'
Thursday, May 23, 2013
JAYDEE: NITASAMBAZA ALBAMU YANGU KWA KUTUMIA MAX MALIPO
MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura 'JayDee' amesema anatarajia kuuza albamu yake mpya ya Nothing but the Truth kwa kutumia wakala wa Max Malipo.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, JayDee alisema amefikia uamuzi huo kwa lengo la kudhibiti wizi wa kazi za sanaa na pia kuboresha soko la kazi zake.
JayDee alisema Max Malipo itaitumia Kampuni ya Posta yenye ofisi zake kote nchini kwa ajili ya kusambaza albamu hiyo.
"Naamini kwa kutumia wakala wa Max Malipo, albamu yangu itaweza kupatikana kote nchini na kwa muda mfupi,"alisema msanii huyo aliyewahi kushinda tuzo kadhaa za muziki nchini.
"Nataka nijaribu na kujifunza, nikifanya hivi itakuwaje au nifanyeje ili kuboresha soko la muziki wangu,"aliongeza.
Kwa mujibu wa msanii huyo, onyesho la uzinduzi wa albamu yake hiyo mpya limepangwa kufanyika Mei 31 mwaka huu kwenye ukumbi wa Nyumbani Lounge.
JayDee alisema katika onyesho hilo, atamshirikisha msanii Juma Kassim 'Nature', mwanamuziki mkongwe nchini, Hamza Kalala, Grace Matata na Joseph Haule 'Profesa Jay', ambaye ameshirikiana naye kuimba kibao cha Joto la hasira.
Msanii huyo anayemiliki bendi ya Machozi alisema, ameamua kuandaa onyesho la uzinduzi wa albamu hiyo kwa ajili ya kusherehekea kutimiza miaka 13 katika fani ya muziki.
Alisema katika kipindi hicho, ameweza kujifunza mambo mengi kuhusu muziki ikiwa ni pamoja na kupata uzoefu mkubwa wa fani hiyo.
Mwanadada huyo alisema alisimama kwa muda mrefu kutoa nyimbo mpya kutokana na kuelekeza nguvu zake zaidi katika bendi yake ya Machozi.
"Unajua usipotoa nyimbo kwa muda mrefu, si rahisi kupata maonyesho. Lakini kwa upande mwingine, bendi ina manufaa makubwa zaidi katika muziki,"alisema.
JayDee alikiri kuwa, muziki wa kizazi kipya kwa sasa umekuwa na mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira nyingi kwa vijana na kuwabadilisha kimaisha.
Hata hivyo, alisema soko la muziki huo lilikuwa zuri miaka ya nyuma kutokana na kuwepo kwa wasanii wachache, tofauti na sasa, ambapo idadi ya wasanii wa muziki huo imekuwa kubwa na hivyo kusababisha mauzo yapungue.
Aliitaja changamoto nyingine inayowakabili wasanii wa muziki huo kuwa ni kukithiri wa wizi wa kazi za sanaa, ambapo baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiendelea kudurufu nyimbo za wasanii na kutengeneza albamu bila ridhaa yao huku wengine wakifanya biashara ya kuingiza nyimbo za wasanii kwenye simu za mkononi bila kuwalipa chochote.
"Ninachowaomba watanzania ni kuendelea kuwaunga mkono wasanii wa muziki huu ili kuongeza ajira kwa vijana,"alisema msanii huyo mkongwe wa muziki wa kizazi kipya.
Pamoja na kupatikana kwa mafanikio hayo, JayDee alisema bado maonyesho yanayofanywa na wasani wa Tanzania katika baadhi ya nchi za Ulaya ni ya kiwango cha chini.
Alisema mara nyingi maonyesho hayo yamekuwa yakihudhuriwa na watanzania wachache wanaoishi katika nchi hizo za Ulaya, ama raia wengine kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda na zile zinazozungumza lugha ya kiswahili.
"Ninachoweza kusema ni kwamba, faida pekee wanayoipata wasanii wa Tanzania wanapokwenda Ulaya ni kusafiri, kujifunza mambo tofauti na kukutana na watu wengi,"alisema.
JayDee alisema binafsi amekuwa akitembelea baadhi ya nchi za Ulaya kwa ajili ya shughuli zake binafsi na ni mara chache amewahi kualikwa kufanya maonyesho.
Msanii huyo alisema amefurahi kukamilisha ndoto yake ya kurekodi wimbo na mwanamuziki mkongwe wa Zimbabwe, Oliver Mutukuzi na kwamba kwa sasa, ndoto nyingine aliyonayo ni kurekodi na mwanamuziki Dr. Dre wa Marekani.
Msanii huyo alisema pia kuwa, ndoto nyingine aliyonayo katika maisha yake ni kuanzisha kituo cha redio, ambacho kitakuwa kikifanyakazi kwa ajili ya watanzania wote.
Aliongeza kuwa, yupo tayari kutoa mchango wa mawazo kwa wasanii wanaochipukia wa muziki huo kuhusu nini la kufanya kwa lengo la kuendeleza vipaji vyao, lakini si kuwapa pesa kwa vile hana uwezo huo kwa sasa.
WASIFU WA JAYDEE
ALIZALIWA: Juni 15, 1979
KAZI: Mwanamuziki
NDOA: Ameolewa na mtangazaji wa redio, Gardner Habbash
TUZO ALIZOSHINDA: Msanii bora wa kike wa R&B (2002)
Albamu bora ya R&B (2004)
Video bora ya msanii wa kike nchini Afrika Kusini
(2005)
Wimbo bora wa mwaka wa Tanzania (2008)
Mwimbaji bora wa kike (2010)
Mwimbaji bora wa kike (2012)/
Mwimbaji bora wa kike anayechipukia Afrika Mashariki (2003, 2004 na 2005).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment