KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 5, 2014

YANGA, AL AHLY KURUDIANA UWANJA WA JESHI, YABEBA VYAKULA NA MAJI, KAVUMBAGU KUCHUKUA NAFASI YA KIIZA



WAKATI kikosi cha timu ya soka ya Yanga kimeondoka nchini kwenda Misri, mechi ya marudiano ya michuano ya klabu bingwa Afrika kati yao na Al Ahly itachezwa Jumapili kwenye uwanja wa jeshi mjini Cairo.

Kikosi cha Yanga kiliondoka jana saa tano usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri kikiwa na msafara wa watu 30, wakiwemo wachezaji 16.

Yanga imekwenda Misri ikiwa imefungasha vyakula na maji ya kunywa kwa hofu ya kuhujumiwa na wapinzani wao.

Habari kutoka Misri zimeeleza kuwa, pambano kati ya Yanga na Al Ahly, imeamriwa lichezwe kwenye uwanja wa jeshi ili kuepuka vurugu zinazoweza kufanywa na mashabiki wa soka wa Misri.

Tayari viongozi wawili wa Yanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa, Ahmed Seif 'Magari' na Ofisa Habari, Baraka Kazuguto, wameshawasili nchini Misri kwa ajili ya kuweka mambo sawa kabla ya pambano hilo.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam jana, Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alisema kikosi chao kinakwenda Misri kikiwa na wachezaji 16.

Mkwasa alisema wanatarajia kutua mjini Cairo leo asubuhi na kwenda moja kwa moja kwenye hoteli waliyotafutiwa na viongozi wao waliotangulia kufika nchini humo.

Awali, Yanga ilikataa kukaa kwenye hoteli ya Baron waliyopangiwa na wenyeji wao, iliyoko maeneo ya Uwanja wa Michezo wa Kimataifa wa Cairo kwa madai kuwa haina hadhi.

Mbali na kuikataa hoteli hiyo, Yanga pia imekataa kufanya mazoezi kwenye uwanja waliopangiwa na wenyeji wao ulioko kwenye mji wa Nasri kwa vile kiwango chake sio kizuri.

Kwa mujibu wa Mkwasa, wachezaji wanaotarajiwa kuwemo kwenye msafara huo ni Deo Munish
'Dida', Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro' na Kelvin Yondani.

Wengine ni Frank Domayo, Saimon Msuva, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngasa, Said Bahanuzi, Athuman Idd 'Chuji', David Luhende na Didier Kavumbagu.

Mkwasa alisema wachezaji Hamis Kiiza na Emmanuel Okwi, watajiunga na timu hiyo nchini Misri wakitokea Zambia, ambako jana walitarajiwa kuichezea timu yao ya taifa ya Uganda katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Zambia.

Akizungumzia mechi hiyo ya marudiano, Mkwasa alisema wamewaelekeza wachezaji wao kucheza kwa umakini mkubwa na kuepuka kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu uwanjani, ambavyo vinaweza kuigharimu timu yao.

Alizitaja hujuma wanazoweza kufanyiwa uwanjani kuwa ni pamoja na kuwapandisha hasira wachezaji kwa lengo la kumshinikiza mwamuzi awatoe nje baadhi yao kwa kadi nyekundu.

Mkwasa alisema pia kuwa, wamewatahadharisha wachezaji wao waepuke kucheza rafu katika eneo la hatari ili kukwepa wapinzani wao kupewa adhabu ya penalti.

"Zaidi ya hayo, tumewaelekeza wachezaji wetu kucheza kwa kushambulia tangu mwanzo na kuepuka kucheza mchezo wa kujihami ili tupate bao la mapema na kuwavunja nguvu wapinzani wetu,"alisema.

Kocha huyo alisema katika mechi hiyo, wamepanga kumwanzisha Kavumbagu tangu mwanzo wa mchezo ili aweze kushirikiana vyema na Okwi na Ngasa katika kutafuta mabao.

Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliichapa Al Ahly bao 1-0. Bao hilo la pekee lilifungwa na beki Cannavaro kipindi cha pili, akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Msuva.

Katika mechi hiyo, Kavumbagu aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Kiiza na kuongeza uhai mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji.

Wakati huo huo, uongozi wa Yanga umeamua kubeba vyakula na maji ya kunywa na kwenda navyo Misri ili kukwepa hujuma kutoka kwa wapinzani wao.

Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, timu hiyo itakwenda Misri ikiwa na mpishi maalumu, atakayekuwa akiwapikia chakula wachezaji nyumbani kwa balozi wa Tanzania nchini Misri.

No comments:

Post a Comment