'
Sunday, March 31, 2013
NANCY SUMARI: KUJIAMINI KUMENIFIKISHA NILIPO
MREMBO wa Tanzania wa 2005, Nancy Sumari amesema kufanya kitu bila kuogopa kushindwa ndio siri ya kufanikiwa kwake katika mambo mbalimbali.
Akihojiwa katika kipindi cha Makutano kilichorushwa hewani wiki iliyopita kupitia kituo cha televisheni cha DTV, Nancy alisema katika maisha yake, haogopi kufanya kitu chochote hata kama hana uzoefu nacho.
Nancy alisema utamaduni wake huo wa kujiamini ndio uliomwezesha kushinda mataji ya Miss Dar Indian Ocean, Miss Kinondoni na hatimaye Miss Tanzania.
Mbali na kutwaa mataji hayo, Nancy pia alikuwa Mtanzania wa kwanza kuweka rekodi ya kushinda taji la Miss World Africa 2005 baada ya kufuzu kuingia hatua ya fainali.
Mama huyo wa mtoto mmoja alisema, kabla ya kujitosa katika mashindano ya urembo, aliwahi kufanyakazi kama muuzaji katika duka la fenicha na kulipwa mshahara wa sh. 120,000 kwa mwezi.
Alisema aliamua kufanyakazi hiyo baada ya kukwama kupata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo cha sheria, kutokana na chuo hicho kutoruhusu mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne kwa elimu ya Kenya, kujiunga moja kwa moja kwa masomo ya shahada.
"Nilifanyakazi hiyo kwa moyo wote hadi nilipopata nafasi ya kushiriki mashindano ya urembo baada ya waandaaji kuniona na kuvutiwa na mimi,"alisema.
Akizungumzia uamuzi wake wa kuchapisha kitabu cha Nyota Yako, Nancy alisema umetokana na kutokuta vitabu vya watoto madukani vilivyoandikwa na waandishi wa Tanzania.
"Mbali ya kuwa mimi ni mama kwa wakati huu, kila nilipokwenda kwenye maduka ya vitabu, nilikosa vitabu vya watoto vilivyoandikwa na waandishi wa Tanzania. Vingi vimeandikwa na waandishi wa nje,"alisema.
"Hivyo niliamua kuandika kitabu, ambacho watoto wa kike wa Tanzania wataweza kukisoma na kuvutiwa kufanya kile, ambacho nimekiandika kwenye kitabu hicho,"aliongeza.
Kwa mujibu wa Nancy, kitabu hicho kinapatikana katika maduka ya Scholastica lililopo Mlimani City na Novel Idea lililopo Masaki, Dar es Salaam kwa bei ya sh. 5,000.
Nancy amewataka vijana wanaochipukia kujaribu kuwa wazuri kwa sababu kila mmoja anafanya makosa, hakuna aliye sahihi kwa asilimia 100.
"Lakini ni muhimu kama binadamu, tujitahidi kufanya vitu sahihi, sawa na unapoona ua linafifia, limwagilizie maji likue na unapomwona mwenzako anahitaji msaada na unayo nafasi, usisite kumsaidia,"alisema.
Nancy kwa sasa ni Mkurugenzi wa Matukio wa Kampuni ya Frontline Management, ambayo amekuwa akiiongoza kwa kushirikiana na mrembo mwenzake, Irene Kiwia na anatarajia kumaliza masomo ya Chuo Kikuu Julai mwaka huu.
MOURINHO, ABRAMOVICH WAMALIZA TOFAUTI ZAO
LONDON, England
MMILIKI wa klabu ya Chelsea ya England, Roman Abramovich amemaliza tofauti kati yake na kocha mkuu wa zamani wa timu hiyo, Jose Mourinho na kukubaliana kumrejesha katika klabu hiyo.
Abramovich na Mourinho walifikia makubaliano hayo Jumatatu iliyopita baada ya kufanya mazungumzo kwa faragha.
Mourinho alikuwepo nchini England kwa ajili ya kushuhudia mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Brazil na Russia iliyochezwa kwenye uwanja wa Stamford Bridge. Katika mechi hiyo, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Abramovich alitofautiana na Mourinho baada ya kocha huyo kushindwa kuiwezesha Chelsea kutwaa mataji aliyokuwa akiyataka baada ya kuiwezesha kutwaa ubingwa wa England, Kombe la FA na Kombe la Carling.
Gazeti la Daily Mail la Uingereza liliripoti jana kuwa, Abramovich amekuwa akimtaka Mourinho arejee England kwa mara ya pili kwa ajili ya kuinoa Chelsea.
Tayari Abramovich na Mourinho wameshafikia makubaliano hayo, lakini hakuna yeyote kati yao aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha Sky Sports, Mourinho alisema kwa sasa bado yeye ni kocha mkuu wa Real Madrid ya Hispania na kwamba lengo lake ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji la ligi ya mabingwa wa Ulaya msimu huu.
Hata hivyo, Mourinho hakuona aibu kuelezea mapenzi yake kwa England na kuvifananisha vyombo vya habari vya nchi hiyo kuwa sawa na sukari na pilipili katika chakula chake cha kila siku.
Abramovich amekuwa na mapenzi makubwa kwa Mourinho baada ya kushindwa kumpata kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola, ambaye amejiunga na Bayern Munich ya Ujerumani.
"Siwezi kupinga. Licha ya hali hii ya hewa, napenda kuwepo hapa,"alisema Mourinho, ambaye pia ni maarufu kwa jina la Special One.
"Nafikiri siku moja nitarejea katika ligi kuu ya England katika klabu ya Chelsea au nyingineyo. Chelsea ipo moyoni mwangu, hivyo siku moja nitarejea. Tunayo nyumba hapa, binti yetu anakuja kusoma London hivyo kuwepo kwangu London ni kitu cha kawaida kwetu," aliongeza kocha huyo.
"Lakini kila ninapokuja hapa na watu wakiniona nakatiza mitaani ama kufanya manunuzi, wanaanza kuunganisha mambo. Sijali kwa sababu kila siku ninapopata nafasi, naeleza wazi kwamba napenda kuwepo hapa. Nilikuwa na wakati mzuri hapa na kwamba nitarejea. Huwa sipendi kusema mengi kuhusu hisia hizi kwa sababu napenda kuwepo hapa,"aliongeza.
Mbali na Chelsea, Mourinho pia amekuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na Manchester United na Manchester City.
Kwa sasa, Chelsea inanolewa na kocha wa muda, Rafael Benitez, ambaye mashabiki wa klabu hiyo wamekuwa hawamuungi mkono kutokana na matokeo mabaya katika ligi.
"Nilikuwepo Manchester wiki tatu zilizopita na hali ya hewa ya huko ilikuwa nzuri zaidi. Nilifanya mazungumzo na Sir Alex Ferguson kwa kumtumia ujumbe japokuwa alikuwa akikabiliwa na mechi,"alisema Mourinho.
"Lakini Manchester ni utawala wa Sir Alex na ningependa kazi hiyo iwe ya kudumu kwake. Bila shaka haiwezi kuwa hivyo, lakini ningependa aendelee na kazi hiyo kwa miaka mingi zaidi," alisisitiza.
Mourinho pia aliizungumzia Manchester City na kocha wake, Roberto Mancini. Alisema kutokana na kocha huyo kuiwezesha Manchester City kutwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita, hafikirii iwapo yanaweza kufanyika mabadiliko yoyote.
"Hata kwa Benitez, natumaini kila kitu kinakwenda vizuri kwake na watamaliza msimu vizuri,"alisema Mourinho, ambaye pia amewahi kuzinoa FC Porto ya Ureno na Inter Milan ya Italia.
"Mwisho wa siku, nipo Real Madrid, nakabiliwa na majukumu mazito hadi mwisho wa msimu huu. Tumefuzu kucheza robo fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya, tumefuzu kucheza fainali ya Kombe la Mfalme, hivyo watu wanaelewa mimi ni kocha wa kulipwa na kwamba kwa sasa nafikiria kazi yangu Real Madrid," alisema kocha huyo.
Mourinho alisema anaona fahari kuwa kocha aliyeweza kutwaa mataji mawili ya ligi ya mabingwa wa Ulaya akiwa na timu tofauti na kwamba angependa kutwaa tena taji hilo msimu huu.
Kocha huyo alisema atavunjika moyo iwapo atashindwa kutwaa taji hilo msimu huu baada ya baadhi ya vigogo kama vile Manchester United na Chelsea kutolewa hatua ya awali.
Hata hivyo, alikiri kuwa timu zote nane zilizosalia katika michuano hiyo ni nzuri na yoyote inaweza kutwaa ubingwa.
Msimu huu umekuwa mbaya kwa Mourinho, kufuatia Real Madrid kuzidiwa kwa tofauti ya pointi 13 na mahasimu wao, Barcelona katika msimamo wa ligi kuu ya Hispania.
Matumaini pekee ya kocha huyo kwa sasa yamebaki katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya na Kombe la Mfalme wa Hispania, ambapo Real Madrid itacheza fainali dhidi ya Atletico Madrid.
Real Madrid imepangwa kumenyana na Galatasaray ya Uturuki katika robo fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya.
YANGA YAWAONYA WAFANYABIASHARA
KLABU ya Yanga imewaonya wafanyabiashara wanaotengeneza na kuuza bidhaa mbalimbali zenye nembo ya klabu hiyo bila idhini ya uongozi.
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kufanya hivyo ni makosa kisheria na kwamba wahusika watachukulia hatua.
"Kwa miaka mingi sasa, kumekuwepo na tabia kwa wafanya biashara mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi kujihusisha na utengenezaji, uingizaji na uuzaji wa bidhaa zenye nembo ya Yanga.
"Yanga inapenda kutoa angalizo kuwa tabia hiyo iliyokithiri ni ukiukwaji wa sheria na unaikosesha klabu mapato halali, ambayo ingeyapata kutokana na matumizi ya nembo yake,"alisema Mwalusako.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema, nembo ya Yanga iliyosajiliwa rasmi kwa msajili Juni 2, 2009, inamilikiwa na klabu hiyo hivyo hairuhusiwi kwa mtu mwingine kuitumia bila ridhaa ya uongozi.
"Kwa mantiki hiyo, Yanga inatangaza rasmi kuwa ni marufuku kwa kampuni, mtu binafsi au kikundi chochote kutengeneza ama kuuza bidhaa zenye nembo ya Yanga bila ridhaa ya klabu.
Iwapo itatokea mtu yeyote kukiuka amri hii, uongozi utachukua hatua kali za kisheria ili kuikomesha,"alionya Mwalusako.
Kiongozi huyo wa Yanga amewashauri wafanya biashara wanaotaka kutengeneza na kuuza bidhaa zenye nembo ya klabu hiyo, kuwasiliana na uongozi ili wapewe haki hiyo kisheria.
Alisema mfanya biashara atakayekubali kufikia makubaliano na uongozi, atakubaliwa kutengeneza ama kuingiza bidhaa hizo kwa malipo maalumu.
Hata hivyo, Mwalusako alionya kuwa, lazima bidhaa hizo ziwe zenye kiwango na ubora, ambao utakubaliwa na kupitishwa na uongozi wa Yanga.
Mwalusako ametoa mwito kwa wanachama na wapenzi wa Yanga kutonunua bidhaa zozote zenye nembo ya klabu hiyo iwapo muuzaji hajaruhusiwa na uongozi kufanya hivyo.
WADAU WA FILAMU WAMPONGEZA WEMA KWA KUMWOKOA KAJALA
WADAU mbalimbali wa fani ya filamu wamempongeza msanii nyota wa tasnia hiyo nchini, Wema Sepetu kwa kumwokoa msanii mwenzake, Kajala Masanja kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 12.
Wakizungumza na Burudani kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam jana, wadau hao walisema kitendo kilichofanywa na Wema kumlipia Kajala faini ya sh. milioni 13 ni cha ujasiri na mfano wa kuigwa.
Kajala, ambaye alisota rumande kwa mwaka mmoja, alinusurika kwenda jela Jumatatu iliyopita baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili kati ya matatu ya kutakatisha fedha.
Mume wa msanii huyo, Faraja Chambo alihukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 12 baada ya kupatikana na hatia ya makosa yote matatu na kushindwa kulipa faini ya sh. milioni 213.
Kajala na Chambo, walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Marchi 15, mwaka jana, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama ya kubadilisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi, Salasala, Dar es Salaam kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
"Kwa kweli kitendo kilichofanywa na dada huyu ni ujasiri wa aina yake. Wapo wasanii wengine maarufu wa filamu, lakini wameshindwa kumsaidia mwenzao kama alivyofanya Wema,"alisema Robert Justine, mkazi wa Kiwalani, Dar es Salaam.
Mwanadada Lucy Tesha, mkazi wa Mnazi Mmoja, Dar es Salaam alisema, alichokifanya Wema, hakuna mwingine wa kumlipa fadhila zake, isipokuwa Mwenyezi Mungu.
"Wema asisubiri kulipwa wema wake hapa duniani. Atalipwa na Mungu,"alisema dada huyo.
Mkazi mwingine wa Buguruni, aliyejitambulisha kwa jina la Chambo Waziri alisema, Wema amefanya kile, ambacho si watanzania wengi wanaweza kukifanya.
"Fikiria, Kajala amehukumiwa kwenda jela miaka 13, wazazi wake ni masikini, yeye na Wema ni marafiki wa kawaida tu, lakini amemsaidia utadhani ndugu yake wa kuzaliwa tumbo moja,"alisema.
Shamsa Majid, mkazi wa Ilala Boma alisema, msanii mwingine anayestahili kupongezwa ni Mahsen Awadh, maarufu kwa jina la Dk. Cheki kutokana na kuwa mstari wa mbele kusaidia wenzake.
"Kwa kweli nampa big up Cheni. Alikuwa mstari wa mbele kumsaidia Lulu (Elizabeth Michael) na juzi tumemuona akiwa mstari wa mbele kumsadia Kajala. Hawa wengine wamebaki maneno maneno tu,"alisema.
YANGA YABANWA, SIMBA YACHECHEMEA, AZAM YAPASUA ANGA
VINARA wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana walipunguzwa kasi baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Polisi Moro katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Sare hiyo imeifanya Yanga iwe na pointi 49 baada ya kucheza mechi 21, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 43, baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0.
Kukosekana kwa kiungo Haruna Niyonzima kulionekana dhahiri kuipunguza kasi Yanga, hasa katika safu yake ya ushambuliaji.
Beki Mbuyu Twite alilazimika kufanyakazi ya ziada dakika ya 24 kuokoa mchomo mkali wa mshambuliaji Mokili Rambo wa Polisi uliokuwa ukielekea kwenye nyavu.
Kipa wa Polisi, Kondo Salum naye alilazimika kufanya kazi ya ziada dakika ya 26 kupangua mpira wa kichwa wa beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga kufuatia kona maridadi ya David Luhende.
Said Bahanuzi ‘Spider Man’ aliikosesha Yanga bao la wazi, baada ya kuchelewa kuiwahi krosi nzuri ya Simon Msuva na mpira ukapitiliza hadi mikononi mwa kipa wa Polisi.
Nayo Azam ilijipatia bao la pekee katika mechi yake dhidi ya Ruvu Shooting dakika ya 44 lililofungwa na Kipre Tchetche.
Wakati huo huo, mabingwa watetezi Simba jana waliendelea kuchechemea baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Toto African katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CM Kirumba mjini Mwanza.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inabaki nafasi ya tatu kwa pointi zake 35 baada ya kucheza mechi 21, nyuma ya Azam yenye pointi 43 na Yanga 49 kileleni.
Toto African ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 25 lililofungwa na Mussa Saidi kabla Rashid Ismail kuisawazishia Simba dakika ya 2.
Mrisho Ngasa aliyeingia kipindi cha pili, aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 62 kwa shuti kali lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Toto ilisawazisha dakika ya 72 kwa bao lililofungwa na Selemani Kibuta baada ya mabeki wa Simba kujichanganya.
Monday, March 25, 2013
WEMA AMWOKOA KAJALA KWENDA JELA, AMLIPIA FAINI YA MILIONI 13
NA FURAHA OMARY
MSANII nyota wa filamu nchini Wema Sepetu, amemnusuru msanii mwenzake wa fani hiyo, Kajala Masanja kwenda kutumikia kifungo cha miaka 12 jela, baada ya kumlipia faini ya fedha taslim sh. milioni 13.
Wakati Kajala, ambaye amesota rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja akinusurika na kifungo hicho kutokana na adhabu iliyotolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mumewe Faraja Chambo, alihukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 12 kutokana na kushindwa kulipa faini ya sh.milioni 213.
Kajala na mumewe Chambo, walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Marchi 15, mwaka jana, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama ya kubadilisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi, Salasala, Dar es Salaam kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Akisoma hukumu hiyo jana katika ukumbi namba moja wa mahakama uliokuwa umejaa wasanii wa filamu, akiwemo Elizabeth Michael au Lulu, Mansour Awadh ‘Dk. Cheni’ na Wema, Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, alisema katika shitaka la kula njama, mahakama imejiuliza iwapo ni kweli washitakiwa, ambao ni mke na mume walikaa na kupanga kuuza nyumba hiyo.
“Baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka na wa utetezi na hoja za kisheria zilizowasilishwa, mahakama inajiuliza kama kweli washitakiwa walikula njama ya kutenda kosa. Hakukuwa na pingamizi kutoka kwa mawakili wa pande zote kwamba washitakiwa walikaa na kuuza nyumba na uuzaji huo ulikuwa halali au la,” alisema Hakimu Sundi alipokuwa akisoma hukumu hiyo huku Kajala, ambaye alikuwa katika kizimba akiangua kilio.
Hakimu Sundi alisema katika shitaka la pili, mahakama imeridhika na ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka kwamba kulikuwa na notisi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuzuia uuzaji wa nyumba.
Alisema kutokana na ushahidi huo, mahakama imewatia hatiani washitakiwa wote kwa sababu si kweli walikuwa hawafahamu kulikuwa na notisi hiyo, lakini waliidharau na kuuza nyumba.
Kuhusu shitaka la tatu la kutakatisha fedha haramu, Hakimu Sundi alisema mahakama inamtia hatiani mshitakiwa Chambo, kwa sababu imeridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka, kwamba wakati anafanyakazi katika benki ya NBC, alipata fedha kwa michezo aliyokuwa anaijua na kujenga nyumba na baadae kuficha ukweli kwa kuiuza baada ya TAKUKURU kujua hilo.
Hakimu Sundi alisema kuwa, Kajala hana hatia katika kosa hilo kwa kuwa hahusiki katika upatikanaji wa fedha hizo zilizotumika kujengea nyumba.
“Mahakama inawatia hatiani washitakiwa wote kwa kosa la kwanza na la pili na kosa la tatu linamtia hatiani Chambo pekee,” alisema Hakimu Sundi.
Baada ya kutiwa hatiani washitakiwa hao, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai, alidai hana kumbukumbu za makosa kwa mshitakiwa Kajala, lakini Chambo ana shitakiwa mahakamani hapo kwa makosa mengine.
Swai aliiomba mahakama hiyo, kutoa adhabu kali dhidi ya washitakiwa kwa kuwa makosa ya utakatishaji fedha haramu yamekuwa tatizo katika nchi na kwamba washitakiwa hao walikaidi amri ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kutouza kwa nyumba hiyo.
“Naomba washitakiwa wapewe adhabu kali kwa mujibu wa sheria husika ya utakatishaji fedha haramu,” aliomba Swai.
Kwa upande wa wakili wa washitakiwa, Barnarbas Lubuwa, aliiomba mahakama wakati inafikiria adhabu, ikumbuke kwamba washitakiwa, ambao ni mume na mke wana familia inawategemea, ambapo inaweza kuwaumiza wazazi huku familia ikiathirika.
Pia, alidai Kajala hajui upatikanaji wa fedha hizo, ambapo kuhusika kwake ni kutia saini mbele ya wakili kwa nafasi yake ya mke katika suala la uuzaji wa nyumba. Aliiomba mahakama katika kutoa adhabu izingatie mazingira.
HAKIMU ATOA ADHABU
Hakimu Sundi alisema katika shitaka la kula njama, washitakiwa walipe faini ya sh. milioni tano au kifungo cha miaka miwili jela. Shitaka la pili, washitakiwa walipe faini ya sh. milioni nane au kifungo cha miaka mitano na shitaka la tatu, ambalo ametiwa hatiani Chambo peke yake, alipe faini ya sh. milioni 200 au kifungo cha miaka mitano jela.
HALI ILIVYOKUWA BAADA YA ADHABU
Baada ya Hakimu Sundi kutoa adhabu hiyo, Kajala ambaye wakati hukumu hiyo ikitolewa, alikuwa akiangua kilio, aliendelea kulia kwa uchungu jambo lililowaliza wasanii wenzake na ndugu na jamaa zake waliokuwepo mahakamani hapo.
Mbali ya Kajala, mama mkwe wake naye alishindwa kujizuia, ambapo kwa wakati wote alikuwa akilia hadi washitakiwa hao walipopelekwa mahabusu wakisubiri hatma yao.
Akiwa katika chumba cha mahabusu, Kajala alikuwa akilia kwa wakati wote hali iliyowafanya washitakiwa wenzake kumfariji kwa kumbembeleza.
Kajala alipokuwa mahabusu, wasanii Cheni na Wema walikuwa wakihangaika huku na huko kuhakikisha wanamnusuru kwenda jela, ambapo waliamua kuitisha kikao cha wasanii wote na baadae Wema kuamua kwenda benki kuchukua fedha.
WASANII WAHAHA KUMNUSURU
Dk. Cheni alisema kuwa, Mwenyezi Mungu amesikia maombi yao kwa Kajala kutokana na mahakama kutoa adhabu ya kulipa faini au kifungo.
“Mwenyezi Mungu amesikia maombi yetu kwa Kajala. Tunashukuru kwa hilo. Tumekutana na kuchangishana, hata hivyo Wema amesema atalipa yeye faini yote na sasa ameenda benki kuchukua fedha,” alisema Dk. Cheni.
Baada ya Wema kurejea na kitita hicho cha fedha, nyuso za furaha zilitawala kwa Kajala, ndugu na jamaa zake ambapo baada ya kulipa faini hiyo, vicheko vilitawala mahakamani hapo, hali iliyowalazimu askari kuwaondoa wasanii hao na kwenda eneo la kusubiria kesi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Wema alisema kuwa ametoa fedha hizo kwa moyo mmoja kwa kuwa Kajala ni zaidi ya rafiki na zaidi ya ndugu.
“Kajala rafiki yangu, ndugu yangu na ni zaidi ya ndugu, kumsaidia kwangu sijaona kama nimepoteza, najua Mwenyezi Mungu atanilipia,”alisema Wema
KAJALA HUYOOOOOOO
Baada ya kutoka mahabusu, Kajala alimkumbatia mama yake mzazi, mdogo wake na wasanii wenzake, akiwemo Lulu huku akilia, jambo lililoangua vilio kwa wengine waliokuwa wakimsubiri wakiwemo ndugu zake.
Hata hivyo, msanii huyo hakuruhusiwa kuzungumza na mtu yeyote baada ya ndugu zake kumtaka aingie katika gari lililokuwa likimsubiri ili aende akapumzike nyumbani.
RAGE BADO MWENYEKITI HALALI SIMBA-TFF
MKUTANO Mkuu wa Dharura ulioitishwa na wanachama wa Simba, Machi 17 mwaka huu na kuuondoa uongozi wa klabu hiyo si halali kwa vile haukufuata taratibu, na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halitambui Kamati za Muda.
Uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana mjini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa.
Kamati imebaini kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 22(2) ya Katiba ya Simba, Mkutano Mkuu wa Dharura unaitishwa na Kamati ya Utendaji baada ya wanachama wasiopungua 500 kuwasilisha ombi hilo kwa maandishi na kujiorodhesha.
Mkutano huo haukuitishwa na Kamati ya Utendaji ya Simba.
Utaratibu huo haukufuatwa ambapo barua ya Mkutano huo iliandikwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo badala ya Kamati ya Utendaji ya Simba ambayo ndiyo matakwa ya Katiba ya Simba.
Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, Kamati ya Utendaji ndiyo inayoitisha Mkutano Mkuu wa Dharura baada ya kuhakiki uhai na uhalali wa wanachama waliojiorodhesha kuomba mkutano huo.
Kamati imesisitiza kuwa Katiba za wanachama wote wa TFF hazina kipengele cha kura ya kutokuwa na imani na uongozi (vote of no confidence), ndiyo maana uko nyuma wanachama wa Yanga, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) walipiga kura hiyo, na TFF kutotambua uamuzi wao.
Hata Katiba ya Simba haitoi mamlaka kwa Mkutano Mkuu wa Dharura kufukuza uongozi uliochaguliwa.
Katiba za wanachama wote wa TFF zimezingatia katiba mfano za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambazo zinasema kiongozi ataingia madarakani kwa uchaguzi, na si kuteuliwa (Kamati ya Muda).
Pia Kamati imesema endapo wanachama wa Simba wangefuata taratibu na uongozi ukakataa kuitisha mkutano, wanachama wangetuma ombi hilo TFF kupitia Kamati ya Sheria ili kutoa mwongozo kwa uongozi wa Simba .
TFF ina mamlaka ya kutoa adhabu kwa viongozi wa wanachama wake wanaokwenda kinyume cha Katiba zao. Pia Kamati imesisitiza kwa wanachama wa TFF kuitisha mikutano yao kwa mujibu wa taratibu na Katiba zao, na wale ambao muda umefika wafanye hivyo haraka.
STARS, MOROCCO ZAINGIZA MILIONI 226
MECHI ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania, Taifa Stars na Morocco, Simba wa Atlas iliyochezwa jana na wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 imeingiza Sh. 226,546,000.
Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 32,614 waliokata tiketi
kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 34,557,864.41, maandalizi ya mchezo Sh. 28,450,000 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 8,625,641.88.
Nyingine ni bonasi kwa timu ya Taifa Stars sh. 28,798,220.34, asilimia 15 ya uwanja sh. 18,917,141.01, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 25,222,854.67 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 6,305,713.67.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 71,885,135.82 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,783,428.20 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
Katika hatua nyingine, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amewapongeza wachezaji wa Taifa Stars na benchi lao la ufundi,washabiki, mdhamini na Serikali kwa kufanikisha ushindi wa jana.
Tenga amesema ushindi huo umetokana na ushirikiano kutoka kwa wadau wote, na hasa wachezaji walioonesha kiwango kikubwa kulinganisha na mechi zilizopita ikiwemo kiwango cha kujituma uwanjani.
Amesema Serikali ni mdau mkubwa wa mpira wa miguu katika miundombinu, usalama na idara zake mbalimbali ikiwemo Uhamiaji ambayo imefanikisha kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mechi hiyo.
Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 32,614 waliokata tiketi
kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 34,557,864.41, maandalizi ya mchezo Sh. 28,450,000 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 8,625,641.88.
Nyingine ni bonasi kwa timu ya Taifa Stars sh. 28,798,220.34, asilimia 15 ya uwanja sh. 18,917,141.01, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 25,222,854.67 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 6,305,713.67.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 71,885,135.82 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,783,428.20 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
Katika hatua nyingine, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amewapongeza wachezaji wa Taifa Stars na benchi lao la ufundi,washabiki, mdhamini na Serikali kwa kufanikisha ushindi wa jana.
Tenga amesema ushindi huo umetokana na ushirikiano kutoka kwa wadau wote, na hasa wachezaji walioonesha kiwango kikubwa kulinganisha na mechi zilizopita ikiwemo kiwango cha kujituma uwanjani.
Amesema Serikali ni mdau mkubwa wa mpira wa miguu katika miundombinu, usalama na idara zake mbalimbali ikiwemo Uhamiaji ambayo imefanikisha kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mechi hiyo.
Sunday, March 24, 2013
NANCY AZINDUA KITABU CHA NYOTA YAKO
Mrembo wa Tanzania wa mwaka 2007, Nancy Sumari na warembo wenzake wa zamani, Faraja Kotta na Jacqueline Ntuyabaliwe wakiwa na kitabu cha Nyota Yako kilichoandikwa na Nancy na kuzinduliwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
KALA JEREMIAH AJA NA KARIBU DAR ES SALAAM
MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Kala Jeremiah ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Karibu Dar es Salaam.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Kala alisema tayari kibao hicho kimeshaanza kupigwa kwenye vituo vya redio na kuonyeshwa kwenye vituo mbalimbali vya televisheni nchini.
Kala, ambaye ni mmoja wa wasanii walioibuliwa kupitia shindano la Bongo Star Search (BSS) alisema, kibao hicho kinaelezea matatizo ya maisha yanayowakumba vijana katika jiji la Dar es Salaam.
Katika kibao hicho, Kala anasimulia jinsi watu wenye maisha ya juu wasivyojua shida ya maji, chakula na usafiri wakati wale wenye maisha ya dhiki, maji kwao ni sawa na almasi.
Kala amerekodi kibao hicho huku kibao chake cha Dear God kikiwa bado kinaendelea kutamba kwenye vituo vya redio na luninga.
Msanii huyo alisema kwa sasa hana mpango wa kurekodi albamu mpya kwa vile bado albamu yake ya Pasaka inaendelea kufanya vizuri sokoni.
"Utaratibu wangu kwa sasa ni kurekodi wimbo mmoja mmoja, sina mpango wa kurekodi albamu. Kama ni kutafuta pesa, nitategemea zaidi matamasha ya muziki,"alisema msanii huyo.
CHOKI; HATUWEZI KULINGANA NA WACONGO KIMUZIKI
KIONGOZI wa bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo, Ally Choki amesema si rahisi kuyalinganisha mafanikio ya wanamuziki wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na yale ya Watanzania.
Choki alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, wanamuziki wa Congo wamepata mafanikio makubwa kimuziki kutokana na muziki wao kukubalika kimataifa.
Mbali na muziki wao kukubalika kimataifa, Choki alisema wanamuziki wa Congo kama vile Fally Ipupa na Koffi Olomide wanao udhamini wa uhakika ndio sababu wanaweza kukaa muda mrefu bila kurekodi albamu.
"Mauzo ya albamu moja ya mwanamuziki wa Congo kama vile Fally Ipupa na Koffi Olomide, yanaweza kuwafanya wapate pesa za kutumia kwa miaka minne hadi mitano, tofauti na wanamuziki wa Tanzania,"alisema Choki.
Alisema kutokana na ukweli huo, si rahisi kuyalinganisha mafanikio ya wanamuziki wa Congo na Tanzania kwa sababu yana tofauti kubwa.
Choki alitetea utaratibu wa bendi za Tanzania kufanya maonyesho matatu hadi manne kwa wiki kwa sababu ndiyo yanayowaingizia pesa nyingi kuliko mauzo ya albamu.
"Bendi za Tanzania zitaendelea kupata pesa kutokana na maonyesho ya kwenye kumbi za burudani na wenzetu wataendelea kutegemea mauzo ya albamu kwa sababu muziki wao ni wa uhakika,"alisisitiza Choki.
Kwa upande wake, mwimbaji nyota wa muziki wa dansi nchini, Ramadhani Masanja 'Banza Stone' amesema ni jambo lisilokwepeka kwa bendi za Tanzania kufanya maonyesho matatu au manne kwa wiki.
Banza alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, mauzo ya albamu hayawezi kuzitosheleza bendi kimapato kutokana na usimamizi mbovu wa sheria ya hatimiliki.
"Kwa hapa Tanzania, bendi kufanya maonyesho matatu au manne kwa wiki ni sawa kwa sababu ndizo siku, ambazo mashabiki wanakwenda kustarehe, hakuna ujanja mwingine wa kutuwezesha kupata mapato,"alisema.
NDANDA: MAONYESHO MATATU KWA WIKI HAYALIPI
KIONGOZI wa bendi ya muziki wa dansi ya Watoto wa Tembo International, Ndanda Kosovo amesema kwa sasa hana mpango wa kufanya maonyesho kila wiki kwa vile hayalipi.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Ndanda alisema ameamua kuja na staili mpya ya kufanya onyesho moja kila baada ya mwezi mmoja hadi mitatu ili kujipa sura ya kimataifa.
Ndanda alisema kufanya maonyesho matatu kwa wiki ni kujichosha na kwamba hakuna faida yoyote, ambayo wanamuziki wanaweza kuipata.
"Huko ni kutumika, kuanzia sasa nitafanya onyesho moja kila baada ya kipindi fulani, nikipata pesa natumia, zikiisha nafanya onyesho lingine,"alisema mwanamuziki huyo wa zamani wa bendi ya FM Academia
Ndanda alisema lengo lake ni kuwa kama baadhi ya wanamuziki maarufu barani Afrika kama vile Fally Ipupa, Koffi Olomide, JB Mpiana na Werrason.
Mwimbaji huyo anayependa kupaka rangi nywele zake alisema, wanamuziki wengi wa kiafrika wanaopiga muziki Arabuni, wamekuwa wakifanyakazi siku saba kwa wiki, lakini hakuna faida yoyote wanayoipata.
"Wanapiga muziki kuanzia Jumatatu hadi Jumatatu. Wanatumika wiki nzima, lakini hakuna faida yoyote ya maana wanayoipata,"alisema mwimbaji huyo, ambaye kuna wakati aliwahi kutamba kwa miondoko ya Wajelajela Origino.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za ushirikina katika muziki, Ndanda alisema haamini iwapo vitu hivyo vinafanyika kwa vile hapendi kuvifuatilia.
Alisema wakati alipokuwa katika bendi ya FM Academia, aliwahi kushutumiwa na baadhi ya wanamuziki wenzake kwamba anawafanyia ushirikina, lakini hakuwahi kufanya kitu kama hicho.
Ndanda alisema masuala ya ushirikina yanatokana na imani ya mtu na kwamba inawezekana wapo wanamuziki, ambao wamekuwa wakitegemea ushirikina katika kupata mafanikio.
Mwanamuziki huyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) aliibuka na bendi ya Watoto wa Tembo International mwaka 2010.
Bendi hiyo ilikuwa ikiundwa na wanamuziki 18, wakiwemo waimbaji wanne, marapa wawili, wapiga vyombo sita na wacheza shoo watano. Mkurugenzi wa bendi hiyo alikuwa Jane Mawole.
Watoto wa Tembo ilikuwa ikifanya maonyesho yake kwenye hoteli zilizoko mbuga ya Mikumi mkoani Morogoro na kwenye baadhi ya hoteli za mjini Arusha.
Miongoni mwa vibao vilivyoitambulisha bendi hiyo ni pamoja na Afrika yetu, Usitoe mimba, Uniache, Kosovo Kiboko ‘Jambembe’ na Cecika. Bendi hiyo ilikuwa ikipiga muziki wake kwa kutumia miondoko ya Lilolo na Swala-k-Lakaswa.
Licha ya kupata umaarufu katika bendi ya FM Academia, Ndanda hana uhusiano mzuri na wanamuziki wa bendi hiyo, hasa kiongozi wake, Nyoshi El-Saadat.
Wanamuziki hao wawili wamekuwa wakitoleana lugha za kukashifiana mara kwa mara huku kila mmoja akijigamba kuwa juu ya mwenzake.
Ndanda pia aliwahi kukaririwa akisema kuwa, hana muda wa kusikiliza nyimbo za bendi za Kitanzania kwa kile alichodai kuwa, hazina ubunifu.
"Sina bifu na wanamuziki wa FM Academia ama Akudo Impact, lakini ukweli ni kwamba muda mwingi huwa napenda kusikiliza nyimbo za wasanii wa nje kwa vile wanafanya kweli katika muziki,"alisema.
"Sijawahi kusikiliza nyimbo za Akudo ama FM Academia kwa sababu ubunifu ni sifuri. Siwapondi wala sizungumzi hivi kwa nia mbaya, huu ndio ukweli wenyewe,"aliongeza.
Kuna wakati Ndanda aliwahi kwenda Marekani, ambako aliishi kwa zaidi ya miaka miwili akiwa anapiga muziki na bendi mbalimbali zinazoundwa na wanamuziki wa kiafrika.
VICENT KIGOSI 'RAY' : WATOVU WA NIDHAMU HAWANA NAFASI BONGO MOVIE UNIT
MSANII nyota wa filamu nchini, Vicent Kigosi 'Ray' amesema wameamua kuunda klabu ya Bongo Movie Unit kwa lengo la kusaidiana katika shida na raha.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Ray alisema wanachama wa klabu hiyo ni wasanii wa fani ya filamu wanaofuata na kuzingatia maadili ya uanachama.
Ray, ambaye ni mwenyekiti wa klabu hiyo alisema, awali ilikuwa ikiundwa na wasanii wachache, lakini baadaye waliamua kupanua wigo kwa kuwashirikisha wasanii wote wa fani hiyo.
Alisema lengo la klabu hiyo ni kuwa na wasanii wenye nidhamu na wanaofuata maadili na kuongeza kuwa, watakaokwenda kinyume watatimuliwa.
Ray alisema hawakuweza kumsaidia msanii mwenzao, Matumaini tangu alipokuwa akiugua nchini Msumbiji hadi aliporejeshwa nchini kwa sababu suala lake lilikuwa likishughulikiwa na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF).
"Lakini wapo baadhi yetu wanachama wa Bongo Movie Unit, ambao tuliamua kumsaidia mmoja mmoja,"alisema.
Akizungumzia tatizo la baadhi ya wasanii wa kike kupenda kuvaa nusu uchi, Ray alisema inategemea ni katika mazingira gani.
Alisema kama msanii anacheza filamu inayozungumzia vitendo vya umalaya, ni lazima avae mavazi ya aina hiyo, lakini kama anafanya hivyo nje ya kazi, anakuwa na lake jambo.
"Unajua baadhi ya wasanii wa kike wameingia kwenye fani hii kwa lengo la kuuza sura. Wanataka waonekane kwenye filamu ili wapate wanaume wa kuwaoa ama kuwapa fedha ili wapate nyumba na magari. Hawa ndio wanaotuharibia fani yetu,"alisema.
Hata hivyo, Ray alivilaumu baadhi ya vyombo vya habari hasa magazeti ya udaku kwamba, vimekuwa vikiwachafua wasanii kwa makusudi kwa lengo la kuuza magazeti yao.
"Mimi sioni sababu kwa nini vyombo vya habari vifuatilie maisha binafsi ya msanii anapokuwa sehemu ya starehe. Huku ni kushusha heshima ya wasanii,"alisema.
Ray alisema uamuzi wao wa kujichuja katika klabu ya Bongo Movie Unit umelenga kujenga heshima ya wasanii wa fani hiyo na pia kuondokana na vitendo vya utovu wa nidhamu.
Akitoa mfano, alisema hivi karibuni waliamua kumsimamisha uanachama Jacqueline Pentzel baada ya kukiri makosa aliyoyafanya na kuomba radhi.
Alisema si kweli kwamba wamemtimua msanii huyo kwenye klabu yao bali bado wanatafakari hatua za kuchukua dhidi yake.
"Kumtimua mwanachama katika klabu yetu si kumrekebisha. Dawa ni kumuweka sawa ili ajirekebishe,"alisema.
Ray alisema kazi ya kucheza filamu ilikuwa ikichukuliwa kuwa ni ya watu wasio na elimu, lakini hivi sasa imekuwa kivutio kwa wasomi, ambao wameanza kumiminika kwa wingi kuicheza hivyo inapaswa kuheshimiwa.
STARS YAIUA MOROCCO
Katika mechi hiyo ya kundi C iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars ilipata mabao hayo matatu kipindi cha pili.
Mshambuliaji Thomas Ulimwengu, aliyeingia kipindi cha pili badala ya Mrisho Ngassa, alianza kuzitikisa nyavu za Morocco dakika ya 46 baada ya kupokea pasi kutoka kwa beki Erasto Nyoni.
Mbwana Samatta aliiongezea Taifa Stars bao la pili dakika ya 66 baada ya kuambaa na mpira kutoka wingi ya kushoto na kufumua shuti lililompita kipa Lamyagir Dadir.
Samatta, ambaye pamoja na Ulimwengu wanacheza soka ya kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, aliongeza bao la tatu dakika ya 79 baada ya gonga safi kati yao.
Morocco ilipata bao la kujifariji dakika ya 89 lililofungwa na Elarabi Yousser baada ya kipa Juma Kaseja wa Taifa Stars kutema shuti la mchezaji mwingine wa timu hiyo.
Morocco ililazimika kumaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji 10 baada ya Abdelaziz kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi, Neermal Bodhoo wa Afrika Kusini kwa kosa la kutoa lugha chafu.
Kutokana na ushindi huo, Taifa Stars inaendelea kushika nafasi ya pili katika kundi hilo, ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi tatu.
Ivory Coast, ambayo mwishoni mwa wiki iliyopita iliibamiza Gambia mabao 3-0, bado inaongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi saba wakati Morocco imeambulia pointi mbili.
Tuesday, March 19, 2013
SMALL KIDS, MORO UNITED, MORANI ZASHUKA DARAJA
Timu tatu zimeshuka daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kurudi Ligi ya Mkoa msimu ujao wa 2013/2014 baada ya kushika nafasi za mwisho katika ligi hiyo msimu huu 2012/2013 iliyomalizika wikiendi iliyopita.
Small Kids ya Rukwa imeporomoka kutoka kundi A baada ya kuondolewa kwenye michuano hiyo mapema kwa kushindwa kufika uwanjani kwenye moja ya mechi zake. Kwa mujibu wa kanuni matokeo yote ya mechi ilizocheza yalifutwa.
Moro United ya Dar es Salaam ndiyo iliyoaga FDL kutoka kundi B baada ya kumaliza mechi zake ikiwa na pointi tatu. Wakati kutoka kundi C timu iliyoshuka ni Morani ya Manyara iliyomaliza ligi ikiwa na pointi kumi na moja.
Timu zilizopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2013/2014 ni Mbeya City ya Mbeya iliyoongoza kundi A ikiwa na pointi 31, vinara wa kundi B timu ya Ashanti United ya Dar es Salaam yenye pointi 29 wakati Rhino Rangers ya Tabora imepanda kutoka kundi C ikiwa na pointi 32.
Mwamuzi Msaidizi wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Leslie Liunda ameteuliwa kuwa mtathimini wa waamuzi (referee assessor) kwenye moja ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia.
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Liunda kutathimini waamuzi kwenye mechi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Libya itakayochezwa Jumapili (Machi 24 mwaka huu).
Mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Martyrs jijini Kinshasa kuanzia saa 9.30 alasiri kwa saa za Afrika ya Kati (CAT).
Waamuzi watakaochezea mechi hiyo William Selorm Agbovi atakayekuwa mwamuzi wa kati, Malik Alidu Salifu (mwamuzi msaidizi namba moja), David Laryea (mwamuzi msaidizi namba mbili) na mwamuzi wa mezani (fourth official) Cecil Amatey Fleischer. Waamuzi wote hao wanatoka Ghana.
KUZIONA STARS, MOROCCO BUKU TANO
Kiingilio cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku mbili ya mchezo (Ijumaa na Jumamosi) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi. Vilevile tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
Washambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamewasili nchini jana usiku na kwenda moja kwa moja kambini.
Ujio wa washambuliaji hao unafanya idadi ya wachezaji walioripoti kambini kufikia 20 kati ya 23 walioitwaa baada ya mshambuliaji Khamis Mcha aliyekuwa na kikosi cha timu yake ya Azam nchini Liberia naye kuripoti kambini leo asubuhi.
Wachezaji John Bocco na makipa Mwadini Ally na Aishi Manula ambao pia nao walikuwa Liberia na timu yao ya Azam wataripoti kambini leo alasiri. Wachezaji hao ni sehemu ya msafara wa timu ya Azam ambao utakuja na ndege ya mchana kutokea Nairobi kwa vile ile ya asubuhi waliyotangulia nayo wenzao kuwa imejaa.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Kim Poulsen leo inaendelea na mazoezi Uwanja wa Taifa. Mazoezi hayo yataanza saa 9 alasiri.
Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku mbili ya mchezo (Ijumaa na Jumamosi) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi. Vilevile tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
Washambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamewasili nchini jana usiku na kwenda moja kwa moja kambini.
Ujio wa washambuliaji hao unafanya idadi ya wachezaji walioripoti kambini kufikia 20 kati ya 23 walioitwaa baada ya mshambuliaji Khamis Mcha aliyekuwa na kikosi cha timu yake ya Azam nchini Liberia naye kuripoti kambini leo asubuhi.
Wachezaji John Bocco na makipa Mwadini Ally na Aishi Manula ambao pia nao walikuwa Liberia na timu yao ya Azam wataripoti kambini leo alasiri. Wachezaji hao ni sehemu ya msafara wa timu ya Azam ambao utakuja na ndege ya mchana kutokea Nairobi kwa vile ile ya asubuhi waliyotangulia nayo wenzao kuwa imejaa.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Kim Poulsen leo inaendelea na mazoezi Uwanja wa Taifa. Mazoezi hayo yataanza saa 9 alasiri.
MGONGOLWA KUIHUKUMU SIMBA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea barua kutoka uongozi wa Simba ikielezea kutotambua mkutano ulioandaliwa na wanaodaiwa kuwa wanachama wake na kufanyika jana ukumbi wa Starlight, Dar es Salaam.
Vilevile katika barua hiyo uongozi wa Simba umeahidi kuitisha mkutano wa wanachama wake. Mkutano huo utaitishwa na Mwenyekiti wa Simba kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo.
Kutokana na hali hiyo, TFF imeitisha mara moja kikao cha Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kinachoongozwa na Wakili Alex Mgongolwa kwa ajili ya kutoa mwongozo kwa matukio ya aina hiyo.
Hata hivyo, TFF tunasisitiza kwa wanachama wetu ikiwemo Simba kuwa wanachama wanapotaka kufanya uamuzi wowote ule wanatakiwa kuzingatia katiba na kanuni zilizopo.
TFF YAUPONGEZA UONGOZI MPYA WA TAFCA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi (Machi 16 mwaka huu) mjini Dodoma.
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAFCA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia taaluma ya ukocha nchini.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TAFCA chini ya uenyekiti wa Oscar Don Koroso aliyeibuka mshindi kwa kura zote za ndiyo baada ya kukosa mpinzani.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya TAFCA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA chini ya Ramadhan Mambosasa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Safu nzima ya uongozi wa TAFCA iliyochaguliwa inaundwa na Dk. Oscar Dan Koroso (Mwenyekiti), Lister Manyara (Makamu Mwenyekiti), Michael Bundala (Katibu Mkuu), Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Dismas Haonga (Mhazini), Wilfred Kidao (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF).
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliochaguliwa ni Jemedari Saidi, George Komba na Magoma Rugora.
RATIBA YA STARS HII HAPA
Taifa Stars itacheza mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka nchini Brazil dhidi ya Morocco. Mechi hiyo itachezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Jumamosi, Machi 16- Wachezaji kuanza kuripoti kambini
Jumapili, Machi 17- Mazoezi Uwanja wa Karume- Saa 2 asubuhi
Jumatatu, Machi 18- Mazoezi Uwanja wa Karume- Saa 9 alasiri
Jumanne, Machi 19- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 9 alasiri
Jumatano, Machi 20- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 2 asub na saa 9 alasiri
Alhamisi, Machi 21- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 9 alasiri
Ijumaa, Machi 22- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 9 alasiri
Jumamosi, Machi 23- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 10.30 jioni
TFF YAIPONGEZA AZAM
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaipongeza klabu ya Azam kwa ushindi wa mabao 2-1 ilioupata timu yake katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
Mechi hiyo dhidi ya Barrack Young Controllers II ilichezwa jana jijini Monrovia, na timu hizo zitarudiana wikiendi ya Aprili 6 au 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo unaiweka Azam chini ya kocha wake Stewart John Hall katika mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya mechi ya marudiano. Bila shaka ushindi wa timu ya Azam pamoja na mambo mengine umechangiwa na klabu hiyo kujipanga vizuri.
Hata hivyo ushindi huo bado ni changamoto kwa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa Azam kuhakikisha unajipanga vizuri kwa mechi ya marudiano kwa vile mpira wa miguu una matokeo ya aina tatu; kushinda, kutoka sare au kufungwa.
Msafara wa timu ya Azam unaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Blassy Kiondo unatarajiwa kurejea nchini kesho alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi.
Mechi hiyo dhidi ya Barrack Young Controllers II ilichezwa jana jijini Monrovia, na timu hizo zitarudiana wikiendi ya Aprili 6 au 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo unaiweka Azam chini ya kocha wake Stewart John Hall katika mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya mechi ya marudiano. Bila shaka ushindi wa timu ya Azam pamoja na mambo mengine umechangiwa na klabu hiyo kujipanga vizuri.
Hata hivyo ushindi huo bado ni changamoto kwa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa Azam kuhakikisha unajipanga vizuri kwa mechi ya marudiano kwa vile mpira wa miguu una matokeo ya aina tatu; kushinda, kutoka sare au kufungwa.
Msafara wa timu ya Azam unaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Blassy Kiondo unatarajiwa kurejea nchini kesho alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi.
Monday, March 18, 2013
AZAM YAJIWEKA PAZURI KOMBE LA SHIRIKISHO
AZAM FC imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kucheza raundi ya tatu ya michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho baada ya kuichapa Barrack Young Controllers ya Liberia mabao 2-1.
Katika mechi hiyo ya awali ya raundi ya pili iliyochezwa jana kwenye uwanja wa Antonette Tubman mjini Monrovia, Azam ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0.
Kwa matokeo hayo, Azam sasa inahitaji sare yoyote katika mechi ya marudiano itakayochezwa wiki mbili zijazo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Seif Abdalla Karihe aliibuka shujaa wa Azam baada ya kuifungia bao la pili na la ushindi dakika ya 90. Seif aliingia uwanjani dakika 10 kabla ya kufunga bao hilo, akichukua nafasi ya Kipre Tchetche.
Barrack ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 44 lililofungwa na Junior Barshall.
Bao la kusawazisha la Azam lilifungwa na Humphrey Mieno dakika 10 baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Jabir Azizi na Khamis Mcha.
WANACHAMA SIMBA WAMNG'OA RAGE, AUFANANISHA MKUTANO WAO NA KIKAO CHA HARUSI
WANACHAMA wa klabu ya Simba jana walitekeleza azma yao kwa vitendo baada ya kutangaza kumng'oa madarakani mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage.
Mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Star Light, Dar es Salaam, ulihudhuriwa na wanachama wanaodaiwa kufika 600.
Wanachama hao walipiga kura ya kumkataa Rage kwa madai kuwa, uongozi wake umekuwa ukiendesha klabu hiyo kinyume cha katiba.
Katika mkutano huo, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope na makamu mwenyekiti wa kamati ya fedha, Rahma Al-Kharoos waliteuliwa kuwa viongozi wa kamati ya muda ya Simba.
Jukumu la viongozi hao litakuwa kuisimamia timu hadi michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakapomalizika.
Hata hivyo, bado kuna utata kuhusu uhalali wa wanachama waliohudhuria mkutano huo kwa vile hakukuwa na leja ya wanachama kwa ajili ya kuwabaini iwapo ni halali au la.
Vilevile kuna wasiwasi iwapo wanachama hao ni hai kwa vile hakukuwa na mtu wa kuhakiki iwapo wamelipia kadi zao za uanachama kwa mujibu wa katiba.
Mkutano huo uliodumu kwa saa mbili, uliendeshwa na Dk. Mohamed Wandi, ambaye alitoa fursa kwa wanachama kujadili mustakabali wa Simba.
Idadi kubwa ya wanachama walimkataa Rage kwa madai kuwa, ameivuruga timu na amekuwa akisema uongo. Pia waliuelezea uamuzi wake wa kumuuza mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwamba uliidhoofisha timu.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka India ambako amelazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu, Rage aliufananisha mkutano huo kuwa ni sawa na kikao cha harusi.
Alisema wanachama hao hawana ubavu wa kumng'oa kwa sababu mkutano waliouitisha ulikuwa kinyume cha katiba na baadhi ya wanachama waliohudhuria ni mamluki kwa vile si wanachama wa Simba.
14 WARIPOTI KAMBINI STARS
Wachezaji walioripoti ni nahodha Juma Kaseja kutoka Simba na msaidizi wake Aggrey Morris wa Azam, Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba), Shomari Kapombe (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
Wengine ni Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mrisho Ngasa (Simba) na Simon Msuva (Yanga).
Wachezaji Hussein Shariff, Issa Rashid na Shabani Nditi ambao timu yao ya Mtibwa Sugar jana ilicheza mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mjini Turiani wataripoti kambini leo jioni.
Kikosi hicho kitakamilika Jumanne asubuhi baada ya wachezaji walio katika kikosi cha Azam nchini Liberia kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho kurejea nchini. Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo (DRC) wanatarajiwa kutua nchini kesho usiku.
MECHI MBILI ZA YANGA KUIVUA UBINGWA SIMBA
UBINGWA wa michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara umezidi kunukia kwa Yanga baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0 katika mechi iliyopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeiwezesha Yanga kuwa na pointi 48 baada ya kucheza mechi 20 na sasa inahitaji kushinda mechi mbili ili iweze kuwavua ubingwa, mabingwa watetezi Simba.
Iwapo Yanga itashinda mechi hizo mbili, itafikisha pointi 54, ambazo Simba haitaweza kuzifikia hata kama itashinda mechi zake sita zilizosalia. Simba itakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 52.
Katika mechi zake mbili zijazo, Yanga itakipiga na Polisi Morogoro Machi 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kabla ya kukipiga na JKT Oljoro Aprili 10 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Ruvu Shooting na Yanga iliyochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 62,228,000 kutokana na watazamaji 10,929.
Viingilio katika mechi hiyo namba 146 iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 14,336,764.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 9,492,406.78.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,289,880.48, tiketi sh. 4,136,390, gharama za mechi sh. 4,373,928.29, Kamati ya Ligi sh. 4,373,928.29, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,186,964.14, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 850,486.06 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 850,486.06.
WAANGOLA KUZICHEZESHA STARS NA MOROCCO
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeteua waamuzi kutoka Angola kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas).
Mechi hiyo ya kundi C itachezwa Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne na kufuatiwa na Taifa Stars yenye pointi tatu.
Mwamuzi wa mechi hiyo ni Helder Martins de Carvalho wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Inacio Manuel Candido huku Ricardo Daniel Cachicumi akiwa mwamuzi msaidizi namba mbili. Mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Antonio Muachihuissa Caxala.
Waamuzi hao watawasili nchini saa 1.20 usiku Machi 22 mwaka huu kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Luanda, Angola kupitia Nairobi, Kenya.
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa David Fani kutoka Botswana anatarajiwa kuwasili Machi 22 mwaka huu saa 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.
Naye mtathmini wa waamuzi (referee assessor) Neermal Boodhoo kutoka Afrika Kusini atawasili nchini Machi 22 mwaka huu 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.
Thursday, March 14, 2013
MAMILIONI YA OKWI YATAFUNWA
UONGOZI wa klabu ya Simba umepanga kutuma viongozi wake watatu kwenda Tunisia kufuatilia malipo ya ada ya uhamisho wa mshambuliaji, Emmanuel Okwi aliyeuzwa kwa klabu ya Etoile du Sahel.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, viongozi hao wanatarajiwa kuondoka nchini mwishoni mwa wiki hii baada ya taratibu zote muhimu kukamilika.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, uongozi wa Simba umefikia uamuzi huo baada ya kuzuka kwa utata kuhusu dola 300,000 (sh. milioni 450) zilizolipwa na Etoile du Sahel kwa Simba kwa ajili ya ada ya uhamisho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, inasemekana kuwa Etoile du Sahel ilishalipa nusu ya fedha hizo kwa Simba, lakini baadhi ya viongozi wameamua kuzitafuna.
Okwi aliuzwa kwa klabu hiyo mwishoni mwa mwaka jana, ikiwa ni siku chache baada ya kuongeza mkataba mpya na Simba na kulipwa mamilioni ya fedha.
"Unajua kumekuwepo na taarifa tofauti kuhusu malipo hayo, ndio sababu tumeamua kufuatilia kwa karibu ili tujue ukweli. Tumewatuma viongozi watatu kwenda Tunisia kufuatilia malipo hayo,"alisema mjumbe mmoja wa kamati ya utendaji ya Simba, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Aliongeza kuwa, taarifa walizozipata zinaeleza kuwa, Etoile du Sahel ilishalipa nusu ya fedha hizo kwa kiongozi mmoja wa Simba na kuahidi kumalizia fedha zilizobaki mwezi uliopita.
"Ajabu ni kwamba viongozi wote wanadai kuwa, hakuna fedha zilizolipwa. Haiwezekani, tunahisi hapa kuna ujanja umefanyika, tutachunguza hadi tupate ukweli,"alisema mjumbe huyo.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, iwapo ni kweli fedha hizo zimelipwa na baadhi ya viongozi wamezitafuta, watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa uanachama.
Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alikaririwa akisema kuwa, klabu yake inadai fedha nyingi kutoka kwa watu mbalimbali, ikiwemo klabu ya Etoile Du Sahel, ambayo alisema wanaidai zaidi ya sh. milioni 450 za mauzo ya Okwi.
WALIOIUA CAMEROON WAITWA TENA TAIFA STARS
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen ametangaza majina ya wachezaji 23 watakaoingia kambini Jumamosi kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi dhidi ya Morocco.
Mechi hiyo ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 zitakazofanyika Brazil, itachezwa Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kim, wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini Machi 15 mwaka huu katika hoteli ya Tansoma iliyopo barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
Wachezaji walioitwa ni makipa Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha, Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Mwadini Ally (Azam).
Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba) na Simon Msuva (Yanga).
Benchi la ufundi la Taifa Stars linaundwa na Sylvester Marsh (kocha msaidizi), Juma Pondamali (kocha wa makipa), Leopold Tasso (meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (daktari wa timu), Frank Mhonda (mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (mtunza vifaa).
Mechi hiyo ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 zitakazofanyika Brazil, itachezwa Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kim, wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini Machi 15 mwaka huu katika hoteli ya Tansoma iliyopo barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
Wachezaji walioitwa ni makipa Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha, Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Mwadini Ally (Azam).
Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba) na Simon Msuva (Yanga).
Benchi la ufundi la Taifa Stars linaundwa na Sylvester Marsh (kocha msaidizi), Juma Pondamali (kocha wa makipa), Leopold Tasso (meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (daktari wa timu), Frank Mhonda (mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (mtunza vifaa).
FIFA YASITISHA MPANGO WA KULETA WAJUMBE WAKE TZ
SHIRIKISHO la Soka la Dunia (FIFA) limesitisha kwa muda mpango wake wa kutuma ujumbe nchini kuja kuchunguza kiini cha mgogoro uliojitokeza katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, FIFA imeahirisha kutuma ujumbe wake hadi serikali itakapofikia mwafaka na shirikisho hilo.
"FIFA wamesema wameahirisha kuja hadi suala la serikali kuingilia kati masuala ya soka litakapopatiwa ufumbuzi,"alisema Wambura.
FIFA iliahidi kutuma wajumbe wake kuja nchini kuchunguza mgogoro huo baada ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kuwasilisha malalamiko kwa shirikisho hilo wakipinga kuenguliwa kwao.
Hata hivyo, kabla ya FIFA kutuma ujumbe wake, serikali ilitangaza kuifuta katiba ya FIFA ya 2012 kwa madai kuwa, usajili wake ulifanyika bila kufuata taratibu.
Mbali na kufuta katiba hiyo, serikali iliitaka TFF iitishe mkutano wa marekebisho ya katiba na kuitisha uchaguzi mkuu kwa kufuata katiba ya 2006.
Hata hivyo, TFF imekuwa ikisita kutekeleza maagizo hayo kwa madai kuwa, katiba ya shirikisho hilo hairuhusu serikali kuingilia kati masuala ya soka.
TFF ilitoa waraka wiki hii kutoka kwa FIFA, ikitishia kuifungia Tanzania, iwapo serikali itaendelea kuingilia kati masuala yanayohusu soka.
Waraka huo ulieleza kuwa, FIFA imepata taarifa kupitia kwenye mitandao mbalimbali, zikieleza kuwa serikali imeitaka TFF ianze upya mchakato wa uchaguzi kwa kufuata katiba ya 2006.
Kupitia barua hiyo, FIFA imeeleza kuwa, nchi zote wanachama zinatakiwa kuendesha shughuli zake kwa uhuru bila ya kuingiliwa na mtu kama ilivyoelezwa katika ibara ya 13 na 17 za katiba ya shirikisho.
Hata hivyo, waraka na maelezo hayo ya FIFA yamepingwa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala ambaye alisema wiki hii kuwa, serikali haiwezi kupokea maagizo kutoka shirikisho hilo kwa vile Tanzania ni nchi huru na yenye taratibu zake.
Makala alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa, iwapo Tanzania itafungiwa na FIFA, wanaopaswa kulaumiwa ni viongozi wa TFF kwa kutoa taarifa za upotoshaji kwa shirikisho hilo.
SEMINA ELEKEZI COPA COCA-COLA MACHI 19
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema, semina elekezi kwa ajili ya michuano ya Copa Coca-Cola 2013, inatarajiwa kufanyika Machi 19 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, washiriki wa semina hiyo wanatakiwa kuripoti kwenye ofisi za shirikisho hilo Machi 18 mwaka huu.
Alisema washiriki hao ni makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Aliwataja washiriki wengine kuwa ni waratibu wa mikoa wa mashindano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
Wambura alisema barua za mwaliko kwa ajili ya semina hiyo tayari zimetumwa kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa.
SIMBA WAMWANGUKIA HANSPOPE
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Simba, Rahma Al-Kharoos akisalimiana na wanachama wa tawi la Mpira Pesa alipotembelea tawi hilo mwishoni mwa wiki iliyopita Magomeni, Dar es Salaam. (Picha kwa hisani ya Simba).
KLABU ya Simba imepanga kumshawishi mwenyekiti wake wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope abadili uamuzi wake wa kujiuzulu wadhifa huo.
Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, wameunda kamati ya watu watatu kwa ajili ya kwenda kumshawishi Hanspope.
Itang'are, maarufu kwa jina la Kitare alisema uamuzi wa kuunda kamati hiyo ulifikiwa katika kikao cha viongozi wa matawi ya Simba ya mjini Dar es Salaam kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema kamati hiyo ilitarajiwa kukutana na Hanspope wakati wowote kuanzia jana.Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina ya wajumbe wa kamati hiyo, lakini alisema ni watu maarufu na wanaoheshimika ndani ya Simba.
Kaimu Makamu Mwenyekiti huyo wa Simba alisema uongozi umeshaanza kuchukua hatua za kunusuru kuzuka kwa mgogoro ndani ya klabu hiyo, ikiwa ni pamoja na kumaliza tofauti zilizojitokeza kati yake na tawi la Mpira Pesa.
Alisema baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji ya Simba, wakiongozwa na Rahma Al-Kharoos walitembelea tawi hilo mwishoni mwa wiki iliyopita na kuzungumza na wanachama.
"Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wanachama wote wa Simba kuendeleza utulivu na mshikamano ndani ya klabu ili tuwe kitu kimoja. Tukiwa kitu kimoja tutaweza kutatua matatizo yetu kwa ufanisi. Tukigawanyika tutazidi kuharibikiwa," alisema.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa tawi la Mpira Pesa, Ustaadh Masoud amesema hawana nia mbaya dhidi ya uongozi wa Simba, isipokuwa kuna mambo ambayo ni lazima yawekwe sawa kwa lengo la kuondoa tofauti zilizokuwapo siku za nyuma.
LYON, TOTO, POLISI ZACHUNGULIA KABURI
WAKATI michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara ikiwa inaelekea ukingoni, timu za African Lyon, Toto African na Polisi Moro zipo kwenye hatari ya kushuka daraja.
Lyon inashika mkia katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi 20, ikifuatiwa na Toto African yenye pointi 14 na Polisi Moro yenye pointi 17.
Timu hizo tatu kila moja imesaliwa na mechi sita na hazina uwezo wa kushinda zote ili kujinusuru katika janga hilo la kuteremka daraja.
Iwapo Lyon itashinda mechi hizo sita, itafikisha pointi 31, Toto African itafikisha pointi 32 wakati Polisi Moro itafikisha pointi 35.
Timu nyingine, ambayo ikitereza inaweza kushuka daraja ni JKT Ruvu inayoshika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 19 baada ta kucheza mechi 19. Iwapo JKT Ruvu itashinda mechi zote zilizosalia, itafikisha pointi 37.
Wakati timu hizo nne zikipigana vikumbo kuepuka kushuka daraja, Yanga na Azam zinachuana vikali kuwania ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Yanga inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 19, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 37 na Simba yenye pointi 34.
Kwa sasa, Yanga inahitaji kushinda mechi nne ili iweze kuivua ubingwa Simba. Iwapo itashinda mechi hizo nne, itafikisha pointi 57, ambazo Simba haitaweza kuzipata.
Wakati huo huo, Yanga inaongoza kwa kufunga mabao katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Hadi sasa, Yanga imefunga mabao 36, ikifuatiwa na Azam yenye mabao 32 na Simba yenye mabao 28.
Coastal Union na Mtibwa Sugar zimefunga mabao 22 kila moja, zikifuatiwa na Kagera Sugar na Ruvu Shooting zilizofunga mabao 21 kila moja. JKT Oljoro imefunga mabao 20.
African Lyon ndiyo inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi baada ya nyavu zake kutikisika mara 32, ikifuatiwa na JKT Ruvu iliyofungwa mabao 30 na Toto African iliyofungwa mabao 28.
BRANDTS: MECHI ZOTE ZILIZOSALIA KWETU NI FAINALI
KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts ametamba kuwa, mechi zote zilizosalia katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara kwao ni sawa na fainali hivyo hawawezi kuzipuuza.
Brandts alisema hayo baada ya mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika juzi kwenye uwanja wa Mabatini uliopo Kijitonyama, Dar es Salaam.
Kocha huyo alisema wanaipa uzito mkubwa mechi kati yao na Ruvu Shooting itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa vile wapinzani wao si timu ya kubeza.
Katika mechi ya kwanza kati ya timu hizo iliyochezwa Oktoba 20 mwaka jana, Yanga iliichapa Ruvu Shooting mabao 3-2.
Yanga inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 19 wakati Ruvu Shooting inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 18.
"Ninakiandaa kikosi changu kuhakikisha kinapata pointi tatu katika kila mchezo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa,"alisema Brandts.
"Kila mchezo tunaocheza kwa sasa ni fainali kwetu, kila timu inahitaji kupata pointi ili kujiweka katika nafasi nzuri, na sisi pia tunahitaji kupata pointi tatu katika kila mchezo. Nadhani mechi itakuwa ngumu,"aliongeza kocha huyo.
Katika mechi yake iliyopita, Yanga iliwalaza ndugu zao wa Toto African bao 1-0. Mechi hiyo ilipigwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, daktari wa Yanga, Nassoro Matuzya amesema wachezaji Kevin Yondan na Saidi Bahanuzi wameanza mazoezi na wenzao baada ya kuwa majeruhi kwa siku kadhaa.
Nassoro alisema Yondan alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kidole gumba, aliyoyapata katika mechi dhidi ya Toto African wakati Bahanuzi alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya msuli wa kisigino.
Daktari huyo alisema pia kuwa, beki Ladislaus Mbogo ameshafanyiwa upasuaji wa uvimbe shavuni na hali yake inaendelea vizuri.
UHURU MEDIA YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA NSSF
TIMU ya soka ya Uhuru Media juzi ilifuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la NSSF baada ya kuichapa Mlimani TV mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam.
Kutokana na ushindi huo, Uhuru Media sasa itakutana na mshindi wa mechi kati ya Jambo Leo na Global iliyochezwa jana kwenye uwanja huo.
Iliwachukua Uhuru dakika nne kuhesabu bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na Saidi Ambua kutokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Moni Lyambiko.
Bao la pili la Uhuru lilifungwa na Moni dakika ya 25 kwa mpira wa adhabu uliomponyoka kipa Aikael wa Mlimani TV aliyekuwa akijiandaa kuuweka kwenye himaya yake.
Uhuru ilipata pigo dakika ya 65 baada ya kipa wake, Ricardo Bigenda kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kudaka mpira nje ya eneo lake. Awali, Ricardo alionyeshwa kadi ya njano kwa kosa hilo.
Ilibidi Uhuru impuzishe kiungo wake, Nassoro Nassoro na kumwingiza kipa Emmanuel Koba, ambaye alishindwa kuzuia shuti la mpira wa adhabu lililopigwa na Singute wa Mlimani TV na kuwa bao la kwanza.
Bao hilo liliongeza kasi kwa Mlimani TV, ambayo iliwapumzisha wachezaji wake watano na kuingiza wengine kwa lengo la kuiongezea nguvu.
Hata hivyo, ukuta wa Uhuru uliokuwa chini ya Brendan, Moni, Haji Iddi na Abdalla Saidi ulikuwa imara kuokoa hatari zote zilizosababishwa na safu ya ushambuliaji ya Mlimani TV.
Katika mechi za netiboli, IPP ilitoa kipigo kikali cha mabao 33-4 dhidi ya Jambo Leo wakati Business Times iliikung'uta Changamoto bila huruma mabao 69-4.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mechi kati ya Mwananchi na Sahara zitakazomenyana kwenye uwanja wa Sigara wakati TSN itamenyana na Tumaini kwenye uwanja wa DUCE.
Katika netiboli, mabingwa watetezi Habari Zanzibar watamenyana na wenyeji NSSF katika mechi za kwanza za robo fainali wakati TBC itamenyana na Free Media.
BURIANI KILAMBO ATHUMANI
Marehemu Kilambo Athumani (katikati) akiwa na wachezaji wa zamani wa Pan African, Saad Matheo (kushoto) na Kitwana Manara. Kulia ni mmoja wa wanachama maarufu wa Pan African
Kilambo Athumani (wa pili kushoto waliosimama) akiwa na kikosi cha Yanga kilichokwenda Brazil miaka ya 1960. Hapa ni kwenye uwanja wa Macarana.MWANASOKA mkongwe wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Kilambo Athumani amefariki dunia.
Kilambo (75) alifariki dunia usiku wa Jumapili iliyopita nyumbani kwake Mwananyamala mjini Dar es Salaam na kuzikwa katika makaburi ya Kisutu.
Kocha huyo wa zamani wa Pan African, alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kansa ya koo.
Mazishi ya mwanasoka huyo mkongwe yalihudhuriwa na wanamichezo mbalimbali, wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete.
Kabla ya kifo chake, Kilambo aliwahi kujitokeza hadharani kupitia kwenye vyombo vya habari, akiomba apatiwe msaada wa fedha ili aweze kutibiwa ugonjwa huo.
Wapo waliosikiliza kilio chake na kumsaidia, lakini wengine kutokana na kutokuwa na uwezo, walishindwa kufanya hivyo.
Kilambo atakumbukwa na mashabiki wengi wa soka nchini waliowahi kumshuhudia akiichezea Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars miaka ya 1960 na 1970.
Alikuwa beki kisiki wa Yanga, aliyekuwa akicheza nafasi ya ulinzi wa pembeni kulia. Baadhi ya wachezaji aliocheza nao Yanga ni pamoja na Maulid Dilunga, Leonard Chitete, Omar Kapera, Hassan Gobosi, Muhidin Fadhili, Sunday Manara, Kitwana Manara, Abdulrahman Juma, Adamu Juma na Gibson Sembuli.
Marehemu Kilambo alizaliwa 1938 wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na kupate elimu ya msingi katika shule ya Mwamba. Hata hivyo, hakuweza kuendelea na masomo hayo na kujikuta akiishia darasa la pili kutokana na wazazi wake kukosa fedha za kumlipia karo.
Baada ya kukatishwa masomo, Kilambo aliamua kujishughulisha na uvuvi wa samaki. Kila asubuhi na jioni alijumuika na watoto wenzake kucheza kabumbu hadi 1956 alipojiunga na timu ya TANU Boys, iliyokuwa ikimilikiwa na vijana wa TANU wakati huo.
Akiwa katika timu hiyo, alichaguliwa katika kombaini ya wilaya ya Bagamoyo kati ya 1960 na 1962, ambayo ilishiriki katika michuano maalumu ya kuwania Kombe la Dosa, iliyokuwa ikifanyika mjini Morogoro kwa kuzishirikisha timu za wilaya za Mahenge, Kisarawe, Kilosa, Mafia na Bagamoyo.
Mwishoni mwa 1962, Kilambo aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75, aliamua kujiunga na kikosi cha pili cha Yanga, ambacho wakati huo kilikuwa kikijulikana kwa jina la African Boys, ambayo aliichezea kwa mwaka mmoja kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza.
Kutokana na uhodari wake wa kutandaza kabumbu, Kilambo aliweza kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga. Wakati huo alikuwa akicheza nafasi ya beki wa kati kabla ya kuhamia nafasi ya beki wa pembeni kulia.
Namba hiyo ndiyo aliyokuwa akiicheza wakati alipoitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Taifa Stars kabla ya kustaafu kuichezea timu hiyo 1973 kutokana na umri kuwa mkubwa.
Pamoja na kucheza mechi nyingi akiwa na Yanga, Kilambo alikuwa akiukumbuka zaidi mchezo kati yao na Asante Kotoko ya Ghana uliopigwa 1969, ambapo mshindi ilibidi apatikane kwa njia ya kura ya shilingi baada ya timu hizo kutoka sare mechi zote mbili.
Katika mechi ya kwanza kati ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, zilitoka sare ya bao 1-1. Ziliporudiana mjini Accra, timu hizo zilitoka tena sare hiyo ya mabao. Asante Kotoko iliibuka na ushindi huo wa kura ya shilingi.
Baada ya kustaafu kucheza soka, Kilambo alianza kazi ya kuzifundisha timu mbalimbali kama vile Yanga B na Nyota Afrika ya Morogoro, iliyoanzishwa baada ya kumeguka kwa Yanga. Baadaye, Nyota Afrika ilibadilishwa jina na kuitwa Pan African. Aliifundisha timu hiyo hadi 1983.
Kilambo ndiye aliyeiwezesha Pan African kupata mafanikio makubwa katika michuano ya ligi na kimataifa miaka ya 1980.
Ilipofika 1984, kocha huyo aliombwa kuifundisha Asante Tololo iliyokuwa na maskani yake mitaa ya Kariakoo, Dar es Salaam hadi 1988 alipoingia mkataba wa kuifundisha Nyota Nyekundu hadi iliposhuka daraja 1990.
Mwaka uliofuata, Kilambo aliifundisha Cargo iliyokuwa ikishiriki ligi daraja la tatu na kuipandisha hadi daraja la pili.
Marehemu Kilambo aliwahi kuhudhuria kozi mbili za ukocha. Alihudhuria kozi ya kwanza 1977 iliyoendeshwa na Hans Marischna kutoka Hungary kabla ya kuhudhuria kozi nyingine 1986 iliyoendeshwa na Trutman kutoka Ujerumani.
Akihojiwa na Burudani 1997, Kilambo alisema soka ya kulipwa nchini haitawezekana hadi hapo klabu ama taasisi zinazomiliki klabu za ligi kuu, zitakapokuwa na vitega uchumi vya kutosha.
Kilambo alisema ni vigumu jambo hilo kufanikiwa kutokana na klabu zenyewe kutokuwa tayari kufanikisha azma hiyo kwa kuwa nyingi zimetawaliwa na kasumba ya kutegemea misaada kutoka kwa mtu mmoja ama kikundi cha watu wachache.
Alikitaja kikwazo kingine katika kufanikisha azma hiyo kuwa ni klabu nyingi kutawaliwa na migogoro ya mara kwa mara kati ya uongozi na wanachama na hivyo kuchangia kudumaza maendeleo ya mchezo huo.
Marehemu Kilambo alisema mara nyingi migogoro hiyo ilikuwa ikichangiwa na viongozi na baadhi ya wanachama kujali zaidi maslahi yao binafsi badala ya kuendeleza klabu zao.
Akizungumzia kiwango cha soka nchini wakati huo, Kilambo alisema enzi zao walikuwa wakicheza soka ka moyo na kwa lengo la kujipatia umaarufu na kuziletea timu zao ushindi, tofauti na sasa, ambapo wachezaji wengi wameweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.
Alisema hali hiyo ndiyo iliyosababisha wachezaji kuhama kila mwaka kutoka timu moja hadi nyingine na kusababisha kiwango chao cha soka kushuka haraka na pia timu kutokuwa na mfumo unaoeleweka.
Kilambo alisema enzi zao ilikuwa vigumu kwa wachezaji kuhama holela kutokana na mapenzi waliyokuwa nayo kwa klabu zao na pia kuhofia kuonekana wasaliti.
"Tulichojali ni upenzi katika timu zetu, tofauti na ilivyo sasa, ambapo wachezaji wamekuwa wakiweka mbele maslahi yao binafsi kuliko mapenzi kwa timu wanazozichezea,"alisema.
Marehemu Kilambo pia alilalamikia tabia iliyokuwa imekithiri kwa viongozi na wachezaji kupanga matokeo ili waweze kujipatia chochote kwa lengo la kukabiliana na makali ya maisha.
Alisema kupanda na kushuka kwa kiwango cha soka nchini kutaonekana kwa wachezaji kuwa na maisha mazuri itakayowawezesha kucheza soka bila matatizo yoyote na pia kutokuwepo kwa migogoro katika klabu.
Mwanasoka huyo mkongwe pia alilalamikia uchezeshaji mbovu wa waamuzi katika ligi za nyumbani, ambao alisema husababisha timu za Tanzania kutolewa mapema katika michuano ya kimataifa.
Marehemu Kilambo ameacha watoto kadhaa. Watoto wake wawili, Ramadhani Kilambo na Athumani Kilambo waliwahi kuzichezea timu za Reli ya Morogoro, Yanga na Coastal Union ya Tanga.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pepa.
SIPENDI KUWA CHEMBEMBE-INI EDO
LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Ini Edo ameamua kuwapa ujumbe mashabiki wa fani hiyo wanaompenda na kumchukua.
Ini ameamua kutoa ujumbe huo, kufuatia shutuma nyingi zilizoelekezwa kwake kuhusu kuongezeka uzito kwa kiwango kikubwa.
Katika ujumbe huo, alioutoa kupitia akaunti yake ya twitter, Ini amesema kamwe hapendi kuwa mwembamba.
Mcheza filamu huyo, ambaye ni mzaliwa wa Jimbo la Akwa aliandika hivi: "Asanteni wapenzi wangu kwa kunipa moyo. Kwa wale wanaonichukia, kamwe sipendi kuwa mwembamba. Siku zote nitaendelea kuwa mwanamke wa kiafrika."
Mashabiki wanaomshutumu Ini kwa kuongezeka uzito wanadai kuwa, amepoteza uzuri na urembo wake.
Ini alifunga ndoa mwishoni mwa mwaka jana na Philip Ehiagwina, anayeishi na kufanyakazi nchini Marekani, ambaye amekuwa akimuelezea kuwa ni shujaa wake na kipenzi chake.
KIVAZI CHA GENEVIEVE CHAZUA GUMZO
LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Genevieve Nnaji mwishoni mwa wiki iliyopita alikuwa kivutio kikubwa wakati wa sherehe za utoaji wa tuzo za AMVCA zilizofanyika mjini hapa.
Sababu iliyomfanya Genevieve awe kivutio kwa watu waliohudhuria sherehe hiyo ni kivazi alichokuwa amevaa, ambacho kiliacha sehemu kubwa ya kifua chake kikiwa wazi.
Gauni hilo jeupe alilovaa mwanadada huyo lilisababisha sehemu ndogo ya matiti yake yote mawili kuonekana na hivyo kuwatoa udenda akina yakhe.
Baadhi ya mapaparazi waliohudhuria sherehe hiyo walipigana vikumbo, kila mmoja akitaka kupata picha nzuri za mcheza filamu huyo, ambaye muda wote huo alionekana akitabasamu.
Maziwa madogo ya mwanadada huyo na chuchu zilizosimama mithili ya msichana aliyevunja ungo, ndivyo vitu vilivyokuwa kivutio kutoka kwa mwanadada huyo.
Mbali na hayo, sura yake mwanana na umbile lenye mvuto ni baadhi ya vitu vingine vilivyomfanya awe kivutio cha aina yake wakati wa sherehe hiyo.
Baadhi ya mapaparazi walijaribu kumuuliza maswali mcheza filamu hiyo, lakini hakufunua mdomo wake kujibu chochote.
Hata hivyo, baada ya muda, Genevieve aliamua kubadili kivazi hicho na kuvaa kivazi kingine kirefu cha rangi nyekundu, iliyomeremeta ambacho kilimfanya azidi kupendeza.
2FACE: NITAMTOSHELEZA MKE WANGU KIMAPENZI
LAGOS, Nigeria
MWANAMUZIKI nyota wa Nigeria, 2Face Idibia ameahidi kumtosheleza mkewe, Annie Macaulay masuala yote yanayohusu unyumba.
2Face alitoa ahadi hiyo wakati wa ndoa ya kimila iliyofungwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika viwanja vya shule ya Apostolic vilivyopo Urua.
Ndoa hiyo ilifungwa mbele ya baadhi ya wanasiasa maarufu wa Nigeria, Godwill Akpabio (Gavana wa Jimbo la Akwa) na Florence Ita Giwa.
Wakati wa ndoa hiyo, 2Face aliulizwa maswali mbalimbali, ikiwa ni pamoja na iwapo ataweza kumtosheleza mkewe kitandani.
Huku akicheka na kuonyesha kulifurahia swali hilo, 2Face alijibu kwa kusema, ataweza kumtosheleza mkewe bila matatizo yoyote. Jibu hiyo lilisababisha kicheko kutoka kwa watu waliohudhuria sherehe hiyo.
Wakati huo huo, Gavana Akpabio ameamua kumzawadia 2Face Idibia na mkewe Annie Macaulay, gari jipya aina ya Prado SUV.
Gavana Akpabio alitoa zawadi hiyo wakati wa ndoa ya 2Face na Annie iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwanasiasa huyo pia aliahidi kupeleka ujumbe wa watu 30 mjini Dubai kwa ajili ya sherehe ya wanandoa hao inayotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
Subscribe to:
Posts (Atom)