KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 14, 2014

ISERE KUFUNGUA MADUKA YA VIFAA VYA MICHEZO MIKOANI


KAMPUNI ya Isere Sports imesema itaendelea kufungua maduka ya vifaa vya michezo katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kujenga mazingira ya kuwafanya vijana wapende kushiriki kwenye michezo.

Mkurugenzi wa Masoko wa Isere Sports, Abbas Isere, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, tayari ameshafungua duka lingine la vifaa hivyo katika mkoa wa Dodoma.

Isere alisema duka lake la kwanza lipo mtaa wa Mchikichi, Dar es Salaam, na limekuwa likiuza vifaa vya michezo ya aina mbalimbali.

Mbali na kuuza vifaa vya michezo, Isere alisema kampuni yake imekuwa ikitoa msaada wa vifaa hivyo kwa shule za msingi, sekondari na kwa timu zinazoshiriki katika ligi mbalimbali za soka nchini.

Alisema hivi karibuni alitoa msaada wa vifaa hivyo kwa shule ya sekondari ya Kerezange iliyoko Majohe mkoani Dar es Salaam na kwa timu ya Fresh Niga inayoshiriki michuano ya ligi daraja la tatu Kilwa Masoko mkoani Lindi.

"Lengo langu katika kutoa misaada ya aina hii ni kukuza vipaji vya vijana katika soka na kuwaendeleza katika mchezo huo,"alisema Isere.

Aliongeza kuwa mbali na michezo kutoa ajira, pia imekuwa ikiwasaidia vijana kuimarisha afya zao na kuwaepusha na vitendo viovu kama vile uvutaji dawa za kulevya, ulevi na uhuni.

Kwa mujibu wa Isere, maduka yake yanauza vifaa vya michezo mbalimbali, ikiwemo soka, netiboli, ngumi, riadha, mpira wa kikapu na mingineyo.

Alisema kwa sasa, soko lake kubwa ni fulana za michezo zenye nembo za klabu mbalimbali maarufu duniani, lakini anazouza zaidi ni za timu za Barcelona, Real Madrid, Manchester United, Chelsea na Liverpool.

"Vifaa vyangu vyote ninavyouza ni orijino na vya kiwango cha juu ndio sababu bei zake zipo juu kidogo. Siuzi vifaa feki. Nauza vifaa orijino kwa lengo la kuimarisha biashara yangu na ninaviuza kwa bei ya jumla na rejareja," alisema Isere.

Mkurugenzi huyo amesema pia kuwa, fulana za Simba na Yanga na zile zenye nembo na rangi ya Taifa Stars, ndizo zinazoongoza kwa mauzo, hasa timu hizo zinapofanya vizuri katika michuano ya ligi na kimataifa.

Ameongeza kuwa, amekuwa akiuza jezi kwa bei ya sh. 500,000 kwa seti moja na kuongeza kuwa, bei ya fulana ni kati ya sh. 20,000 na sh. 15,000 kwa kutegemea ubora wake.

No comments:

Post a Comment