KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 26, 2014

ZAWADI KOMBE LA NSSF ZAONGEZWA, BINGWA WA SOKA KUPATA MIL 4.5/- WA NETIBOLI MIL NNE

 Meneja Kiongozi wa Idara ya Uhusiano na Huduma za Wateja wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eunice Chiume (kushoto) akikabidhi jezi kwa mwakilishi wa Uhuru Media, Rashid Zahor, katika hafla iliyofanyika leo makao makuu ya shirika hilo mjini Dar es Salaam.
Meneja Kiongozi wa Idara ya Uhusiano na Huduma za Wateja wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eunice Chiume (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kutangaza zawadi za washindi wa mashindano ya Kombe la NSSF mwaka huu. Katikati ni Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo, Rashid Zahor na kulia ni katibu, Modest Msangi. (Picha zote na Emmanuel Ndege).

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limeamua kuongeza zawadi kwa washindi wa mwaka huu wa michuano ya soka na netiboli ya vyombo vya habari nchini.

Meneja Kiongozi wa Idara ya Uhusiano na Hudma za Wateja wa NSSF, Eunice Chiume, amesema mjini Dar es Salaam leo kuwa, bingwa wa soka atapata sh. milioni 4.5 wakati bingwa wa netiboli atazawadiwa sh. milioni nne.

Eunice alisema mshindi wa pili wa soka atazawadiwa sh. milioni 3.5 wakati mshindi wa tatu atapata sh. milioni mbili. Alisema katika netiboli, mshindi wa pili atapata sh. milioni 2.5 na wa tatu sh. milioni 1.5.

Zawadi zingine zitakazotolewa ni sh. 350,000 kwa wachezaji bora wa mashindano hayo kwa mpira wa miguu na netiboli.

Kwa mujibu wa Eunice, wameamua kuongeza zawadi kwa washindi kwa lengo la kuongeza ushindani kwa timu shiriki na pia kuyafanya mashindano hayo yawe na msisimko zaidi.

Alisema NSSF imepanga kutumia sh. milioni 19 kwa ajili ya zawadi kwa washindi wa michuano hiyo, ambayo imepangwa kuanza keshokutwa kwenye viwanja vya TCC na DUCE vilivyoko Chang'ombe, Dar es Salaam.

Katika mechi za ufunguzi, New Habari itamenyana na Habari Zanzibar katika soka wakati katika netiboli, Jambo Leo itamenyana na Wizara ya Habari na kufuatiwa na mchezo kati ya Azam na TSN. Michezo hiyo itaanza saa 1.30 asubuhi.

Eunice alisema mashindano hayo, yatakayozishirikisha timu 20 za soka na 18 za netiboli, yataendeshwa kwa njia ya mtoano na yatafikia kilele Aprili 12 mwaka huu. Alisema mgeni rasmi katika sherehe za ufunguzi anatarajiwa kuwa Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka.

Mashindano ya Kombe la NSSF yametimiza miaka 11 tangu yalipoanzishwa na mwaka huu yatakwenda sambamba na sherehe za miaka 50 ya shirika hilo na miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

"Michuano hii kwa mwaka huu, itafanyika katika sherehe hizo kubwa mbili na ndiyo yenye idadi kubwa ya timu kuliko miaka mingine tangu ilipoanzishwa 2004,"alisema Eunice.

Timu zitakazoshiriki katika mashindano ya mwaka huu ni IPP, Jambo Leo, BTL, New Habari, Mwananchi, Uhuru Media, Changamoto, Habari Zanzibar, Tumaini Media, Star TV na TBC.

Zingine ni TSN, Mlimani TV, Redio Maria, Wizara ya Habari, Global Publishers, Free Media, Raia Mwema na Azam TV.

No comments:

Post a Comment