'
Sunday, May 5, 2013
RATIBA RCL KUPANGWA J'NNE, LIGI KUANZA MEI 12
Upangaji ratiba (draw) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) uliokuwa ufanyike juzi (Mei 3 mwaka huu), sasa utafanyika Jumanne (Mei 7 mwaka huu) na ligi hiyo itaanza Mei 12 mwaka huu kama ilivyopangwa.
Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Mei 5 mwaka huu) kujadili maandalizi ya ligi hiyo, yakiwemo maombi ya baadhi ya mikoa ambayo haijamaliza yao kutaka RCL isogezwe mbele.
Kamati ya Mashindano chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ilipitia maombi hayo na kuangalia athari ambazo zinaweza kujitokeza huko mbele iwapo RCL itasogezwa mbele.
Baadhi ya athari iwapo RCL itasogezwa mbele ni timu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutopata muda wa kufanya usajili wa wachezaji kwa msimu mpya.
Hivyo draw hiyo itakayofanyika saa 6 mchana itahusisha mikoa ambayo tayari imemaliza ligi na kuwasilisha majina ya mabingwa wao. Mabingwa ambao wamewasilishwa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).
Mingine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).
Ada ya ushiriki ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.
Mikoa iliyoshindwa kuwasilisha mabingwa wake ni Dodoma, Geita, Iringa, Lindi, Manyara, Mtwara, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Tanga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment