KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, June 30, 2012

Yanga mpya yaanza kuonyesha cheche

Timu ya soka ya Yanga jana iliichapa Express mabao 2-1 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Yanga tangu ilipokamilisha usajili wa msimu wa 2012/2013 na iliwachezesha wachezaji wake kadhaa wapya wakiwemo kipa Ally Mustafa, beki Kevin Yondani na kiungo Frank Domayo.

Mshambuliaji Jerry Tegete ndiye aliyewajaza furaha mamia ya mashabiki wa Yanga waliofurika kwenye uwanja huo, ambao walikuwa na hamu kubwa ya kuiona timu yao mpya, ambayo ilikuwa chini ya Kocha Fred Felix Minziro.

Jerry aliifungia Yanga mabao hayo mawili baada ya kucheza kwa uelewano mkubwa na Saidi Bahanuzi, Nizar Khalfan na Simon Msuva, ambaye alikuwa nyota ya mchezo.

Express ilizinduka katika kipindi cha pili baada ya kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji na kufanikiwa kupata bao la kujifariji baada ya beki mmoja wa Yanga kujifunga alipokuwa katika harakati za kuokoa mpira wa kona.

Katika mechi hiyo, Yanga ilionyesha uhai kwenye safu yake ya ulinzi iliyokuwa chini ya Yondani, Nadir Haroub, Juma Abdul na Oscar Joshua huku kiungo mkongwe, Athumani Iddi na chipukizi Domayo wakicheza vizuri kwenye safu hiyo.

WINFRIDA ASHINDA TAJI LA MISS UNIVERSE TANZANIA 2012MREMBO Winfrida Dominic (19) wa Dar es Salaam ameshinda taji la Miss Universe Tanzania, baada ya kuwashinda washiriki 16 katika fainali za mashindano hayo zilizofanyika kwenye Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam.
Pamoja na ushindi huo, Winfrida alipata ushindani mkali hasa katika hatua ya tano bora, ambapo warembo walijibu maswali mbalimbali kabla ya kutangazwa mshindi.
Winfrida, alionekana kujiamini tangu mwanzo wa mashindano hayo, na hiyo kuwa silaha kubwa katika mafanikio yake. Uzuri wake wa asili pia ulichangia kupata ushindi na kupata tiketi ya kuiwakilishaTanzania katika mashindano ya dunia yaliyopangwa kufanyika Desemba katika nchi itakayotangazwa baadaye.
Mbali na kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya Miss Universe, mrembo huyo pia alizawadiwa sh. milioni 3, na kupewa ofa ya kwenda kusoma nchini Marekani katika Chuo cha New York Film Academy.
"Ndoto yangu imetimia, nilipoamua kushiriki katika mashindano haya, lengo langu lilikuwa ushindi, ushindani ulikuwa mkubwa sana na hasa hatua ya tano bora, namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kushinda taji hili," alisema Winfrida.
Nafasi ya pili katika mashindano hayo ilikwenda kwa Bahati Chando (20), pia wa Dar es Salaam, ambaye alipata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss Earth na kuzawadiwa kitita cha sh milioni 1, huku Dorice Mollel (21) akiibuka katika nafasi ya tatu na kupata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss Tourism Queen International na kitita cha sh 500,000.
Dar es Salaam ilitawala mashindano hayo, kwani hata nafasi ya nne na tano zilichukuliwa na Kundi Mligwa (23) na Lilian Kolimba, ambao walizawadiwa sh 100,000 kila mmoja

Friday, June 29, 2012

Yanga kukata utepe na Atletico Kombe la Kagame

KATIBU Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye.MABINGWA watetezi Yanga watafungua dimba la mechi za michuano ya soka ya Kombe la Kagame kwa kumenyana na Atletico ya Burundi.
Ratiba ya michuano hiyo iliyotangazwa jana na Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye inaonyesha kuwa, mechi hiyo itapigwa Julai 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ratiba, pambano hilo litakaloanza saa 10 jioni, litatanguliwa na pambano lingine kati ya APR ya Rwanda na Wau Salaam ya Sudan Kusini.
Yanga imepangwa kundi C pamoja na timu za APR, Wau Salaam na Atletico.
Kundi A linaundwa na timu za Simba ya Tanzania Bara, URA ya Uganda, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Ports ya Djibouti.
Azam imepangwa kundi B pamoja na timu za Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya. Timu 11 zinatarajiwa kushiriki kwenye michuano hiyo.
Ratiba inaonyesha kuwa, timu tatu za kwanza kutoka kundi A na C na timu mbili kutoka kundi B zitafuzu kucheza hatua ya robo fainali. Mechi za hatua hiyo zitachezwa Julai 23 na 24, mechi za nusu fainali Julai 26 wakati fainali na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu itapigwa Julai 28.
Ratiba kamili ni kama ifuatavyo:

Julai 14, 2012- APR vs Wau Salaam Taifa C Saa 8

Yanga vs Atletico Taifa C Saa 10

Julai 15, 2012 Azam vs Mafunzo Chamazi B Saa 10

Julai 16, 2012 Vita Club vs Ports Taifa A Saa 8

Simba vs URA Taifa A Saa 10

Julai 17,2012 Atletico vs APR Taifa C Saa 8

Walau Salaam vs Yanga Taifa C Saa 10

Julai 18,2012 Vita Club vs URA Taifa A Saa 8

Ports vs Simba Taifa A Saa 10

Julai 19,2012 Atletico vs Walau Salaam Taifa C Saa 8

Mafunzo vs Tusker Taifa B Saa 10

Julai 20, 2012 Ports vs URA Taifa A Saa 8

Yanga vs APR Taifa C Saa 10

Julai 21, 2012 Azam vs Tusker Taifa B Saa 8

Simba vs Vita Club Taifa A Saa 10

WEMA AMPA ZAWADI OMOTOLA

Mcheza filamu wa kimataifa wa Nigeria, Omotola Jalade akijaribu kuvaa kanga aliyozawadiwa na mwenyeji wake, msanii nyota wa fani hiyo nchini, Wema Sepetu.

Msanii nyota wa filamu nchini, Wema Sepetu akimkabidhi zawadi ya kanga, viatu na shanga, mcheza filamu wa kimataifa wa Nigeria, Omotola Jalade muda mfupi kabla hajapanda ndege na kurejea kwao Nigeria juzi usiku. Kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya One Touch Solutions, Petter Mwendapole na katikati ni mwigizaji, Snura.

Simba, Azam uso kwa uso Kombe la Urafiki

TIMU za soka za Simba na Azam zinatarajiwa kukutana katika michuano ya Kombe la Urafiki inayotarajiwa kuanza Jumatatu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Simba na Azam ni miongoni mwa timu nane zilizoalikwa kushiriki kwenye michuano hiyo iliyolenga kuimarisha ujirani mwema katika michezo.

Wakati Simba na Azam zimethibitisha kushiriki kwenye michuano hiyo, Yanga imetangaza kujitoa kwa madai ya kutokuwa na maandalizi mazuri.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uamuzi wa kushiriki kwenye michuano hiyo umefikiwa kati ya benchi la ufundi na kamati ya ufundi.

“Tumeamua kushiriki kwa sababu tumeona haitakuwa vema kufanya hivyo wakati watu wa Zanzibar wametupa heshima kubwa ya kutualika kwenye michuano hii. Kombe la Urafiki lina maana kubwa kwa sasa kutokana na hali halisi ya kisiasa na kijamii iliyopo visiwani humo,"alisema.

Kaburu alisema pia kuwa, Simba itatumia fursa hiyo kuweka kambi maalumu kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame iliyopangwa kufanyika kuanzia Julai 14 mwaka huu. Kwa mujibu wa Kaburu, Simba pia itatumia ziara hiyo ya Zanzibar kutembeza kombe la ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwa mashabiki wao wa huko, ambao alisema walichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa ubingwa huo.
“Tusisahau pia kwamba kabla ya kucheza mechi yetu ya mwisho dhidi ya watani wetu wa jadi Yanga, ambayo tulishinda kwa idadi ya mabao 5-0, Simba ilikwenda kuweka kambi Zanzibar,” alisema Kaburu.
Simba itaanza michuano hiyo siku ya Jumatatu usiku kwa kucheza na Mafunzo.

Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Jumatatu jioni, lakini imesogezwa mbele hadi Jumatatu usiku.
Jumla ya timu nane zinashiriki katika michuano hiyo, ambapo Waekundu wa Msimbazi wapo katika kundi A lenye timu za Azam, Mafunzo na timu ya soka ya taifa ya vijana ya Zanzibar wenye umri wa chini ya miaka 23 (Karume Boys).
Wakati huo huo, Simba inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Express ya Uganda, itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Awali, Simba ilicheza na Express wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, ambapo zilitoka sare ya bao 1-1.

Thursday, June 28, 2012

ILALA YAENDELEA KUGAWA POINTI COPA COCA COLA

Ilala imeendelea kufanya vibaya kwenye michuano ya Copa Coca-Cola baada ya leo asubuhi (Juni 28 mwaka huu) kuchapwa mabao 4-0 na mabingwa watetezi Kigoma katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Mabao yote katika mechi hiyo ya kundi A yalifungwa kipindi cha kwanza huku Ramadhan Salum akipiga hat trick (mabao matatu). Alifunga mabao hayo dakika ya 13, 43 na 45.
Bao la pili kwa washindi lilifungwa dakika ya 19 na Athuman Rashid.
Wakati Kigoma imeshinda mechi mbili kati ya tatu ilizocheza mpaka sasa katika kundi hilo, Ilala imepoteza mechi zote tatu ilizocheza. Ilala imefungwa na Arusha, Kigoma na Lindi wakati mechi yake inayofuata itakuwa Juni 30 mwaka huu dhidi ya Kusini Pemba.
Nayo Kilimanjaro imeendelea kufanya vizuri katika kundi lake la D baada ya leo asubuhi (Juni 28 mwaka huu) kuitandika Shinyanga mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Mabao ya Kilimanjaro ambayo hadi sasa imeshinda mechi mbili na kutoka sare moja yalifungwa na Adam Soba dakika ya 11 na 46 wakati la tatu lilifungwa dakika ya 81 na James Henry. Katika mechi nyingine zilizochezwa leo asubuhi (Juni 28 mwaka huu), Temeke na Mtwara zilitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Tamco mkoani Pwani.
Ali Makalani alianza kuifungia Temeke na baadaye Adam swaleh akaisawazishia Mtwara. Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani ulishuhudia Morogoro na Kaskazini Pemba zikitoka sare ya bao 1-0. Amin Kassim aliifungia Kaskazini Pemba dakika ya 51, na Morogoro wakasawazisha dakika ya 75 kupitia kwa Mutalemwa Katunzi katika mechi hiyo ya kundi B.
Mechi zitakazochezwa leo jioni (Juni 28 mwaka huu) ni Lindi vs Arusha (Tanganyika Packers), Manyara vs Mjini Magharibi (Nyumbu), Kinondoni vs Mbeya (Tamco) na Kusini Unguja vs Pwani (Karume). Kesho (Juni 29 mwaka huu) ni mapumziko, na michuano hiyo itaendelea tena Juni 30 mwaka huu kwenye viwanja vyote vinne.

KUZIONA YANGA, EXPRESS KESHO BUKU TATU

WAKATI mabingwa wa ligi kuu ya soka nchini Uganda, Express wakiwasili leo tayari kwa mchezo wao wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Yanga, kiingilio cha juu cha mchezo huo utakaoipgwa jumaosi katika uwabnja wa Taifa kimepangwa kuwa shilingi 20,000 kwa VIP A.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu amesema kwamba mashabiki watakaokaa VIP watalipa shilingi, 15,000 kwa VIP B na C ,shilingi 5,000 ni kwa watakaokaa biti vya kijani na wale watakaokaa viti vya rangi ya bluu na chungwa watalipa shilingi 3,000.VODACOM KUZIZAWADIA SIMBA, AZAM J'MOSI

Kampuni ya Vodacom itakabidhi zawadi kwa washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu 2011/2012 katika hafla itakayofanyika Juni 30 mwaka huu kwenye hoteli ya Double Tree Hilton jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo itakayohudhuriwa na wawakilishi wawili kutoka katika klabu za Ligi Kuu, itaanza saa 12 jioni.

Katika hafla hiyo, washindi mbalimbali wakiwemo bingwa, makamu bingwa na mshindi wa tatu watakabidhiwa zawadi zao.

Wengine watakaozawadiwa ni mfungaji bora, kipa bora, timu bora yenye nidhamu, mchezaji bora wa ligi, refa bora na kocha bora.

Mabingwa wa ligi hiyo msimu uliopita ni Simba, wakifuatiwa na Azam na Yanga. Mfungaji bora ni John Bocco wakati kipa bora ni Juma Kaseja.

JOSE CHAMELEONE KUTUA BONGO SABASABA

Msanii wa Uganda, Jose Chameleone (pichani juu) leo amekamilisha taratibu zote za kusaini mkataba wa kufanya shoo kali Uwanja wa Taifa mpya, jijini Dar es salaam, siku ya sabasaba baada ya Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho, kutia timu Entebe mapema leo. Pichani chini ni Chameleone akijigamba kufanya shoo na akisaini mkataba wa mwisho huku akishuhudiwa na meneja wake. Chameleone ametoa onyo kwa Diamond kuwa atamchakaza na Valuvalu

Wednesday, June 27, 2012

MANJI AKATIWA RUFANI TFF

WAGOMBEA wawili wa uongozi katika uchaguzi mdogo wa klabu ya Yanga wamekatiwa rufani na baadhi ya wanachama kwa madai kuwa, hawana sifa zinazotakiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura aliwataja wagombea hao kuwa ni Yussuf Manji na Yono Kevela.
Katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Julai 15 mwaka huu, Manji anawania nafasi ya mwenyekiti wakati Kevela anawania nafasi ya makamu mwenyekiti.
Hata hivyo, Wambura hakutaja majina ya wanachama waliowakatia rufani wagombea.
Alisema mwanachama aliyemkatia rufani Manji, amewasilisha pingamizi 14 dhidi ya mgombea huyo wakati Kevela amekatiwa rufani moja.
Wambura alisema pia kuwa, baadhi ya wanachama wamekata rufani dhidi ya kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo kwa madai ya kuwapitisha Manji na Kevela wakati hawana sifa za uongozi.
Kwa mujibu wa Wambura, rufani hizo zinatarajiwa kujadiliwa wiki ijayo katika kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF, inayoongozwa na Deo Lyattu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamidu Mbwelezeni alisema jana kuwa, wamepanga kuzijadili rufani hizo wiki ijayo kwa vile Lyattu yupo nje ya nchi.
Hii ni mara ya pili kwa Manji kuwekewa pingamizi na wanachama wa Yanga kwa ajili ya uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa klabu hiyo.
Awali, mwanachama Ishashabaki Ruta alimwekea pingamizi Manji kwa kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo kwa madai kuwa, hana sifa na amekuwa chanzo cha migogoro mingi ndani ya klabu hiyo.
Hata hivyo, pingamizi hilo lilitupwa baada ya kubainika kuwa Ishashabaki hakuwa mwanachama halali wa Yanga na alishindwa kwenda kutetea hoja zake siku ya kusikilizwa.
Akizungumza na Burudani jana kwa njia ya simu kuhusu rufani aliyokatiwa kwa kamati ya uchaguzi ya TFF, Manji aliwataka wanachama wa Yanga wawe na watulivu na wenye subira.
Manji alisema hana wasiwasi kuhusu rufani hiyo kwa vile inafanana na pingamizi alilowekewa awali na kutupwa na kamati ya uchaguzi ya Yanga.
“Nawaomba wana Yanga wasiwe na wasiwasi kwa sababu naamini haki itatendeka na uchaguzi wetu utafanyika kama ilivyopangwa,”alisema.
Uchaguzi mdogo wa Yanga umeitishwa baada ya kujiuzulu kwa mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga, makamu wake, Davis Mosha na wajumbe wanne wa kamati ya utendaji.

Bi Cheka ampa shavu Godzilla

MWANAMAMA mkongwe kuliko wote katika muziki wa kizazi kipya, Mwahija Cheka (55) ameibuka na kibao kingine kipya kinachokwenda kwa jina la Good Brother Fella.
Mwahija, maarufu zaidi kwa jina la Bi Cheka, amerekodi wimbo huo kwa kushirikiana na msanii machachari wa muziki wa kizazi kipya, Godzilla.
Mmiliki wa kundi la TMK Wanaume Family, Saidi Fella alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kwa sasa Bi Cheka yupo kwenye maandalizi ya mwisho ya kurekodi wimbo huo.
Fella alisema kwa watakaousikia wimbo huo, watakubaliana na ukweli kwamba, bibi huyo hakupotea njia kujitosa kwenye muziki huo.
Kwa mujibu wa Fella, katika wimbo huo, Bi Cheka amepiga swagga za kutosha na za uhakika kiasi cha kuufanya uonekane kuwa wa aina yake.
Bi Cheka ameutumia wimbo huo kumshuruku Fella, ambaye ndiye aliyemfikisha alipo na kumtoa katika biashara yake ya zamani ya kuuza vitumbua na maandazi.
Mama huyo mkongwe mwenye uwezo wa kuimba aina nyingi za muziki, alianza kutamba baada ya kuibuka na kibao cha Ni wewe, alichomshirikisha Mheshimiwa Temba.
Bi Cheka anaamini kuwa, muziki wa bongo fleva upo kwenye damu yake na moja ya malengo yake ya baadaye ni kufika mbali zaidi.
Kipaji cha mama huyo kilivumbuliwa na Temba, ambaye alikutana naye miaka mitatu iliyopita mjini Morogoro. Tayari Bi Cheka ameshafanya maonyesho kadhaa ya kumtambulisha katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza na Morogoro.
“Nashukuru nilipokewa vizuri na ninapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wasanii wenzangu wa kituo cha kuendeleza vipaji cha Mkubwa na Wanawe,”alisema mama huyo.
“Kilichonipa moyo zaidi ni kuona kuwa mara baada ya kujaribiwa, wote walisema huyu bibi anajua kuimba, atatufaa, nikapewa nafasi, nikaonyesha vitu vyangu, ”aliongeza.
Pamoja na kuanza kupata umaarufu kimuziki, Bi Cheka alisema maisha yake hayajabadilika na kwamba ataendelea kubaki yule yule na kufanya yote aliyokuwa akiyafanya awali.

Ommy Dimpoz aibuka na ngoma mpya

BAADA ya kutamba vilivyo kwa kibao chake cha Nai Nai kilichomwezesha kushinda tuzo mbili za muziki za Kilimanjaro, msanii Ommy Dimpoz ameibuka na kibao kingine kipya.
Msanii huyo wa zamani wa bendi ya Top, inayoongozwa na Khaleed Mohamed (TID) ameshusha wimbo mpya unaokwenda kwa jina la Baadaye.
Dimpoz, ambaye pia hupenda kujiita kwa jina la Super Handsome alisema wiki hii mjini Dar es Salaam kuwa, anaamini kibao hicho kitawashika vilivyo mashabiki wake.
Msanii huyo alisema lengo la kurekodi kibao hicho ni kuwadhihirishia mashabiki wake kwamba hakubahatisha aliporekodi wimbo wake wa Nai Nai, akiwa amemshirikisha Ali Kiba.
Wakati kibao chake hicho kikiwa kimeshaanza kupigwa kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini, Dimpoz pia anasubiri ujio wa wimbo wake mwingine unaojulikana kwa jina la Tonight.
Dimpoz alirekodi wimbo huo kwa kushirikiana na msanii DJ Cleo wa Afrika Kusini wakati msanii huyo alipokuwepo nchini kwa ziara ya kimuziki mapema mwaka huu. Wimbo huo ulirekodiwa kwenye studio za B Hits za Dar es Salaam.
DJ Cleo aliondoka na demo ya wimbo huo kwa ajili ya kwenda kumalizia kazi ya kuurekodi nchini kwao na kazi hiyo imeshakamilika.
Kwa mujibu wa Dimpoz, wimbo huo unatarajiwa kuanza kusikika hivi karibuni baada ya CD yake kuwasili nchini.
“Nashukuru na nimefurahi sana kwamba nimepata bahati ya kurekodi wimbo na mmoja wa wasanii nyota wa muziki wa hip hop barani Afrika,”alisema Dimpoz. “Nilichokifanya ni kumpatia demo yenye wimbo huo ili akamalizie kwao kazi ya kuingiza sauti na kuchanganya mipigo ili kuiongezea ubora na akishairejesha, wimbo utakuwa umekamilika,”aliongeza msanii huyo. Dimpoz alisema amerekodi wimbo huo katika miondoko ya soul. Kwa sasa Dj Cleo anatamba na songi lake la 'Facebook'.

Hussein Machozi ataka kuhamia Kenya

MSANII machachari wa muziki wa bongo fleva nchini, Hussein Machozi amesema anafikiria kuhamishia shughuli zake za muziki katika nchi jirani ya Kenya.
Hussein alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa muziki wake unakubalika na kuthaminiwa zaidi nchini humo kuliko Tanzania.
Msanii huyo, ambaye mara nyingi amekuwa akiweka kambi Kenya kila anapojiandaa kutoa wimbo mpya, ameweka wazi kuwa anataka kuhama Tanzania kwa vile kumejaa wanafiki wengi wa kimuziki.
Alipotakiwa kufafanua kuhusu madai yake ya kuwepo kwa unafiki mwingi wa kimuziki bongo, Hussein alisema waandishi wa habari wamechangia kuwepo kwa hali hiyo.
“Okay, watu wa media hawako free kabisa, yaani huwa wanafuata upepo wanapoanzisha wale wenye nguvu,”alisema msanii huyo.
“Yaani wakitaka kumtoa mtu wao na media zingine zinafuata, wala hawashtuki kuwa analazimishwa atoke wakati kuna ngoma kibao kali wanazipotezea ili mtu wao apite. Matokeo yake wanatoa ngoma moja inapata umaarufu, baada ya hapo ni pumba tupu. Huwa inaniuma sana,” aliongeza msanii huyo.
“Kwa Kenya mambo hayo hakuna kabisa. Kule kama ngoma ni kali,itatandikwa hadi noma, ila kama ni mbaya, huwezi hata kuiskia,”alisisitiza msanii huyo asiyekuwa na makeke.
”Nakubalika zaidi Kenya kwa sababu ngoma zangu ni kali na zina kichwa na miguu, namaanisha wimbo unakuwa na stori ya kufuatilia na inaskilizika na rika zote, nadhani hii ni sababu tosha sana,” alisema Machozi.
Hivi karibuni, msanii huyo alirekodi wimbo wake mpya unaojulikana kwa jina la Addicted, akiwa amemshirikisha msanii anayetamba nchini Kenya kwa sasa, Size 8.
Hussein alisema ameamua kurekodi wimbo huo kwa ajili ya mashabiki wake wa kike na kuongeza kuwa, video ya wimbo huo itatengenezwa na Kampuni ya Ogopa DJs.
Msanii huyo, ambaye amekuwepo nchini Kenya tangu wakati wa sikukuu ya Pasaka, amekuwa akifanya maonyesho mbalimbali, hasa katika mji wa Mombasa na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki.
Kabla ya kurekodi kibao hicho, Hussein aliibuka na wimbo wa Jela, ambao unazungumzia matatizo mbalimbali ya kimaisha, ambayo husababisha vijana wengi kuishia huko.
Akizungumzia changamoto, ambazo amekuwa akikabiliana nazo katika kurekodi nyimbo zake hapa nchini, Hussein alisema ni gharama kubwa za kurekodi wimbo studio.
Alisema gharama hizo na zile za kurekodi video zimekuwa kubwa kiasi cha kuwafanya wasanii wengi washindwe kuzimudu na hivyo kukaa kimya kwa muda mrefu ama kuachana na fani hiyo.
Hussein alisema chanzo kikubwa cha kupanda kwa gharama hizo ni matatizo ya umeme, ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara hapa nchini.

MR BLUE APATA MTOTO WA KIUMEMSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Kherry Sameer Rajab, ambaye aliwahi kung’ara kimuziki miaka ya mwanzoni mwa 2000 amepata mtoto wa kiume.
Kherry, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Mr. Blue alipata mtoto huyo wa kiume wiki mbili zilizopita baada ya mchumba wake kujifungua.
Mchumba wake huyo, ambaye Mr. Blue aliwahi kumtambulisha kwa jina la Wahida, alijifungua mtoto huyo mjini Dar es Salaam.
"Nimevuka hatua moja kwenda nyingine,”alisema Mr. Blue alipozungumza na mitandao mbalimbali.
“Kwa sasa mimi si mvulana tena bali ni baba, naitwa Baba Sameer," alisema Mr. Blue huku akitabasamu.
"Nimeamua kumpa mtoto wangu jina hili maana naona linamfaa, kwani ni jina langu la pili, ambalo nimekuwa nikilitumia kwa muda mrefu, pia ni jina la baba yangu," aliongeza.
Mr. Blue alianza kujihusisha na masuala ya muziki mwaka 1999 na kilichosababisha ajitose kwenye fani hiyo ni kaka zake, waliojulikana kwa majina ya The Boy Stain na Obrey.
Kaka zake hao walianza kujitosa kwenye muziki mapema na kusababisha naye avutiwe na fani hiyo na kuamua kuyapa kisogo masomo.
Hata hivyo, Mr. Blue hakuanza kuimba moja kwa moja. Alikuwa akifuatilia ni jinsi gani muziki unatengenezwa na kuanzia mwaka 2001 alikuwa akipenda kuhudhuria sherehe mbalimbali za vikundi vya mitaani.
Mwishoni mwa mwaka 2003, ndipo Mr. Blue alipoanza kuchomoza kimuziki baada ya kuibuka na kibao chake cha kwanza kinachojulikana kwa jina la Mr. Blue, ambacho kilimpatia umaarufu mkubwa.
Baadaye aliibuka na kibao chake cha pili kinachokwenda kwa jina la Mapozi, ambacho kiliendelea kumtangaza vyema katika soko la muziki wa bongo fleva.
Baada ya kutikisa soko la muziki huo kwa kipindi kirefu, ndipo msanii huyo mwenye sura yenye mvuto alipoachia albamu yake ya kwanza inayokwenda kwa jina la ‘Mr. Blue’ na kufuatiwa na albamu ya ‘Yote kheri’
Na sasa baada ya ukimya wa muda mrefu, Mr. Blue ameibuka na video ya wimbo wake mpya wa Loose Control, ambao ameuimba kwa kushirikiana na msanii Majol Power.
Mr. Blue amesema katika video hiyo, amekuja kwa staili tofauti kuanzia katika mavazi, uchezaji pamoja na uimbaji, lengo likiwa ni kuongeza ladha ya muziki wake kwa mashabiki.
Msanii huyo alizaliwa Aprili 14, 1987. Ni mtoto wa tatu kati ya wanne kwa kuzaliwa katika familia ya mzee Sameer Rajab mwenye asili ya Ki-Sudan.
Elimu yake ya msingi aliipata katika shule ya Gerezani, ambako alihitimu darasa la saba mwaka 1999. Hata hivyo, hakuweza kumaliza elimu ya sekondari katika shule ya sekondari ya Dar es Salaam, ambako aliishia kidato cha pili mwaka 2004.
Alipoulizwa ni kitu gani kilichosababisha kukatisha masomo yake ya sekondari, alisema: "Muziki ndio ulionifanya nikaacha shule, lakini bado nahitaji kusoma na baada ya muda nategemea kujiendeleza kimasomo nje ya nchi."
Akizungumzia hatua waliyochukua wazazi wake kutokana na kuacha kwake shule kwa sababu ya muziki, anasema hawakumgombeza kwani walijua ni ujana tu unamsumbua huku wakiamini itafikia wakati atatulia
Anawashukuru mama yake mzazi, Halima Rajab na baba yake Sameer Rajab kwa kumruhusu kujikita katika muziki, ambao umemwezesha kupata faida kubwa kimaisha.

EUCHARIA: Bado natamani kuolewa

LAGOS, Nigeria
MIEZI michache baada ya kuamua kuokoka na kuwa mchungaji, mcheza filamu Eucharia Enunobi amesema bado anatamani kuwa na mume makini.
Eucharia, ambaye ni mama wa mtoto mmoja amesema amekuwa akimuomba Mungu kila kukicha ili aweze kupata mume mwema na makini.
Mwanadada huyo amesema hajawahi kuishi katika maisha matamu ya kimapenzi na anatamani siku moja aweze kuyapata maisha hayo.
“Sijawahi kuwa na maisha ya kimapenzi na mwanaume. Ninaposema maisha ya kimapenzi, simaanishi kwamba wanaume hawanitongozi. Watu wananitongoza, lakini kama ni kwa staili ya kitu kinachoitwa rafiki wa kiume, hapana,”alisema mwigizaji huyo aliyejizolea sifa na umaarufu kutokana na staili yake ya uigizaji. “Siwezi kufanya kitu kama hicho, lakini naomba kwa Mungu niwe na mwanaume, ambaye atakuwa mume wangu,”alisisitiza.
Eucharia alisema anaamini Mungu atamjalia kupata mume bora haraka iwezekanavyo, lakini alisisitiza kwamba, kwa sasa hilo halimsumbui kwa vile yupo bize katika kazi ya kuhubiri dini.
“Naelewa kuwa katika maisha kuna vishawishi vya hapa na pale. Hivyo napenda kusema kwamba katika siku si nyingi zijazo, rafiki yangu atajitokeza na upweke kwangu utatoweka, lakini sina wasiwasi kwa hilo,”alisema.
“Biblia inanifanya niwe bize kutokana na kuhubiri injili. Kutembea kunanifanya niwe bize. Naelewa na kutambua kwamba kila kitu kinakwenda kutokana na mipango ya Mungu. Naamini hivi karibuni atanikutanisha na mwanaume sahihi kwangu,”aliongeza.
Eucharia, ambaye amecheza filamu nyingi, ikiwemo Glamour Girls, hivi karibuni aliibuka na filamu yake ya kwanza, inayojulikana kwa jina la The Kingdom.

Mimi ni albino-Doris Simeon


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu chipukizi wa Nollywood, Doris Simeon, ambaye ndoa yake ilikumbwa na misukosuko hivi karibuni, amefichua kuwa yeye ni albino.
Doris ameueleza mtandao wa naijerules hivi karibuni kuwa, watu wengi hawatambui kuhusu ukweli huo ndiyo sababu iliyomfanya aweke mambo hadharani. ‘Mnaelewa kwamba mimi ni albino na ni rahisi kunigundua kwa sababu ya mwonekano wangu. Hakuna njia, ambayo itamfanya albino asiweze kutambulika mbele ya kundi la watu,’ alisema.
Doris ni mtoto wa pili katika familia ya watoto watano wenye ulemavu wa ngozi ya mwili na asili yake ni Benin katika jimbo la Edo, lakini alizaliwa na kukulia katika jiji la Lagos.
Alipata elimu ya sekondari katika shule ya Maryland na baadaye katika chuo cha PEFTI. Amecheza filamu nyingi za Nollywood na kwa sababu ameanza kutengeneza filamu zake.
Hivi karibuni, Doris aliripotiwa akimlalamikia mcheza filamu mwenzake, Stella Damasus.

Mume wa Omotola ampa somo mume wa Ini Edo

Omotola Jalade akiwa na mumewe, kepteni Mathew Ekeinde

Ini Edo (kulia) akiwa na mumewe, Philip Ehiagwina

LAGOS, NIGERIA
MUME wa mcheza filamu nyota wa Nigeria, Omotola Jalade, Kepteni Mathew Ekeinde ametoa somo kwa mume wa mcheza sinema mwingine, Ini Edo.
Kepteni Ekeinde, ambaye ni rubani wa ndege amemweleza mume wa Ini, Philip Ehiagwina kwamba hapaswi kupandwa na hasira mkewe anapoandikwa vibaya na vyombo vya habari.
Ekeinde amemtaka Philip azipuuze habari hizo kwa sababu hiyo ndiyo gharama ya umaarufu na kuongeza kuwa, habari nyingi zinazoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari ni za kupika.
“Miaka michache iliyopita, (Philip) aliripotiwa akiwaonya waandishi wa habari wa Nigeria wasindike habari mbaya kuhusu mkewe, Ini Edo. Kwa mujibu wa habari hizo, iwapo watafanya hivyo, atawachukulia hatua za kisheria,”alisema Ekeinde.
“Swali la kujiuliza ni kwamba, kama hawezi kuwa na mke maarufu, kwa nini asingeoa mke wa kawaida ? Kama angekuwa ndiye Rais Goodluck Jonathan, angewakata waandishi wote walioandika habari mbaya kuhusu mkewe, Patience?”
“Kwa nini asijifunze kutoka kwa Kepteni Mathew Ekeinde jinsi ya kumudu kuishi na mke maarufu? Pengine ni vizuri ajifunze kutokasirika pale zinaporipotiwa habari mbaya kuhusu mkewe Ini Edo kama ambavyo Kepteni Mathew amefanya kwa Omotola,”alisema.
“Tafadhali msinielewe vibaya, simaanishi kwamba waandishi wa habari wasiandike habari za uongo kuhusu watu, lakini kama hilo litatokea, vyombo vya sheria vipo kushughulikia suala hilo,”alisisitiza.
Ekeinde ametoa ushauri huo kwa Philip kufuatia kauli aliyoitoa hivi karibuni ya kukanusha mkewe Ini Edo kuonekana kwenye ukumbi wa burudani akiwa na mwanaume mwingine.
Philip aliielezea taarifa hiyo iliyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa, haikuwa ya kweli na ililenga kumchafua mkewe.
Kepteni Ekeinde alimuoa Omotola miaka 16 iliyopita na wamefanikiwa kuzaa watoto wanne. Walisherehekea ndoa yao kufikisha idadi hiyo ya miaka Machi 23 mwaka huu.
Ndoa nyingi za wacheza filamu wa kike wa Nollywood zimekuwa hazidumu kwa miaka mingi kutokana na sababu mbalimbali, lakini ndoa ya Kepten Ekeinde na Omotola imedumu kwa miaka mingi na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kijamii wamesema wanandoa hao wanastahili tuzo.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Nigeria vimekuwa vikiripoti habari nyingi kuhusu Omotola kuwa na uhusiano na wanaume wengine, lakini mumewe amekuwa akizipuuza na kukaa kimya.

WASHIRIKI MISS UNIVERSE TANZANIA WATEMBELEA AMINA DESIGN

Baadhi ya washiriki wa shindano la Miss Universe Tanzania 2012 wakipata maelezo kutoka kwa mmiliki wa duka la Amina Design, Amina Plummer walipotembelea kwenye duka hilo lililopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam juzi.

Coastal Union yamnasa Kisambale wa Yanga

KLABU ya Coastal Union ya Tanga imemsajili kiungo wa zamani wa klabu ya Yanga, Pius Kisambale.
Habari kutoka ndani ya Coastal Union zimeeleza kuwa, Kisambale ametia saini mkataba wa kuichezea timu hiyo kwa miaka miwili.
Kisambale amejiunga na Coastal Union akitokea Yanga, ambayo aliichezea kwa msimu mmoja uliopita.
Mchezaji huyo ni ndugu wa damu wa kiungo wa klabu ya Yanga, Athumani Iddi, ambaye aliwahi kuzichezea timu za Polisi Dodoma na Simba.
Hata hivyo, haikuwekwa wazi kuhusu malipo ya usajili wa kiungo huyo na kiwango cha malipo ya mshahara atakayokuwa akilipwa kwa mwezi.
Uamuzi wa Coastal Union kumsajili Kisambale umelenga kukiimarisha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Mbali na Kisambale, uongozi wa Coastal Union pia unafanya mipango ya kumsajili kiungo wa kimataifa wa Kenya, Jerry Santo.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Coastal Union kimeeleza kuwa, mazungumzo kati ya uongozi na mchezaji huyo wa zamani wa Simba yanakwenda vizuri na anatarajiwa kuwasili mjini Tanga wakati wowote.

Wadau walalamikia uzungu kwenye filamu za kiswahili

WADAU wa sanaa nchini wamehoji uhalali wa wasanii wa filamu kutumia lugha ya kiingereza kwenye majina ya filamu zao na pia kazi hizo kubeba maudhui ya kizungu zaidi.
Wakizungumza mwanzoni mwa wiki hii kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa, wadau hao walisema hawaelewi ni kwa nini filamu nyingi zinazoandaliwa nchini zinapewa majina ya kizungu wakati zipo filamu nyingi kutoka nje zinazotumia lugha za kihindi, kichina, kifaransa na zinafanya vizuri.
“Hoja kwamba, wanatumia majina ya kiingereza ili kuteka soko la kimataifa ni ya kitoto. Mbona hapa kwetu kuna filamu nyingi za kihindi na kichina zinanunuliwa kwa wingi? Hapa kuna udhaifu katika kutengeneza filamu zenye ubora, tujikite huko,” msanii Nkwama Bhallanga.
Kwa mujibu wa wadau hao, filamu ni taaluma inayozungumza kwa kutumia picha na vitendo zaidi hivyo haihitaji mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili afahamu maudhui na ujumbe unaowasilishwa na kazi husika ya filamu.
“Maneno kwenye filamu si muhimu sana, kinachozungumza ni matendo na picha zaidi, ndiyo maana kuna watu wanaangalia picha za kikorea na wanaburudika na kuelewa kinachoendelea,” alisema Godfrey Lebejo, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Aliongeza kuwa, kinachoitesa tasnia ya filamu kwa sasa ni kukosekana kwa weledi na uhalisia wa tamaduni za Kitanzania kunakosababishwa na wimbi kubwa la watu kujiingiza kwenye filamu ili kufanikisha mambo yao yaliyo nje ya maadili na utamaduni huo.
“Inawezekana vipi utengeneze filamu ambayo baba, mama na watoto hawawezi kukaa pamoja kuitazama? Tufike mahali tuseme mambo haya ya kipuuzi basi kwenye filamu zetu,” alionya Lebejo.
Awali, akiwasilisha mada kuhusu filamu, wasanii na haja ya kujiendeleza kielimu, msanii wa filamu, Emmanuel Myamba, maarufu kam Pastor Myamba, alisema tasnia ya filamu inakosa weledi hivyo kuhitaji mabadiliko.
“Ni wazi ukiangalia filamu zetu zinakosa weledi katika uandishi wa miswada, uongozaji, uhariri na hata uumbaji wa wahusika. Lazima tukubali udhaifu huu ili tuurekebishe,” alisema Myamba, ambaye kwa sasa amefungua kituo cha mafunzo ya filamu kiitwacho Tanzania Film Training Centre (TFTC) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam.

TWALIPO ACADEMY, KITUO KINACHOTOA MAFUNZO YA UAMUZI WA SOKA KWA VIJANA

WAKATI akifungua michuano ya soka na netiboli ya kuwania Kombe la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka alipatwa na mshtuko mkubwa alipokuwa akitambulishwa kwa waamuzi waliopangwa kuchezesha mechi za soka.
Alipatwa na mshtuko huo baada ya kuwaona waamuzi hao, ambao ni wanafunzi wa shule ya sekondari ya Jitegemee na pia kituo cha kuendeleza soka cha Kambi ya Twalipo iliyopo Chang’ombe, Dar es Salaam.
“Hivi hawa vijana wataweza kweli kuchezesha soka?” Waziri Gaudencia alimtupia swali Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau.
“Hawa vijana ni wazoefu sana, wamekuwa wakichezesha mechi za michuano ya Copa Coca Cola na Kombe la Uhai kila mwaka,” alijibu Dk. Dau huku akitabasamu.
Kauli hiyo ya Dk. Dau ilimfanya Waziri Kabaka awe na hamu kubwa ya kuwashuhudia kwa macho vijana hao wakichezesha soka. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani alitazama mechi hiyo kati ya TBC na Jambo Leo kuanzia mwanzo hadi mwisho.
“Hawa vijana (waamuzi) peke yao ni burudani, ni vijana wadogo sana, lakini wanaifahamu vyema kazi yao, napongeza uamuzi wa kuwapa vijana hawa mafunzo ya uchezeshaji soka tangu wakiwa wadogo,”alisema Waziri Kabaka baada ya mechi hiyo kumalizika huku akionekana kuwa na furaha kubwa.
Waziri Kabaka aliwamwagia sifa waamuzi hao kwa kuonyesha umahiri mkubwa katika uchezeshaji wa mchezo huo na kukipongeza kituo cha Twalipo kwa kutoa mafunzo kwa vijana hao.
Mbali na vijana hao kupewa mafunzo ya uamuzi na wakufunzi wa kituo hicho, pia wamekuwa wakipata mafunzo mbalimbali yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Hivi karibuni, vijana 15 wa kituo hicho walishiriki katika mafunzo ya kuchezesha soka yaliyotolewa na TFF kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kufaulu vizuri mitihani yao.
Mkufunzi mkuu wa kituo hicho, Stafu Sajenti Abel Kitundu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kwa sasa vijana hao wameshaanza kufanya mitihani ya uamuzi kwa ajili ya kupangiwa madaraja.
“Mwanzo vijana hawa hawakuwa wakifanya mitihani ya uamuzi, lakini walikuwa wakitumika kuchezesha mechi za michuano mbalimbali kama vile Copa Coca Cola na Kombe la Uhai,”alisema Kitundu.
“Lakini hivi sasa wameshaanza kufanya mitihani hiyo na wamekuwa wakifanya vizuri. Lengo ni kuwapandisha madaraja kama ilivyo taratibu kwa waamuzi wa soka,”aliongeza.
Kitundu alisema pia kuwa, wamepokea mwaliko kutoka nchini Burundi, ambako waamuzi hao watoto wanatakiwa kwenda kuchezesha mechi za michuano ya Kombe la Rollingstone inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Bujumbura.
Alisema waandaaji wa michuano hiyo wametaka wapelekewe waamuzi 12 kutoka kituo hicho kwa vile hawataki ichezeshwe na waamuzi wengine.
Je, ni nani aliyetoa wazo la kuanzishwa kwa mafunzo ya uamuzi kwa vijana hao?
Kwa mujibu wa Kitundu, wazo hilo lilitolewa na mwamuzi mstaafu, Kanali Issaro Chacha na Meja Bakari mwaka 2007. Alisema kwa kuanzia, walianza kutoa mafunzo ya kucheza soka kwa vijana wadogo.
Lakini baada ya kituo kuanza kukua na vijana wengi zaidi kujitokeza kupata mafunzo hayo, waliona ni vyema pia kuanzisha mafunzo ya kuchezesha soka kwa vijana wengine.
“Tulikuwa na vijana wengi, lakini tulipata tabu katika uchezeshaji wa mechi, tukaona ni vyema tutafute vijana kwa ajili ya kuwapa mafunzo ya kuchezesha soka ili wasaidie katika kazi hiyo,”alisema.
Kwa sasa, kituo hicho kinao wanafunzi 36, kati ya hao waamuzi 32 ni wa kiume na wanne wa kike. Alisema kituo hicho kinafadhiliwa na kuendeshwa na kambi ya Twalipo.
Kitundu alisema awali wanafunzi wa kituo hicho walikuwa wakitoka katika shule mbalimbali za sekondari za mjini Dar es Salaam, lakini baada ya kufanya mazungumzo na uongozi wa shule ya sekondari ya Jitegemee, waliamua kuwahamishia katika shule hiyo.
“Tuliona ili iwe rahisi kuwapata kwa wakati mmoja, ni vyema wasome karibu na mahali ilipo kambi yetu ndio sababu kwa sasa wote wanasoka sekondari ya Jitegemee,”alisema.
Ameushukuru uongozi wa TFF kwa kutoa kipaumbele kwa vijana hao kimafunzo na kuongeza kuwa, anaamini ipo siku watakuwa waamuzi bora hapa nchini na kimataifa.
Je, vijana hao wanafaidika vipi kutokana na malipo yanayotolewa kutokana na kuchezesha mechi za michuano mbalimbali?
Kwa mujibu wa Kitundu, vijana hao wamekuwa wakipatiwa sehemu kubwa ya mgawo wa fedha za malipo hayo, ambazo wamekuwa wakizitumia kulipia ada na mahitaji mengine ya shule.
“Tumekuwa na utaratibu wa kuingia mikataba na wanaosimamia na kuendesha michuano mbalimbali, hivyo sehemu ya malipo wanayotoa kwa ajili ya kazi ya uamuzi, tunawapatia vijana hawa,”alisema.
Kitundu ametoa mwito kwa vijana wenye mapenzi na kazi ya uamuzi wa soka, kujitokeza kujiunga na chuo hicho kwa vile mafunzo hayo yanatolewa bure kwa vijana wote, hakuna malipo.

Dodoma yaitambia Mbeya Copa Coca Cola

TIMU ya soka ya Dodoma ya vijana wa chini ya miaka 17 imeendeleza wimbi la ushindi kwenye michuano ya Copa Coca-Cola baada ya kuifunga Mbeya mabao 2-0.
Mechi hiyo ya kundi C iliyokuwa ya kusisimua na yenye ushindani mkali, ilichezwa jana asubuhi katika uwanja wa Tamco uliopo Kibaha mkoani Pwani.
Katika mechi hiyo, mabao ya Dodoma yalifungwa na Japhet Lunyungu dakika ya 59 na Frank Kaji dakika saba kabla ya mchezo kumalizika.
Nayo Mjini Magharibi ilitoka uwanjani kifua mbele baada ya kuifunga Iringa mabao 3-0 katika mechi ya kundi B iliyochezwa kwenye uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani.
Mechi za asubuhi zilizokuwa zichezwe leo kati ya Arusha na Kusini Pemba kwenye uwanja wa Tanganyika Packers na Pwani na Tabora kwenye uwanja wa Karume, zilitarajiwa kuchezwa mchana kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano ya barabara kutoka Pwani kuingia Dar es Salaam.
Leo jioni kutakuwa na mechi kati ya Rukwa na Ruvuma (Tanganyika Packers), Mwanza na Tanga (Nyumbu), Kaskazini Unguja na Mara (Tamco) na Singida na Kagera (Karume).

Mwogeleaji aongezeka kambi ya Olimpiki

MWOGELEAJI Magdalena Moshi wa Tanzania anatarajiwa kujiunga na wachezaji wenzake watakaoshiriki katika Michezo ya Olimpiki mwishoni mwa wiki hii.
Magdalena ndiye mwogeleaji pekee wa Tanzania aliyefuzu kucheza katika michezo hiyo inayotarajiwa kuanza mwezi ujao katika Jiji la London nchini Uingereza.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Noel Kiunsi amesema Magdalena alitarajiwa kutua nchini jana akitokea Australia ambako anasoma.
"Ni kweli tumepata nafasi ya kupeleka mchezaji mmoja kwenye michezo hiyo mikubwa duniani, na kama ujuavyo, Magdalena yuko nje ya nchi kwa ajili ya masomo, lakini kulingana na taarifa zilizopo, anatarajia kuwasili nchini leo (jana) au kesho (leo)," alisema.
Kiunsi alisema mara mchezaji huyo atakapofika nchini, watawasiliana na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), ambayo ndiyo inayosimamia kambi hiyo.
Michezo ya Olimpiki imepangwa kuanza Julai 27 hadi Agosti 12 mwaka huu na Tanzania itawakilishwa na wanamichezo sita.
Akizungumzia nafasi ya Magdalena katika michezo hiyo, Kiunsi alisema itakuwa vigumu kwake kufanya vizuri kutokana na kupata nafasi hiyo kwa upendeleo.
Kwa mujibu wa Kiunsi, Magdalena amepewa nafasi hiyo na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Kuogelea (FINA).
“Hii itakuwa mara ya pili kwa Magdalena kushiriki kwenye michezo ya kimataifa, lakini nafasi yake kubwa ni kuongeza rekodi yake anayoishikilia sasa,”alisema.
Wanamichezo wengine wa Tanzania watakaoshiriki katika michezo hiyo ni wanariadha Samsoni Ramadhan, Msenduki Mohammed (marathoni) na Zakia Mrisho (mita 5,000) na bondia Seleman Kidunda anayecheza uzito wa kilogramu 69.

Yanga sasa wajifua mchana

BENCHI la ufundi la klabu ya Yanga limeamua kubadilisha programu ya mazoezi kwa wachezaji wake kutoka asubuhi hadi mchana.
Yanga pia imeamua kuhamisha uwanja wake wa mazoezi kutoka Kaunda uliopo Jangwani kwenda shule ya sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, timu hiyo ilifanya mazoezi yake kwa muda asubuhi kwenye uwanja wa Kijitonyama.
Sendeu alisema walilazimika kufanya mazoezi kwa muda kwenye uwanja huo ili kukamilisha mipango ya kuhamia Loyola.
Awali, Yanga ilikuwa ikifanya mazoezi nyakati za asubuhi, lakini Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix Minziro na msaidizi wake, Mfaume Athumani wameamua mazoezi hayo yawe yakifanyika mchana.
Hata hivyo, Sendeu hakuweka wazi kuhusu uamuzi wa makocha hao kubadili muda wa mazoezi.
Yanga inajiandaa kwa michuano ya Kombe la Kagame, iliyopangwa kuanza Julai 14 hadi 29 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Michuano hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, pia itazishirikisha timu za Azam na mabingwa wa Tanzania Bara, Simba. Yanga ni bingwa mtetezi.
Kwa sasa, Yanga bado ipo kwenye mchakato wa kusaka kocha mkuu mpya baada ya kocha wa zamani, Kostadin Papic kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu uliopita.
Ilielezwa kuwa, uongozi wa klabu hiyo upo kwenye mazungumzo na kocha wa zamani wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo, lakini imeamua kufuta mpango huo.
Kikosi cha sasa cha Yanga kinaundwa na wachezaji wengi wapya, wakiwemo kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na beki Kelvin Yondan waliosajiliwa kutoka Simba, Ladislaus Mbogo kutoka Toto African, viungo Frank Damayo kutoka JKT Ruvu, Nizar Khalfan aliyekuwa anakipiga Marekani na mshambuliaji Simon Msuva kutoka Moro United.

Simba yamtema Jabu, yamtoa mkopo Haruna

KLABU ya Simba imetangaza rasmi kuwaacha wachezaji wake wanne katika msimu ujao wa ligi na kuwatoa kwa mkopo wengine wanne kwa klabu zingine.
Simba imewasilisha majina hayo juzi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikiwa ni utekelezaji wa kanuni za shirikisho hilo zinazotaka kila klabu itangaze mapema majina ya wachezaji inaowaacha.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara ni miongoni mwa klabu tano za ligi hiyo zilizowasilisha majina hayo TFF juzi.
Wachezaji, ambao Simba imetangaza kuwaacha katika usajili wa msimu ujao ni Ally Mustafa, Derick Walulya, Gervas Kago na Juma Jabu wakati mkataba wa Salum Kanoni unatarajiwa kumalizika Juni 30 mwaka huu.
Kwa mujibu wa orodha hiyo, Simba imewatoa kwa mkopo Rajabu Isihaka, Salum Machaku, Haruna Shamte na Shija Mkina.
Polisi Morogoro, iliyopanda daraja msimu huu, imewaacha wachezaji 17 wakati Tanzania Prisons ambayo pia imepata hadhi ya ligi kuu msimu huu, imewaacha wachezaji 11.
Habari zaidi kutoka ndani ya TFF zimeeleza kuwa, Azam imekatisha mikataba ya wachezaji watatu wakati wachezaji 12 wamemaliza mikataba yao katika klabu ya Kagera Sugar.
Uhamisho wa wachezaji kwa msimu huu ulianza Juni 15 mwaka huu na utamalizika Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuanza kwa usajili kwa wachezaji wasio wa ligi kuu ni kati ya Juni 15 na 30 mwaka huu.
Wachezaji walioachwa na Polisi Morogoro ni Abdul Ibadi, Ally Moshi, Benedict Kitangita, Hassan Kodo, Hussein Lutaweangu, Hussein Sheikh, Juma Maboga, Mafwimbo Lutty, Makungu Slim na Mbaraka Masenga.
Wengine ni Method Andrew, Moses Mtitu, Ramadhan Kilumbanga, Ramadhan Toyoyo, Said Kawambwa, Salum Juma na Thobias John.
Tanzania Prisons imewaacha Adam Mtumwa, Dickson Oswald, Exavery Mapunda, Ismail Selemani, Lwitiko Joseph, Mbega Daffa, Mwamba Mkumbwa, Musa Kidodo, Rajab Ally, Richard Mwakalinga na Sweetbert Ajiro.
Wachezaji waliomaliza mikataba yao kwa mujibu wa Kagera Sugar ni Cassian Ponera, Hamis Msafiri, Hussein Swedi, Ibrahim Mamba, Martin Muganyizi, Mike Katende, Moses Musome, Msafiri Davo, Said Ahmed, Said Dilunga, Steven Mazanda na Yona Ndabila.
Azam imewasitishia mikataba wachezaji Tumba Swedi, Mau Bofu na Sino Augustino.

Tuesday, June 26, 2012

DC TANGA AWAAHIDI KITITA WACHEZA POOL

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego (katikati) akimkabidhi jezi na pesa taslimu kiongozi wa Klabu ya Michael’s Pub, Michael Bundala wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Safarli Lager Pool Taifa Mkoa wa Tanga jana. Kushoto ni Meneja mauzo wa TBL Mkoa wa Tanga,Bahati Mbise.


MKUU wa wilaya ya Tanga,Halima Dendego ameahidi kutoa pesa taslimu 200,000 kwa timu itakayofanya vizuri katika mashindano ya 'Safari Lager Pool' ngazi ya Mkoa wa Tanga ili kuweza kuipa hamasa ya kwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo ngazi ya taifa.

Dendego alitoa wito huo juzi wakati wa Makabidhiano ya vifaa vya mashindano hayo kutoka kwa Kampuni ya Bia nchini TBL kwa timu 9 ambazo zinashiriki mashindano hayo ambayo yataanza ramsi kesho katika ukumbi wa Mangroose iliyopo Sahare jijini Tanga.

Alisema mchezo huo ni kama michezo mengine hivyo aliwataka wadau wa mchezo huo kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri ya kuuweka mchezo huo nje ya mabaa ili uweze kupendwa na watu wa kila aina.

Aidha aliwaomba viongozi wa mchezo huo kuwa wanapokaa kwenye kamati zao kuhakikisha wanaweka muda maalumu wa kucheza na kueleza kuwa wanapaswa kuujengea mtazamo mzuri ili uweze kupendwa zaidi.

Katika makabidhiana hayo Kampuni ya Bia nchini (TBL)kupitia bia yake ya Safari Lager walikabidhi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya sh. milion 5 kwa timu zote tisa ambazo zinashiriki mashindano hayo ambao yataanza kesho na yanatarajiwa kufikia tamati Jumapili wiki hii ambapo yatafanyika siku nne.

Vifaa vilivyo kabidhiwa ni pamoja na tisheti na pesa taslimu kwa kila timu shiriki katika mashindano hayo ambavyo ni High Way,Spaider,Members Family,Kijiti Pool Table,Tanga Beathing Club,Kibo Garden Pool,Maiko Pub,Kange Brothers na Ngamiani Sports Club.

Akizungumza wakati akikabidhi Vifaa hivyo Meneja Mauzo wa Kampuni ya TBL Mkoa wa Tanga,Bahati Mbise alizitaka timu shiriki kuhakikisha zinatumia ipasavyo vifaa hivyo na kuweza kucheza kwa ushindani na kuwa makini ili kuweza kupata timu bora ambayo itawakilisha vema mkoa katika mashindano hayo ngazi ya taifa.

NGORONGORO HEROES KUJIPIMA KWA MISRI NA RWANDA

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) itacheza mechi nne za kirafiki na timu za Misri na Rwanda kabla ya kuivaa Nigeria kwenye mashindano ya Afrika. Ngorongoro Heroes ambayo kwa mara ya kwanza itakuwa chini ya kocha mpya Jakob Michelsen itaanza kwa kucheza mechi mbili za Misri zitakazofanyika Julai 3 na 5 mwaka huu, na baadaye Julai 14 na 16 mwaka huu dhidi ya Rwanda.

Mechi zote zitachezwa nchini, na kama ilivyo Ngorongoro Heroes, Misri na Rwanda nazo ziko kwenye kinyang’anyiro cha kusaka tiketi za kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazofanyika mwakani nchini Algeria.

Katika raundi ya kwanza, Ngorongoro Heroes iliitoa Sudan ambapo katika raundi ya pili imepangiwa Nigeria, na mechi ya kwanza itafanyika jijini Dar es Salaam, Julai 29 mwaka huu. Timu hizo zitarudiana wiki mbili baadaye nchini Nigeria.

Iwapo Ngorongoro Heroes itafanikiwa kuitoa Nigeria, katika raundi ya mwisho itacheza na mshindi kati ya Congo Brazzaville na Afrika Kusini.

MABINGWA COPA COCA COLA WACHAPWA NA RUVUMA

Ruvuma imeanza vizuri michuano ya Copa Coca-Cola baada ya kuwafunga mabingwa watetezi Kigoma mabao 2-0 katika mchezo wa kundi A uliofanyika leo asubuhi (Juni 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Kigoma ambayo iliifunga Lindi mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa juzi, ilishindwa kufua dafu mbele ya Ruvuma na kuruhusu bao katika kila kipindi.
Mabao yote ya washindi yalifungwa na mshambuliaji Edward Songo. Mshambuliaji huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 34 wakati la pili alilipachika dakika ya 84. Katika mechi nyingine zilizochezwa leo asubuhi, Tanga na Morogoro zilitoka sare ya mabao 3-3 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Mkoani Pwani, Mara iliifunga Temeke bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nyumbu wakati Kagera ililala bao 1-0 mbele ya Kilimanjaro katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tamco

TFF KUZAWADIA WAPIGA PICHA COPA COCA-COLA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litawazawadia wapiga picha za magazetini watakaoripoti mashindano ya Copa Coca-Cola 2012 ngazi ya Taifa yanayoendelea kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Coca-Cola na kushirikisha mikoa 28 yanafanyika viwanja vya Tanganyika Packers, Kumbukumbu ya Karume mkoani Dar es Salaam, na viwanja vya Tamco na Nyumbu mkoani.

Zawadi ya sh. 250,000 itatolewa kwa picha bora katika maeneo matatu; action picture, fair play picture na mpiga picha ambaye ameripoti matukio mengi ya mashindano hayo yanayoshirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17.

Washiriki wanatakiwa kuwasilisha picha zao zilizotumika (cuttings) ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

TFF YAMTAMBULISHA KOCHA MPYA WA VIJANA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemtambulisha rasmi leo mbele ya waandishi wa habari kocha mpya wa timu za Taifa za vijana, Jakob Michelsen kutoka Denmark ambaye amechukua nafasi ya Kim Poulsen ambaye hivi sasa anainoa Taifa Stars.

Michelsen ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja alitambulishwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na kusema falsafa yake ni kama ile ya Poulsen ya kumiliki mpira na kushambulia muda wote wa mchezo.

Kabla ya kuja Tanzania, Michelsen alikuwa kocha wa timu ya daraja la kwanza ya Hobro IK ya Denmark. Ana leseni A ya ukocha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), leseni ya ukocha wa vijana kutoka Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).

Moja ya mafanikio yake ni kuipa ubingwa wa Denmark, timu ya Skovbakken kwenye ligi ya timu zenye umri chini ya miaka 18. Ubingwa huo aliupata msimu wa 2005/2006

Monday, June 25, 2012

TAMASHA LA WAZI LA AIRTEL JIUNGE NA SUPA5 LATIKISA MWANZA

Meneja Mahusiano wa kampuni ya simu za mikononi ya Airtel-Tanzania,Jackson Mmbando akimkabidhi Jamila Juma simu ya mkononi aina ya Sumsung,baada kuibuka mshindi kwa kuichammbua vyema huduma mpya ya Airtel Jiunge na Supa5.

Wakazi wa Mwanza, Jamila Juma na Sandra Mwashitete wakipewa maelekezo mafupi namna ya kutumia mtandao wa Airtel pamoja na huduma zake mbalimbali, mara baada ya kujishindia simu aina ya Sumsung,wakati kampuni ya Airtel ilipokuwa ikizindua huduma yake mpya ya Airtel Jiunge na Supa5,uliofanyika jana kwenye viwanja vya Furahisha,jijini Mwanza.

Ni Mzee wa Makamo hivi lakini alionesha umahiri wake mkubwa wa kuwachangamsha vilivyo sehemu ya wakazi wa jiji la Mwanza.Anaitwa Mzee Salum akikamua jukwaani jana kwenye viwanja vya Furahisha jijini Mwanza,wakati wa uzinduzi wa huduma mpya ya Airtel Jiunge na Supa5.

Msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya na kiongozi wa kundi la Wanaume Halisi kutoka Temeke,jijini Dar,akiwa sambamba na msanii mwenzake (hayupo pichani) aitwaye Kr-Mulla wakilishambulia jukwa huku shangwe kubwa ikilipuka kutoka kwa sehemu kubwa ya wakazi wa jiji la Mwanza waliojitokeza jana wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma mpya ya Airtel Jiunge na Supa5.

Msanii Juma Nature wa kundi la TMK Wanaume Halisi akifanya vitu vyake jukwaani


Baadhi ya wasanii wa kikundi cha Kinonko chenye maskani yake pale Kinondoni,kikionesha umahiri wake wa kucheza mbele ya umati mkubwa wa wakazi wa jiji la Mwanza waliojitokeza kwenye viwanja vya Furahisha wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma mpya ya Airtel Jiunge na Supa5.

Baadhi ya Wakazi wa jiji la Mwanza wakiendelea kuhamia Airtel na kupata huduma mbalimbali za kampuni hiyo,jana jioni kwenye viwanja vya Furahisha wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma mpya ya Airtel Jiunge na Supa5.

Miss Universe Tanzania 2012 kusakwa Ijumaa

MASHINDANO ya kumsaka mrembo wa Miss Universe Tanzania 2012 litafanyika Ijumaa hii kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa yaliyopo Posta jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Compass Comm unications, Maria Sarungi Tsehai alisema jana kuwa mashindano hayo yatashirikisha jumla ya warembo 20 kutoka katika mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Manyara, Arusha, Dodoma, Mwanza, Mtwara, Kilimanjaro na wenyeji Dar es Salaam na kuongeza kwamba warembo wote wanaendelea na mazoezi chini ya wakufunzi walioboea katika masuala ya urembo.

“Tunatarajia kuwa na mashindano bora ili kuweza kumapata mrembo ambaye atatupa sifa katika mashindano ya kimataifa kama ilivyokuwa kwa Flaviana Matata mwaka 2007 ambapo alishika nafasi ya saba katika mashindano yaliyofanyika nchini Mexico,” alisema Maria.

Maria aliwataja warembo hao kuwa ni Bahati Chando, Aisha Maulidi, Catherine Mpulule, Cecilia Moses, Consolata Mosha, Devotha Keregese, Doris Mollel, Doreen Mapunda na Edith Tesha.

Wengine ni Getrude Asanterabi, Jescha Tiba, Kundi Mligwa, Lilian Kolimba, Mary Joel, Naomi Joseph, Nyaso Malilo, Neema Mpanda, Susan Manoko, Theodora Msenya na Winfrida Dominic.

Alisema kuwa shindano hilo limedhaminiwa na gazeti la The Citizen, gazeti dada la Mwananchi kwa kushirikiana na wadhamini wengine, Le Grand Casino, Urban Rose Hotel, Amina Design, Dodoma Hotel na New York Film Academy.

Maria alisema kuwa shindano hilo litaanza saa 1.00 usiku kwa warembo hao kupita jukwaani wakiwa katika aina mbalimbali za mavazi kama vile ya ubunifu na lile la usiku.

Alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya shindano hilo kubwa la urembo yamekamilika na kinachosubiliwa ni siku ya shindano hili kupata mrithi wa Miss Universe anayemaliza muda wake Nelly Kamwelu.

Alifafanua kuwa wameboresha mashindano ya mwaka huu na wanatarajia kuwa na mashindano bora kabisa tofauti na ya miaka ya nyuma.

Sakata la Lulu sasa latinga Mahakama ya Rufani

JAMHURI imewasilisha maombi Mahakama ya Rufani Tanzania, kuomba kupitia uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Dk. Fauz Twaib wa kukubali kufanyia uchunguzi wa umri wa msanii wa filamu Elizabeth Michael 'Lulu'.
Hati hiyo ya maombi ya Jamhuri iliwasilishwa jana Mahakama ya Rufani ikiiomba ipitie uamuzi wa Jaji Dk. Twaib alioutoa Juni 11, mwaka huu kwa madai kuwa, una makosa.
Juni 11, mwaka huu, Jaji Dk. Twaib, aliamua suala la uchunguzi wa umri wa Lulu, litasikilizwa Mahakama Kuu na kupatiwa ufumbuzi, licha ya maombi hayo ya msanii huyo, kuletwa kimakosa.
Wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda, alidai hayo jana katika Mahakama Kuu, mbele ya Jaji Dk. Twaib, wakati maombi ya uchunguzi wa umri wa Lulu yalipotajwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Lulu anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, anawakilishwa na mawakili Keneth Fungamtama akisaidiana na Flugence Massawe na Peter Kibatala.
Mawakili hao walidai kwamba wapo tayari kwa usikilizwaji wa maombi hayo. Katika maombi hayo, tayari mawakili wa Lulu na Jamhuri walishawasilisha ushahidi wao wa hati za viapo na wa maandishi ili kutatua juu ya umri wa muombaji huyo.
Hata hivyo, Wakili Elizabeth aliiomba Mahakama Kuu kuahirisha usikilizwaji wa maombi hayo kwa muda kwa kuwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), imewasilisha hati ya Mahakama ya Rufani kuomba kupitiwa kwa uamuzi wa Jaji huyo kwa kuwa una makosa.
Ombi hilo la kuahirishwa kwa muda usikilizwaji wa maombi hayo lilipingwa na mawakili wa Lulu, Fungamtama na Kibatala kwa madai kwamba hakuna amri iliyotoka Mahakama ya Rufani ya kuahirishwa usikilizwaji huo.
Fungamtama alidai kuwa mahakama hiyo haiwezi kuahirisha usikilizwaji huo kutokana na maombi ya Jamhuri kwani ilipaswa iwepo amri kutoka Mahakama ya Rufani.
Pia alidai katika hati yao ya maombi, hakuna sehemu ambayo wanaomba ahirisho la usikilizwaji wa maombi hayo hadi hapo Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi.
Wakili Fungamtama alidai kuwa kitendo cha DPP kuwasilisha hati hiyo jana ni kuharibu mwenendo wa mahakama.
Kwa upande wake, Wakili Kibatala alidai Jamhuri imechelewa kuwapa hati hiyo ya maombi ya kupitia uamuzi wa Jaji.
Akijibu hoja hizo, Wakili Elizabeth alidai wamewasilisha maombi hayo jana na kupewa namba na kwamba wao walipewa na Mahakama na hivyo kuamua kuwapatia mawakili hao kwani si kazi yao.
Wakili Elizabeth alikiri kwamba hakuna amri ya Mahakama ya Rufani iliyoletwa Mahakama Kuu ya kusimamishwa kwa usikilizwaji huo, alisikia ipo na itapelekwa hivyo kama haijafika suala hilo lipo nje ya uwezo wake.
Pia aliiomba mahakama kuahirisha usikilizwaji huo na kwamba wanaiachia itoe uamuzi wake wa kukubali au kukataa hivyo si kazi yao ni ya mahakama.Mbali na hilo, Wakili huyo alidai nia ya ofisi ya DPP ni kuona haki inatendeka.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Dk. Twaib aliamua kuwa amezingatia hoja hizo na ameiona hati hiyo ya maombi ya Jamhuri hivyo hawezi kupoteza muda wa kuendelea kusikiliza maombi hayo wakati muda wowote mwenendo wa kesi na uamuzi wake utaitwa Mahakama ya Rufani.
Jaji huyo alisema kuwa maombi hayo yataahirishwa kwa muda mfupi hadi Julai 9, mwaka huu yatakaposikilizwa.
Pia aliamuru kusimamishwa kwa mwenendo wa kesi katika Mahakama ya Kisutu, hadi hapo utakapotolewa uamuzi na Mahakama za juu kama alivyoamuru Juni 11, mwaka huu.
Jaji Dk. Fauz alitoa uamuzi wa kusimamishwa kwa mwenendo huo, baada ya Wakili wa Lulu, Fungamtama kuomba maelekezo ya mahakama kutokana na ofisi ya DPP na Mahakama ya Kisutu kufungua faili la dharura na kuendelea na mwenendo wakati ulisimamishwa.
Akiwasilisha hoja hiyo, Wakili Fungamtama alidai licha ya Mahakama Kuu kusimamisha mwenendo wa kesi ya mauaji inayomkabili Lulu, lakini bado mteja wao alifikishwa Mahakama ya Kisutu.

Milovan atua Dar, timu kurejea leo usiku kutoka Mwanza

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amerejea nchini kwa ajili ya kuendelea kuinoa timu hiyo kwa michuano ya Kombe la Kagame na msimu ujao wa ligi.Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga ameieleza blogu ya liwazozito leo kuwa, Milovan aliwasili nchini usiku wa kuamkia leo akitokea kwao Serbia alikokwenda kwa mapumziko.

Kwa mujibu wa Kamwaga, kocha huyo alitua kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki na kupokewa na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo.

Milovan alikwenda kwao kwa mapumziko mara baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, ambapo aliiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa.

Kurejea kwa kocha huyo kumemaliza uvumi uliokuwa umezagaa kwamba, huenda asingerudi baada ya kutofautiana na viongozi wa Simba kuhusu mkataba mpya.

Wakati Milovan akiwa amerejea nchini, kikosi cha Simba kilichokwenda Mwanza na Shinyanga kwa ajili ya ziara ya mechi za kirafiki, kinatarajiwa kurejea Dar es Salaam usiku huu kwa ndege kikitokea Mwanza.

Simba ilicheza mechi yake ya kwanza Jumamosi kwa kumenyana na Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara walicheza mechi ya pili jana dhidi ya Express ya Uganda kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na kutoka nayo sare ya bao 1-1.

Katika mechi hizo mbili, Simba iliwatumia wachezaji wake kadhaa wapya, akiwemo kiungo Kigi Makasi aliyesajiliwa kutoka Yanga.

TAMASHA LA WAJANJA LA VODACOM LAFANA MOROGORO

Msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya Shetta pamoja na madansa wake wakiwaburudisha wakazi wa Morogoro wakati wa Tamasha la”WAJANJA”lililofanyika mjini humo,Tamasha hilo linaloendeshwa na Vodacom Tanzania,litaendelea katika mikoa ya Mtwara na Tanga likiwa na lengo la kuwaelimisha wananchi kutumia mtandao wa kampuni hiyo kwa kuongea kwa robo shilingi na kutuma ujumbe kwa shilingi ishirini na tano na kutumia facebook na twitter bure.

Msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya Fid Q akiwapagawisha wakazi wa Morogoro kwenye Tamasha la ”WAJANJA”lililofanyika mjini Morogoro hapo jana,Tamasha hilo linaloendeshwa na Vodacom Tanzania,litaendelea katika mikoa ya Mtwara na Tanga likiwa na lengo la kuwaelimisha wananchi kutumia mtandao wa kampuni hiyo kwa kuongea kwa robo shilingi na kutuma ujumbe kwa shilingi facebook na twitter bure.

Msanii wa muziki wa kizazi kipya Diamond akiwa amebebwa juujuu na madansa wake wakati akitumbwiza ishirini na tano na kutumia kwenye Tamasha la ”WAJANJA”lililofanyika mjini Morogoro hapo jana,Tamasha hilo linaloendeshwa na Vodacom Tanzania,litaendelea katika mikoa ya Mtwara na Tanga likiwa na lengo la kuwaelimisha wananchi kutumia mtandao wa kampuni hiyo kwa kuongea kwa robo shilingi na kutuma ujumbe kwa shilingi facebook na twitter bure.

Diamond akikata mauno kama vilivyo wakati wa Tamasha la”WAJANJA”lililofanyika mjini Morogoro hapo jana,Tamasha hilo linaloendeshwa na Vodacom Tanzania,litaendelea katika mikoa ya Mtwara na Tanga likiwa na lengo la kuwaelimisha wananchi kutumia mtandao wa kampuni hiyo kwa kuongea kwa robo shilingi na kutuma ujumbe kwa shilingi ishirini na tano na kutumia facebook na twitter bure.


Msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya Shetta akisakama jukwaa kama vilivyo mjini Morogoro wakati wa Tamasha la”WAJANJA”lililofanyika mjini humo,Tamasha hilo linaloendeshwa na Vodacom Tanzania,litaendelea katika mikoa ya Mtwara na Tanga likiwa na lengo la kuwaelimisha wananchi kutumia mtandao wa kampuni hiyo kwa kuongea kwa robo shilingi na kutuma ujumbe kwa shilingi ishirini na tano na kutumia facebook na twitter bure.

Msanii mkali aliopo kwenye chati hivi sasa Ommy Dimpoz akiwapagawisha wakazi wa mji wa Morogoro wakati wa Tamasha la”WAJANJA”Linaloendeshwa na Vodacom Tanzania hapo jana,Tamasha hilo litaendelea kufanyika katika mikoa ya Mtwara na Tanga, likiwa na lengo la kuwaelimisha wananchi kutumia mtandao wa kampuni hiyo kwa kuongea kwa robo shilingi na kutuma ujumbe kwa shilingi ishirini na tano kwenda mtyandao wowote na kutumia facebook na twitter bure.