KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 5, 2013

BOCCO, MWANTIKA WAIPONZA AZAM



AZAM jana ilitolewa kiume katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho baada ya kuchapwa mabao 2-1 na FAR Rabat ya Morocco katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat.

Kipigo hicho kimeifanya Azam itolewe kwa ushindi wa jumla wa idadi hiyo ya mabao, kufuatia timu hizo kutoka suluhu katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam itabidi ijilaumu kutokana na mshambuliaji wake, John Bocco kukosa adhabu ya penalti dakika ya 85, ambayo ingeiwezesha kupata sare na kusonga mbele katika michuano hiyo.Shuti la Bocco liligonga mwamba wa juu wa goli.

Mbali na kukosa penalti, Azam ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 baada ya beki wake, David Mwantika kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya mchezaji wa FAR Rabat.

Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya sita lililofungwa na Bocco kwa mpira wa adhabu baada ya beki mmoja wa FAR Rabat kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Wamorocco walisawazisha bao hilo dakika sita baadaye kupitia kwa Abdelrahim Achchakir kwa mkwaju wa penalti baada ya Mwantika kumchezea rafu mbaya mchezaji mmoja wa FAR Rabat.

FAR Rabat nayo ilipata pigo dakika ya 35 baada ya beki wake, Achchakir kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Brian Umony.

Bao la pili la FAR Rabat lilifungwa na Mustafa Allaoui dakika ya 42 kwa shuti la mpira wa adhabu la umbali wa mita 25 na kumpita kipa Mwadini Ally.

Waziri Salum wa Azam naye alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 75 baada ya kumchezea rafu Kaddioiu Yuossef.

No comments:

Post a Comment