KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 5, 2014

ULIMBUKENI HUU WA KUNG'OA VITI UWANJA WA TAIFA HADI LINI?





SHIRIKISHO la Soka la Afrika (CAF), huenda likaufungia Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam, kufuatia vurugu zilizofanywa na mashabiki wakati wa mechi ya michuano ya klabu bingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly ya Misri.

Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wiki hii imeeleza kuwa, kufungiwa kwa uwanja huo kutatokana na ripoti itakayowasilishwa CAF na kamisaa wa mechi kati ya Yanga na Al Ahly iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika mechi hiyo iliyoshuhudiwa na mashabiki lukuki, Yanga ilijiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya kuichapa Al Ahly bao 1-0, ukiwa ni ushindi wake wa kwanza dhidi ya timu za Misri katika michuano ya kimataifa.

Kwa mujibu wa sheria za CAF, mashabiki wanapofanya vurugu uwanjani, uwanja hufungiwa kutumika kwa mechi za kimataifa ama timu husika hupewa adhabu ya kucheza mechi zake bila ya mashabiki.

Baadhi ya mashabiki wanaosadikiwa kuwa wa Simba, waliamua kung'oa viti kwenye jukwaa la orange na kuwarushia wenzao wa Yanga baada ya kutokea mabishano kati yao kuhusu sehemu ya kukaa mashabiki wa pande hizo mbili.

Chanzo cha vurugu hizo ni mashabiki wa Yanga kwenda kukaa kwenye jukwaa linalokaliwa na wenzao wa Simba kwa madai kuwa, mechi hiyo haikuwa yao. Kitendo hicho kiliwakera mashabiki wa Simba, ambao walianza kung'oa viti na kuwarushia.

Licha ya tukio hilo kushuhudiwa na polisi, baadhi yao wakishiriki kuwatuliza mashabiki hao na kuwanyang'anya viti hivyo kabla ya kuvirusha, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kwa wahusika. Hii maana yake ni kwamba tukio hilo kwa sasa limeshazoeleka na kuonekana la kawaida kwenye uwanja huo.

Hii si mara ya kwanza kwa mashabiki kung'oa viti kwenye uwanja huo. Iliwahi kutokea mwaka juzi wakati Yanga ilipocheza na Azam kwenye uwanja huo katika mechi ya ligi na kufungwa mabao 3-1 na wakati Simba ilipolazimishwa kutoka sare na Coastal Union mwanzoni mwa msimu huu.

Katika matukio yote hayo, TFF ilizitoza faini Simba na Yanga kutokana na mashabiki wake kufanya vurugu. Pia klabu hizo zilitozwa faini ili kufidia uharibifu wa mali uliotokea kutokana na vurugu hizo.

Licha ya kuchukuliwa kwa hatua hizo, bado tatizo hilo linaonekana kuwa sugu. Baadhi ya mashabiki wanaendeleza vitendo hivyo, ambavyo ni dhahiri kwamba ni vya kihuni na ulimbukeni na ambavyo havipaswi kufumbiwa macho.

Wakati sasa umefika kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo yenye mamlaka ya kusimamia uwanja huo, kushirikiana na TFF pamoja na Jeshi la Polisi kudhibiti vitendo hivyo na kuwachukulia hatua za kisheria mashabiki watakashiriki katika uovu huo.

Nimeviita vitendo hivyo kuwa ni vya kiovu kwa sababu mashabiki hawa wachache wasiokuwa na subira, ustahamilivu na moyo wa kiuanamichezo, wamekuwa wakifanya uharibifu huu bila woga na pengine kwa kuona kuwa hakuna wa kuwachukulia hatua yoyote.

Ieleweke kuwa serikali imetumia mabilioni ya pesa kujenga uwanja huo ili mashabiki wa soka nchini waweze kutazama mechi mbalimbali wakiwa wamekaa sehemu nzuri na bila ya kupata bughudha zozote. Lakini watu hawa wachache, tena wasiokuwa na akili timamu, wanataka kuturejesha kule tulikotoka enzi za 'Shamba la Bibi'.

Katika kudhihirisha kwamba baadhi ya Watanzania hawana ustaarabu, vyoo vyote vya uwanja huo kwa sasa vipo kwenye hali mbaya. Koki za maji ya bomba zimeng'olewa kila mahali na haieleweki ni lini na wakati gani waovu hawa wamekuwa wakifanya uharibifu huu.

Waswahili wana msemo unaosema : 'Usipoziba ufa, utajenga ukuta.' Iwapo serikali haitachukua hatua madhubuti kupambana na uovu huu, ipo siku Uwanja wa Taifa utageuka kuwa gofu na kupoteza ile hadhi ilionao hivi sasa na kuwa kivutio barani Afrika.

No comments:

Post a Comment