KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 5, 2014

KIIZA, OKWI KWENDA MISRI WAKITOKEA ZAMBIA


WASHAMBULIAJI nyota wa Uganda, Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza, wanatarajiwa kujiunga na kikosi cha Yanga nchini Misri leo wakitokea Ndola, Zambia, ambako walikwenda kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo.

Uganda jana ilitarajiwa kumenyana na Zambia katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyomo kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Okwi na Kiiza walikwenda Zambia mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuichezea Yanga katika mechi ya awali ya raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0. Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Jumapili mjini Cairo.

Awali, uongozi wa Yanga uliwasilisha maombi kwa Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA), kutaka wachezaji hao wabaki ili wajiandae kwa mchezo wao wa marudiano dhidi ya Al Ahly.

Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Uganda, Milutin Sredojevic ‘Micho’ aliwajumuisha wachezaji hao kwenye kikosi chake na kuahidi kuwa, wataondoka Zambia leo kwenda Misri baada ya mchezo huo.

Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuondoka nchini leo usiku kwenda Misri kikiwa na msafara wa watu 35, wakiwemo wachezaji na viongozi.

No comments:

Post a Comment