KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 5, 2014

DEWJI AWAPA SOMO YANGA


ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa klabu ya Simba, Kassim Dewji, amewataka viongozi wa Yanga wawe makini na vituko na mbinu chafu watakazofanyiwa na wapinzani wao Al Ahly watakapokuwa Misri.

Dewji alisema hayo mjini Dar es Salaam juzi, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu uzoefu wake wakati Simba ilipokuwa ikicheza na timu za Misri katika michuano ya kimataifa.

Yanga inatarajiwa kurudiana na Al Ahly katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika itakayochezwa Jumapili kwenye uwanja wa jeshi wa mjini Cairo.

Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliichapa Al Ahly bao 1-0.

Ili isonge mbele katika michuano hiyo, Yanga inahitaji ushindi ama sare ya aina yoyote. Iwapo wapinzani wao watashinda bao 1-0, zitaongezwa dakika 30 na hali ikiendelea kuwa hivyo, mshindi ataamriwa kwa njia ya penalti tano tano

Dewji alisema kwa kawaida, Wamisri hutumia mbinu za ndani na nje ya uwanja kwa lengo la kuwahadaa na kuwavunja nguvu wapinzani wao kabla na wakati wa mchezo.

"Kama Yanga wapo tayari, waje nitawaeleza kila kitu, mambo mengine siwezi kuyasema katika vyombo vya habari. Lengo langu ni kutaka kuona Yanga wanashinda mechi hiyo,"alisema kiongozi huyo wa zamani wa Simba.

Dewji alisema Yanga itakuwa na bahati kwa kucheza mechi hiyo bila ya kuwepo kwa mashabiki uwanjani na iwapo wataitumia vyema fursa hiyo, uwezekano wa kusonga mbele ni mkubwa.

"Simba ina uzoefu mkubwa wa kucheza na waarabu, wanaweza kutaka kuwatembeza kwenye mapiramidi au sehemu za historia ili kuwatoa katika mchezo, wajisahau huku wao wakifanya vitu vingine kwa lengo la kusaka ushindi,"alisema.

Dewji alikuwa katibu mkuu wa Simba wakati ilipoitoa Zamalek kwa 'matuta' katika raundi ya tatu ya michuano ya klabu bingwa Afrika miaka ya 1990 na kufuzu kucheza hatua ya makundi.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Dar es Salaam, Simba ilishinda bao 1-0 na ziliporudiana mjini Cairo, Zamalek ilishinda idadi hiyo ya bao.

No comments:

Post a Comment