KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 14, 2014

SIMBA YAIFAGILIA YANGA


UONGOZI wa klabu ya Simba, umeipongeza Yanga kwa kuonyesha kiwango cha juu cha soka katika mechi zake mbili za raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamekunwa na kiwango kilichoonyeshwa na watani wao katika mechi hizo na kuongeza kuwa, kutolewa kwao ni kwa bahati mbaya.

"Tunawapongeza sana Yanga kwa kucheza soka ya kiwango cha juu dhidi ya Al Ahly na sasa tunawakaribisha tena kwenye ligi kuu baada ya kutolewa,"alisema.

Yanga ilitolewa katika michuano hiyo baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 na Al Ahly katika mechi ya marudiano iliyochezwa mjini Alexandria. Mshindi ilibidi apatikane kwa njia ya penalti tano tano baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.

Katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Dar es Salaam, Yanga iliishinda Al Ahly bao 1-0 na ziliporudiana mjini Alexandria, Al Ahly nayo ilishinda idadi hiyo ya bao.

Wakati huo huo, Kamwaga amesema mkutano mkuu wa Simba, utakaojadili marekebisho ya katiba, utafanyika Jumapili kama ilivyopangwa.

Kamwaga amewataka wanachama wa klabu hiyo kulipia kadi zao ili waweze kuhudhuria mkutano huo na kuchangia mambo muhimu yanayoihusu Simba.

Alisema ajenda ya mkutano huo itakuwa ni marekebisho ya katiba na wanachama ndio wenye maamuzi ya mwisho.

Katika hatua nyingine, klabu ya Simba imewasilisha malalamiko kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutaka ufanyike uchunguzi kuhusu mapato yanayopatikana katika mechi za ligi kuu kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Kamwaga alisema jana kuwa, klabu yake imebaini kuna mchezo mchafu unaochezwa na wasimamizi wa uwanja huo ndio sababu mapato yanayopatikana yamekuwa kiduchu.

"Tumewaomba TFF washirikiane na polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi ili kubaini tatizo ni nini,"alisema.

Akitoa mfano, Kamwaga alisema mechi kati yao na Prisons iliyochezwa wiki iliyopita, iliingiza sh. milioni 33, lakini idadi ya mashabiki walioingia uwanjani ilikuwa kubwa kuliko kiwango hicho cha mapato.

Alisema mechi kati yao na Mbeya City iliingiza sh. milioni 143 wakati idadi ya mashabiki walioingia uwanjani ilikuwa sawa na ile ya mechi yao na Prisons.

Kamwaga alisema pia kuwa, wameandika barua TFF kupinga kukatwa sh. milioni 25 kutokana na uharibifu wa viti uliofanywa na mashabiki wao wakati wa mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi dhidi ya Kagera Sugar.

Alisema wanataka warejeshewe pesa hizo kwa sababu kuna kesi mahakamani iliyofunguliwa dhidi ya mashabiki wanaodaiwa kuhusika na uharibifu huo, hivyo Simba haikustahili kukatwa pesa hizo.

No comments:

Post a Comment