi.
Mechi ya mwisho kuwaongoza Mashetani Wekundu itakuwa dhidi ya West Bromwich itakayochezwa Mei 19 mwaka huu, siku ambayo msimu wa ligi kuu England utafungwa.
Kustaafu kwa kocha huyo kunatoa nafasi kubwa kwa mikoba yake kurithiwa na aidha Davis Moye wa Everton au Jose Mourinho wa Real Madrid ya Hispania.
Makocha hao wawili ndio chaguo namba moja la Ferguson kuwaachia mikoba ya kuinoa Manchester United, ambayo ina mashabiki lukuki kote duniani.
Tayari Moyes ameshakaririwa na baadhi ya vyombo vya habari vya England akiwaaga mashabiki wa klabu hiyo huku kukiwa na tetesi kubwa Mourinho anataka kurudi katika klabu yake ya zamani ya Chelsea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment