KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 5, 2014

LUPITA NYONG'O, MWIGIZAJI NYOTA WA KENYA ALIYESHINDA TUZO YA OSCAR






 

LOS ANGELES, Marekani
ULIKUWA usiku wa aina yake kwa waigizaji na watayarishaji wa filamu ya 12 Years A Slave baada ya filamu hiyo kushinda tuzo ya picha bora ya mwaka katika tuzo za Oscar.

Aliyeonekana kuwa na furaha zaidi alikuwa Lupita Nyong'o, mcheza filamu chipukizi kutoka Kenya aliyeshinda tuzo ya mwigizaji bora msaidizi wa kike.

Mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo, Lupita alishindwa kuizuia furaha iliyojionyesha usoni mwake huku ukumbi mzima ukilipuka mayowe ya kumshangilia.

Sherehe za utoaji wa tuzo hizo zilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Jiji maarufu kwa utengenezaji wa filamu nchini Marekani la Hollywood.

Lupita alishinda tuzo hiyo, iliyokuwa na ushindani mkali kutokana na umahiri aliouonyesha katika kuicheza. Alicheza filamu hiyo kama mfanyakazi kwenye shamba la katani, ambaye alibakwa mara kadhaa na mmiliki wake.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Lupita alisema: " Haikwepeki katika mawazo yangu kwamba, hata dakika moja ya furaha katika maisha yangu ni shukrani na maumivu makubwa kwa mtu mwingine.''

Akaongeza: "Na iwe ukumbusho kwangu na kila mtoto kwamba kokote unakotoka, ndoto zako ni halisi.''

Lupita alimshukuru mwongozaji wa filamu hiyo, Steve McQueen kwa kumpatia nafasi ya kucheza filamu hiyo, ambayo imempatia sifa na umaarufu mkubwa duniani.

"Asante sana kwa kuniweka katika nafasi hii, imekuwa furaha kubwa katika maisha yangu,"alisema binti huyo mwembamba, mrefu na mwenye rangi yake ya asili ya kiafrika.

Lupita, ambaye alisherehekea kutimiza umri wa miaka 31 Jumamosi iliyopita, amewahi kucheza filamu nyingine kadhaa, lakini hii ilikuwa ya kwanza kwake kupata nafasi ya kuwa mshiriki msaidizi.

Mwigizaji Jennifer Lawrence, ambaye alikuwa akiwania tuzo hiyo na Lupita, aliwaeleza kwa siri rafiki zake kwamba, alitaka Lupita ashinde tuzo hiyo kwa sababu anastahili.

Tangu filamu hiyo ilipozinduliwa Agosti mwaka jana, Lupita amekuwa kivutio kwa waigizaji chipukizi na amekuwa akimshukuru Mungu kutokana na mafanikio aliyoyapata.

Msanii huyo alizaliwa Machi Mosi, 1983 katika mji wa Mexico nchini Mexico. Kwa sasa anaishi katika Jiji la New York nchini Marekani, lakini asili yake ni Kenya. Ni binti wa kabila la Luo la Kenya

Baba yake ni Peter Anyang' Nyong'o na mama yake ni Dorothy. Alisoma chuo cha Hampshire na baadaye shule ya Yale, inayofundisha sanaa za maonyesho. Kwa sasa kazi yake kubwa ni uigizaji, uongozaji wa filamu na video za muziki.

Lupita anajulikana zaidi kama Mmexico mwenye asili ya Kenya. Ni mtoto wa pili katika familia ya watoto sita. Baba yake ni waziri wa zamani wa huduma za afya wa Kenya. Wakati Lupita alipozaliwa, Peter alikuwa Mexico, akiwa mhadhiri wa sayansi ya siasa katika chuo cha El Colegio de Mexico. Familia yake ilikuwa ikiishi huko kwa miaka mitatu.

Nyong'o alirejea Kenya na wazazi wake akiwa na umri wa mwaka mmoja. Baba yake aliteuliwa kuwa Profesa katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Alisoma katika shule mbalimbali za Kenya na akiwa na umri wa miaka 16, wazazi wake walimrejesha Mexico kwa miezi saba ili kujifunza Kihispania.

Mwaka 2013, baba yake alichaguliwa kuwa seneta wa Kisumu. Kwa sasa, makazi ya Lupita ni Brooklyn. Ana uwezo mkubwa wa kuzungumza lugha za Kijaluo, Kiingereza, Kiswahili na Kihispania.

Lupita amemtaja msanii nyota wa maonyesho ya mavazi duniani, Alek kutoka Sudan ya Kusini, kuwa ndiye aliyemvutia kutokana na mafanikio yake na kumfanya ajitose katika fani hiyo.

"Wakati nilipomuona Alek, ni kama nilikiona kivuli changu, ambacho sikuweza kukikataa,"amesema Lupita, ambaye ana shahada ya uigizaji filamu na sanaa za maonyesho.

Wasanii wengine waliokuwa wakimvutia Lupita ni pamoja na mcheza filamu Whoopi Goldberg na Oprah Winfrey waliocheza filamu ya The Color Purple.

Filamu zake za mwanzo alizozicheza nchini Kenya akiwa na umri wa miaka 14 ni pamoja na
Romeo and Julie, On The Razzle na There Goes The Bride. Baadaye alicheza filamu ya East River, ambayo picha zake zilipigwa katika miji ya Brooklyn na New York.

Mwaka 2008 alicheza tamthilia ya Shuga iliyokuwa iliyotayarishwa na kituo cha televisheni cha MTV Base Africa kwa kushirikiana na UNICEF. Tamthilia hiyo ilikuwa ikizungumzia ugonjwa na kinga ya ukimwi.

Mwaka 2009 aliandika, kutayarisha na kuongoza kipindi maalumu cha televisheni kilichojulikana kwa jina la In My Genes, kilichokuwa kikizungumzia adha wanazopata walemavu wa ngozi (albino).

Lupita pia aliongoza video ya wimbo wa The Little Things You Do wa msanii Wahu, aliyemshirikisha Bobi Wine. Video hiyo ilishinda tuzo za MTV Africa mwaka 2009.

Picha za Lupita zimewahi kutumika kwenye majarida mbalimbali kama vile New York's Spring 2014 Fashion, Dazed & Confused.

No comments:

Post a Comment