KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 5, 2014

TAIFA STARS YATOKA SARE NA NAMIBIA


TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania Taifa Stars imetoka sare ya kufungana bao 1-1 na Namibia katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki unaotambuliwa na Fifa uliochezwa Jumatano usiku kwenye uwanja wa Sam Nujoma nchini Namibia.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika,timu hizo zilikuwa bado hazijafungana na kocha Salum Madadi akafanya mabadiliko katika kipindi cha pili kwa kuwatoa Erasto Nyoni, Ramadhani Singano ‘Messi’ na juma Luizio na nafasi zao kuchukuliwa na Michael Aidan, Athanas Mdam na khamisi Mcha ‘Vialli’.

Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager ndio walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 86 baada ya kona iliyopigwa na Khamisi Mcha ‘Vialli’ aliyetokea benchi na kuingia moja kwa moja nyavuni bila kuguswa.

Namibia walisawazisha bao hilo katika dakika ya tano ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za kawaida, lililofungwa na Nekundi Haleluya Panduleni kwa adhabu.

Refa wa mechi hiyo aliingia lawamani kwa kuzidisha muda kupita kiasi, kwani mwamuzi wa mezani alionyesha dakika tano za nyongeza lakini muamuzi alichezesha dakika tano nyingine hivi kuwawezesha Namibia kupata bao.

Lakini katika hali ya kushangaza waamuzi toka nchini Zambia na msimamizi wa mechi toka nchini Afrika Kusini waliopangiwa kuchezesha mchezo huo hawakutokea, na badala yake shirikisho la soka Namibia NFA, wakaamuru mchezo huo uchezeshwe na waamuzi wa Namibia kwa makubaliano ya pande zote mbili.

Mwalimu Salum Madadi alisema licha ya kuwakosa wachezaji wengi nyota, kikosi hiki kilipigana hadi dakika ya mwisho na ameridhishwa na matokeo yaliyopatikana.

Wachezaji walioshindwa kujiunga na kikosi cha Stars ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Mwinyi Kazimoto ambao hawakuruhusiwa na vilabu vyao kutokana na kukosekana na usafiri wa kuwarudisha vilabuni kwa muda unaotakiwa.

Wengine walioshindwa kufika ni Edward Charles na Hassan Masapili ambao hati zao za kusafiri hazikuwa zimekamilika. Viwango

Matokeo haya huenda yakaiweka Stars kwenye nafasi nzuri ya viwango vya Fifa kwa kupata sare ugenini. IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY.

No comments:

Post a Comment