KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 26, 2014

SIJUTII KUWA NILIVYO-AKI



LAGOS, Nigeria
MARA nyingi watu wenye maumbo madogo na wafupi huwa wakikumbana na misukosuko mingi katika jamii, ikiwa ni pamoja na kutaniwa ama kudhihakiwa.

Lakini hali ni tofauti kwa mcheza filamu machachari wa Nigeria, Chinedu Ikedieze 'Aki', ambaye anaamini kuwa, umbile lake ni zawadi maalumu aliyobarikiwa na Mwenyezi Mungu ana anajivunia kuwa alivyo.

Akihojiwa na gazeti la YES la Nigeria hivi karibuni, Aki alisema anafurahia kupata tuzo za heshima kutokana na fani yake ya uigizaji, lakini hakuna faida yoyote kubwa anayoipata kutokana na tuzo hizo.

Aki alisema hakuna zawadi ya pesa ama nyingine yoyote kubwa anayoipata kama ilivyo kwa wasanii wanaoshinda tuzo hizo katika nchi za Ulaya Magharibi, lakini anafurahia kutambuliwa kwake na kuheshimiwa katika jamii.

"Ninaposafiri na kufika kwenye uwanja wa ndege, napata heshima maalumu na kutambuliwa. Mbali na hilo, hakuna kingine ninachokipata. Silipwi chochote, sipati faida yoyote.

"Sana sana napata heshima kama wanayoipata wanandugu wa ukoo wa kifalme wa Uingereza. Wao wanayo heshima wanayoipata katika jamii ya kimataifa na kutambulika, lakini vitu hivyo havipo hapa,"alisema msanii huyo, ambaye hivi karibuni alitunukiwa tuzo ya heshima ya MFR.

Alipoulizwa iwapo aliwahi kujishangaa kwa nini alizaliwa kama alivyo, mcheza filamu huyo alijibu: "Kwani mimi ndiye niliyejiumba? Kwa nini nijiulize swali kama hilo? Unaweza kujiuliza swali hilo iwapo utakuwa umechanganyikiwa kuhusu maisha ama umechoshwa na maisha."

"Lakini katika suala langu, sipo hivyo. Unapoamka asubuhi na kupata kitu fulani cha kula, unakuwa na watu wanaotabasamu kwa ajili yako na wewe kuwarejeshea tabasamu, unahitaji kitu gani kingine? Baadaye unakwenda kitandani, unalala na unapoumwa unakwenda hospitali, ni zawadi ipi nyingine muhimu kuliko hivyo?" Alihoji Aki.

Aki alisema kwa kadri anavyojitambua, umbo lake ni zawadi pekee aliyopewa na Mungu na kuongeza kuwa, wapo watu waliobarikiwa kuwa na pesa, magari, nyumba za fahari na kila wanachokihitaji, lakini ni wagonjwa.

"Hawazifurahii fedha walizonazo. Hivyo zawadi sahihi kwangu ni kuwa na afya nzuri,"alisisitiza mcheza filamu huyo machachari.

No comments:

Post a Comment