KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 7, 2012

TEVEZ: Sijutii kutemwa Argentina

BUENOS AIRES, Argentina
MSHAMBULIAJI Carlos Tevez wa klabu ya Manchester City ya England amesema hajutii kuachwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Argentina.
Hata hivyo, Tevez amesema yupo tayari kurejea kwenye kikosi hicho iwapo ataitwa na Kocha Alejandro Sabella.
Tevez hajaitwa kwenye kikosi cha Argentina tangu kumalizika kwa michuano ya Copa America, ambapo mshambuliaji huyo alikosa penalti muhimu na kuifanya itolewe hatua ya robo fainali.
Kutemwa kwa Tevez kwenye kikosi hicho kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na msuguano uliojitokeza kati yake na benchi la ufundi la Manchester City.
Msuguano huo ulisababisha Tevez atumie miezi kadhaa akiwa katika mji wa Buenos Aires, Argentina kabla ya kurejea England na kucheza mechi za mwisho za ligi kuu ya nchi hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari kwenye tafrija iliyoandaliwa na klabu yake ya zamani ya Boca Juniors, Tevez alisema hakukerwa na uamuzi huo wa Sabella na kuwaona wachezaji wenzake wakiwa wamevaa uzi wa rangi nyeupe na bluu.
“Sijutii kutokuwemo kwenye kikosi cha Argentina. Nilifurahia zaidi kuwaona wenzangu nikiwa nje ya uwanja,”alisema.
Tevez alikuwa akijibu swali aliloulizwa alijisikiaje kuiona timu yake iliibamiza Ecuador mabao 4-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Nilivutiwa na timu, lakini kwa sasa sitaki niwemo kikosini. Bila shaka wakati nitakapoitwa, nitajiunga na timu,”alisema.
Akizungumzia klabu yake ya Boca Juniors, Tevez alisema angependa kuona anastaafu kucheza soka katika klabu hiyo, ambayo aliiwezesha kutwaa mataji manne akiwa kwenye kikosi cha kwanza. “Lengo langu kubwa ni kustaafu soka hapa nikiwa na jezi ya Boca. Kwa sasa, mashabiki wanapaswa kufurahia mafanikio ya timu. Nipo hapa kwa kila Boca itakachokihitaji,”alisema.
“Bado najihisi sawa na ilivyokuwa kabla sijaondoka. Lakini ukweli ni kwamba, nilimaliza msimu nikiwa na furaha England. Najisikia vizuri. Sina sababu ya kufikiria kuondoka kwa sasa, familia yangu inafurahia kuwepo England,”alisisitiza.

No comments:

Post a Comment