KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 7, 2012

Mwanamichezo bora TASWA kuzoa mil 12/-

MSHINDI wa jumla wa tuzo za wanamichezo bora zitakazotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) mwaka huu atazawadiwa dola 8,000 za Marekani (sh. milioni 12).
Zawadi hiyo ilitangazwa jana na Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Imani Lwinga alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa City Sports Lounge mjini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, TASWA na SBL zilitangaza vipengele na vigezo mbalimbali vitakavyotumika katika kutoa tuzo za mwanamichezo bora wa mwaka 2012. SBL ndiyo mdhamini mkuu wa tuzo hizo.
Sherehe za utoaji wa tuzo kwa wanamichezo bora zimepangwa kufanyika Juni 14 mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam. Sherehe hizo zitahudhuriwa na watu zaidi ya 1,000.
Akizungumza katika mkutano huo, Lwinga alisema maandalizi kwa ajili ya sherehe hizo yanaendelea vizuri na aliishukuru TASWA kwa ushirikiano mzuri na kampuni yake na wa kuigwa.
“Tunatambua umuhimu na uwepo wa kila mmoja wenu katika maandalizi haya na tunajivunia kuwa sehemu muhimu katika maandalizi ya tukio hili muhimu,” alisema Lwinga.
Aliongeza kuwa vipengele vilivyoanishwa katika tuzo hizo ni sahihi na kwamba kila kipengele kimewasilishwa kwa umakini mkubwa, mojawapo ikiwa ni kuwatambua waandishi wa habari za michezo.
"Kupitia udhamini huu, tungependa kuwashauri waandishi wa michezo kujaribu kuangalia mbele zaidi ili kuleta mwanga na uelewa wa haraka kwa jamii juu ya tasnia hii na faida zake kwa jamii hasa hapa kwetu Tanzania,”alisema Lwinga.
Lwinga alisema katika kundi la wanamichezo wa kila mchezo, mshindi atajinyakulia kitita cha sh. milioni moja kila mmoja. Michezo itakayowaniwa tuzo ni wavu, netiboli, judo, soka, kikapu, ngumi za kulipwa, ngumi za ridhaa, gofu, mchezaji bora anayecheza nje, mchezaji chipukizi, riadha na tuzo ya heshima.
Wanamichezo waliowahi kushinda tuzo hizo, miaka ikiwa kwenye mabano ni Samson Ramadhan (2006), Martine Sule (2007), Mary Naali (2008), Mwanaidi Hassan (2009-2010).

No comments:

Post a Comment