'
Thursday, March 27, 2014
YANGA YAUA, AZAM YASONGA MBELE
MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga jana waliendelea kuitimulia vumbi Azam baada ya kuichapa Prisons mabao 5-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo mnono uliiwezesha Yanga kuendelea kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi 21 huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.
Azam, ambayo jana iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, bado inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 50 baada ya kucheza mechi 22.
Yanga ilihesabu bao la kwanza dakika ya 21 lililofungwa na Emmanuel Okwi kwa mpira wa adhabu ya moja kwa moja, ambao kipa Beno Kakolanya wa Prisons hakuweza kuuona.
Prisons ilipata nafasi nzuri ya kusawazisha dakika ya 43 baada ya beki Oscar Joshua wa Yanga kumwangusha Frank Hau ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani kuamuru ipigwe penalti. Hata hivyo, shuti la Lugano Mwangama lilitoka nje ya lango.
Dakika tano baadaye, Mrisho Ngasa aliiongezea Yanga bao la pili baada ya kuunganisha wavuni krosi maridhawa kutoka kwa Hussein Javu, aliyeingia kuchukua nafasi ya Jerry Tegete.
Katika dakika ya 44, lango la Prisons lilikuwa kwenye msukosuko mkali baada ya Yanga kufanya shambulizi zito, lakini shuti la Javu liligonga mwamba wa goli na mpira uliporudi uwanjani, uliokolewa na beki mmoja wa Prisons, ukamkuta Ngasa, ambaye shuti lake lilitolewa nje na kuwa kona.
Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Bao la tatu la Yanga lilifungwa na Hamisi Kiiza dakika ya 67 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Beno wa Prisons, aliyepangua kiki kali ya Simon Msuva ambaye aligongeana vizuri na Hassan Dilunga.
Beki Nadir Haroub 'Cannavaro' aliiongezea Yanga bao la nne dakika ya 78 kwa
njia ya penalti, iliyotokana na Javu kuangushwa ndani ya eneo la hatari. Kiiza alihitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la tano dakika ya 88 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Javu.
Katika kipindi hicho cha pili, Prisons ilionekana kuzidiwa kila idara na kushindwa kufanya mashambulizi kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza wakati Javu aliongeza kasi ya mashambulizi kwa Yanga na kushangiliwa na mashabiki kila alipogusa mpira.
Yanga: Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Jerry Tegete/Hussein Javu, Mrisho Ngasa/Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi/Hamisi Kiiza.
Prisons: Beno Kakolanya, Salum Kimenya, Laurian Mpalile, Lugano Mwagama, Nurdin Chona, Jumanne Fadhil, Godfrey Mageta, Fred Chudu, Peter Michael, Frank Hau/Bryson Mponzi na Ibrahim Mamba/ Six Mwakasega.
Mwandishi Wetu ameripoti kutoka Tanga kuwa, Azam iliendelea kujikita kileleni mwa ligi hiyo baada ya kuichapa Mgambo JKT bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Bao la kwanza la Azam lilifungwa na mshambuliaji John Bocco dakika ya 60 kabla ya Brian Umony kuongeza la pili dakika ya 82.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment