KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 1, 2013

YANGA KUIENDEA SIMBA PEMBA



UONGOZI wa klabu ya Yanga umepanga kuipeleka timu hiyo kambini kisiwani Pemba kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya mwisho ya ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa, Yanga itakwenda Pemba baada ya mchezo wao mwingine wa ligi hiyo dhidi ya Coastal Union uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano kati ya Yanga na Simba limepangwa kuchezwa Mei 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tayari Yanga imeshatwaa taji hilo kutokana na kuwa na pointi 56 baada ya kucheza mechi 24, ambazo hakuna timu nyingine inayoweza kuzifikia.

Simba imeshapoteza matumaini ya kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo na sasa inawania nafasi ya nne, ikichuana vikali na Kagera Sugar.

Kwa mujibu wa habari hizo, Yanga itakwenda Pemba kutokana na kupokea maombi mengi kutoka kwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wanaoishi visiwani humo.

"Wanachama wetu walioko Pemba na Zanzibar kwa ujumla wametuomba tukaweke kambi huko kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Simba na sisi tumewakubalia. Timu itakwenda huko baada ya mchezo wetu dhidi ya Coastal Union," kilisema chanzo hicho cha habari.

Uamuzi wa Yanga kuweka kambi Pemba pia umetokana na ombi la Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ernie Brandts kutaka timu ikaweke kambi nje ya mkoa wa Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment