KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 7, 2012

WEMA ATUMIA MIL 29/- KUTENGENEZA FILAMU







MSANII nyota wa filamu nchini, Wema Sepetu amesema ametumia zaidi ya sh. milioni 29 kwa ajili ya kuandaa na kukamilisha filamu yake mpya inayojulikana kwa jina la Super Star.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Wema alisema filamu hiyo imewashirikisha wasanii mbalimbali nyota nchini, wakiwemo wasanii wa muziki wa kizazi kipya.
Aliwataja baadhi ya wasanii hao kuwa ni Hemed Mlela, Barnaba, Khaleed Mohamed (TID), Mr. Blue, Judith Wambura (Lady JayDee) na Jacob Steven (JB).
Kwa mujibu wa Wema, hii ni filamu yake ya kwanza baada ya kuamua kuwa mtayarishaji na muongozaji wa filamu.
Alisema amelazimika kutumia kiasi kikubwa cha pesa kutengeneza filamu hiyo kutokana na kuwashirikisha wasanii wengi nyota na pia kutumia maeneo mengi ya bei mbaya.
“Unajua hadi sasa nimeshacheza movi nyingi sana, nikaona kwa nini na mimi nisianze kutengeneza filamu zangu mwenyewe. Niliona kama wengine wameweza, kwa nini mimi nisiweze,”alisema Wema, ambaye aliwahi kuwa mrembo wa Tanzania wa mwaka 2006.
Katika filamu hiyo, awali Wema ameigiza kama mwanamke wa hali duni kimaisha, anayeishi kijijini. Akiwa huko, anashawishiana na rafiki yake na kuamua kwenda mjini kutafuta maisha.
Wakiwa mjini, rafiki yake ndiye anayeanza kufanikiwa kimaisha na kujiita Super Star. Kila Wema anapomuomba msaada rafiki yake huyo, anamtolea nje.
Hatimaye, Wema naye anafanikiwa kimaisha na kuwa msanii maarufu, kiasi kwamba kila anapokwenda, anafuatwa na lundo la waandishi wa habari.
Kutokana na kufanikiwa huko kimaisha, Wema anaamua kumshiti mpenzi wake, Hemed aliyemsaidia wakati anatoka kijijini kwao. Naye akaanza kujiona ni Super Star.
Je, ni kwa nini Wema amekuwa akitawala vyombo mbalimbali vya habari kila kukicha?
Akijibu swali hilo, Wema alisema nyota yake inang’ara ndio sababu kila anachokifanya ama kukisema, kimekuwa kikipewa uzito na vyombo vya habari.
“Sifanyi yote hayo kwa makusudi, hapana. Kwamba kila nikiingia sehemu nataka nionekane, hakuna kitu kama hicho na wala sipendi,”alisema Wema.
“Mimi huwa sipendi drama. Vyote hivyo vinatokea kwa malengo maalumu. Bila ya vyombo vya habari, nisingeweza kufahamika kiasi hiki,” aliongeza.
“Tatizo ni kwamba kila ninapokwenda ama kila ninachokifanya, kuna watu wananifuatilia,”alisisitiza na kuongeza kuwa, watu wengi wamekuwa wakimtafsiri tofauti na alivyo.
Akizungumzia maisha yake binafsi, Wema alisema anakipenda sana chumba anacholala na kitandani kwake, yupo mdoli, ambaye amemuelezea kuwa ndiye rafiki yake mkubwa. Mbali na kukipenda chumba chake cha kulala, Wema alisema nyumbani kwake anazo nywele bandia za kila aina, jozi kibao za viatu na vipodozi vya kila aina.
Mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto pia alisema anapenda sana kupika na ni hodari wa kupika vyakula vya aina mbalimbali.
Hivi karibuni, Wema alivikwa pete ya uchumba na mwanamuziki wa bendi ya Machozi, Mwinyi wakati wa onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa klabu ya Maisha.
Tukio hilo lilivuta hisia za watu wengi, hasa ikizingatiwa kuwa hii ni mara ya pili kwa Wema kuvikwa pete ya uchumba. Awali, alivikwa pete kama hivyo na msanii Naseeb Abdul ‘Diamond’, lakini uchumba huo ulikufa katika mazingira ya kutatanisha.
Wema alizaliwa Septemba 28, 1988. Alianza kuwa maarufu mwaka 2006 baada ya kutwaa taji la mrembo wa Tanzania na kuiwakilisha nchi katika shindano la dunia.
Wema ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto wanne wa Mzee Abraham Sepetu. Alianza elimu ya msingi hadi sekondari katika shule moja tu iitwayo 'Academic International' iliyopo maeneo ya Mikocheni, Dar es Salaam.
Kipaji zaidi cha Wema kiligundulika katika sanaa ya filamu, ambapo alifanikiwa kucheza vema katika filamu ya A Point of No Return akishirikiana na mchezaji filamu maarufu wa Kitanzania, marehemu Steven Kanumba.
Mwanadada huyo amekuwa akihusishwa kimapenzi na wasanii mbalimbali maarufu nchini, wakiwemo Mr.Blue, Charlz Baba, Kanumba, James Fredrick na Diamond.

No comments:

Post a Comment