TIMU za soka za New Habari na Habari Zanzibar, zimepangwa kufungua dimba la michuano ya Kombe la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) mwaka huu.
Ratiba ya michuano hiyo inaonyesha kuwa, mechi hiyo itachezwa Machi 29 mwaka huu kwenye uwanja wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam.
Awali, mashindano hayo yanayozishirikisha timu za vyombo mbalimbali vya habari nchini, yalipangwa kuanza keshokutwa kwenye uwanja huo, lakini yamesogezwa mbele kwa wiki moja.
Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo, Rashid Zahor, alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, wameamua kuyazogeza mbele kutokana na maombi ya waandaaji, NSSF.
"Waandaaji wametuomba tuyasogeze mbele mashindano kwa wiki moja kwa sababu bado wanaendelea kukamilisha taratibu muhimu ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya michezo kwa timu zote 20,"alisema.
Kwa mujibu wa Zahor, mashindano ya mwaka huu yatazishirikisha timu 20 za soka na 18 za netiboli na kuongeza kuwa, kamati imeshapitisha usajili wa timu zote.
Alisema kikao cha kupitia usajili na kupanga ratiba ya mashindano hayo kilifanyika juzi kwenye ofisi za makao makuu ya NSSF zilizoko jengo la Benjamin Mkapa Towers, Dar es Salaam.
Zahor alisema ratiba kamili ya michuano hiyo inatarajiwa kutolewa kwa timu zote shiriki kabla ya keshokutwa.
Timu zingine zinazotarajiwa kushiriki kwenye mashindano hayo ni mabingwa watetezi Jambo Leo, Changamoto, TBC, IPP, Mwananchi, Tumaini Media, Uhuru SC, Business Times, Sahara Media, TSN na Mlimani TV.
Zingine ni Global Publishers, Free Media, Azam TV, Raia Mwema, Wizara ya Habari, Redio Maria na wenyeji NSSF.
No comments:
Post a Comment