KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 16, 2013

SHOMARI KAPOMBE: SINA MPANGO NA YANGA


JINA la Shomari Kapombe kwa sasa limetawala katika vinywa vya mashabiki wengi wa soka nchini. Ni kutokana na umahiri wake wa kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani na pia uwezo wake wa kupanda mbele kusaidia mashambulizi. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu, beki huyo anaelezea mambo mbalimbali kuhusu maisha yake kisoka.

SWALI: Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na taarifa kwamba uko mbioni kuondoka katika kikosi cha Simba na kujiunga na mojawapo kati ya timu za Yanga na Azam FC. Je, kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizi?

JIBU: Kusema ule ukweli, kwa sasa sina mpango wowote wa kuondoka Simba na kujiunga na Yanga au Azam. Ninachokifikiria kwa sasa ni kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi. Tayari kuna klabu mbili, moja ya Uholanzi na nyingine ya England zimeshaonyesha nia ya kunifanyia majaribio. Hicho ndicho ninachokifikiria kwa sasa.

Lengo langu ni kuwa na maisha mazuri zaidi kutokana na kucheza soka. Nataka kutumia kipaji na uwezo wangu kunufaika kisoka. Naushukuru sana uongozi wa Simba kwa kunilea vizuri na kunifikisha hapa nilipo hadi nikapewa unahodha msaidizi wa Simba.

Na kwa kuweka mambo wazi, sijawahi kufanya mazungumzo yoyote na viongozi wa Yanga au Azam kuhusu kujiunga nazo. Nawahakikishia viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba kwamba nitaendelea kuwa mchezaji wao hadi mipango yangu ya kwenda nje itakapofanikiwa.Nawaomba watu wanaovumisha habari hizo waache mara moja.

SWALI: Ni klabu zipi ambazo zimekuomba ukafanye majaribio ya kucheza soka ya kulipwa?

JIBU: Ofa ya kwanza inatoka kwa klabu ya Sunderland ya England na nyingine imetoka Uholanzi, lakini sina hakika na jina la timu. Na nitakwenda huko baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu na kwa baraka za uongozi wa Simba.

SWALI: Kwa sasa wewe na wachezaji wenzako wa Simba mnajiandaa kucheza na Yanga katika mechi ya mwisho ya ligi kuu itakayochezwa Mei 18 mwaka huu huku baadhi ya wachezaji wenu nyota wakiwa wamesimamishwa. Unadhani wewe na wachezaji wenzako chipukizi wanaopewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza hivi sasa mtaweza kuhimili mechi hiyo?

JIBU: Kuwepo kwa wachezaji wengi chipukizi kwenye kikosi chetu kumeleta changamoto kubwa na pia kuongeza ushindani wa namba kwa vile kila mchezaji anacheza kwa kujituma. Lengo la kila mmoja ni kuendelea kuwemo kwenye kikosi cha Simba msimu ujao.

Hata mimi nimeshaanza kupata wasiwasi kuhusu namba yangu kwa sababu hawa vijana wameanza kunitisha na kunilazimisha nifanye mazoezi kwa bidii zaidi ili kujihakikishia namba. Ni vijana wazuri na wenye mwelekeo mzuri si kwa Simba tu, bali hata Taifa Stars.

Kuhusu mechi yetu na Yanga, sina wasiwasi nayo kwa sababu naamini tunacho kikosi kizuri. Ninachowaomba mashabiki wetu ni kujenga imani kwa timu yao na kuamini inao uwezo wa kufanya vizuri.

Kwa upande wa wachezaji waliosimamishwa, hilo siwezi kulizungumzia
kwa sababu ni masuala ya kiuongozi na kiutawala, mimi ni mwajiriwa tu kama wachezaji wengine. Isipokuwa napenda kuwahakikishia mashabiki wetu kwamba wasiwe na wasiwasi.

SWALI: Kwa maana hiyo unataka kusema kwamba, kikosi chenu kinachoundwa na chipukizi wengi kinao uwezo wa kuifunga Yanga?

JIBU: Uwezo huo upo ndio sababu umeweza kuona katika mechi zetu za hivi karibuni tumekuwa tukiibuka na ushindi. Hao wanaotamba kuwa Yanga itaifunga Simba idadi kubwa ya mabao, wanakosea kwa sababu mchezo wa soka hauko hivyo. Mchezo wa soka unaweza kutoa matokeo tofauti na inavyotabiriwa.

SWALI: Una maoni gani kuhusu uamuzi wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen kuunda kikosi cha pili cha timu hiyo?

JIBU: Binafsi nimefarijika sana kutokana na uamuzi wake huo kwa sababu utaongeza ushindani wa namba na kuwafanya wachezaji walioko Taifa Stars kuwa na bidii zaidi ili wasipokonywe namba na wale walioko kikosi cha pili.

SWALI: Unapenda kuwaeleza nini mashabiki wa soka nchini?

JIBU: Nawaomba waendelee kuiunga mkono timu yao ya Taifa (Taifa Stars) ili hatimaye iweze kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na zile za dunia.

No comments:

Post a Comment