KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 27, 2014

OKWI AUZIMIA MUZIKI WA MBEYA CITY


Na Emmanuel Ndege
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Yanga, Emmanuel Okwi, amesema anakunwa na kiwango cha juu cha soka kinachoonyeshwa na timu ya Mbeya City katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Akizungumza na Burudani makao makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam juzi, Okwi alisema Mbeya City imeleta changamoto mpya katika ligi kuu msimu huu.

Okwi alisema timu hiyo yenye makao makuu yake mjini Mbeya, haijayumba kisoka tangu ligi kuu ilipoanza na wachezaji wake wanacheza kwa kujiamini na bila kukata tamaa.

"Iwapo wataendelea hivi msimu ujao, haitakuwa ajabu kwa Mbeya City kutwaa ubingwa,"alisema mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda.

Okwi amekiri kuwa, ligi ya msimu huu ni ngumu na yenye ushindani mkali na hakuna timu yenye uwezo wa kutangaza ubingwa mapema.

"Nimeichezea Simba kwa miaka zaidi ya miwili. Huko nyuma timu zilikuwa na uwezo wa kutangaza ubingwa zikiwa zimesalia mechi mbili au tatu, lakini msimu huu ni vigumu,"alisema Okwi.

"Yanga, Azam na Mbeya City kila moja ina uwezo wa kutwaa ubingwa, hali hii imesababisha kuwepo kwa ushindani mkali. Ni vigumu kutabiri bingwa mapema,"aliongeza.

Hata hivyo, Okwi alisema licha ya kuzidiwa kwa pointi na Azam, Yanga bado inayo nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo, iwapo wachezaji wake wataendelea kucheza kwa kujituma.

Alisema atahakikisha anasaidiana vyema na wachezaji wenzake kuiwakilisha vizuri timu hiyo ili itwae ubingwa na kupata nafasi nyingine ya kushiriki michuano ya klabu bingwa Afrika mwakani.

Akizungumzia jinamizi lililoikumba timu hiyo hivi karibuni la kupoteza penalti katika mechi muhimu, Okwi alisema, adhabu hiyo haina ufundi na kwamba mchezaji yeyote anaweza kupoteza.

"Penalti ni sawa na mchezo wa bahati nasibu, unaweza kupata au kukosa, hazina ufundi,"alisisitiza nyota huyo wa zamani wa Simba.

Wakati huo huo, klabu ya Yanga imesema, itakata rufani kwenye Mahakama ya Rufani Tanzania kupinga hukumu ya Makahama Kuu Divisheni ya Kazi ya kuitaka timu hiyo iwalipe wachezaji Wisdom Ndlovu na Stephen Marashi sh. milioni 106.

Katibu Mkuu wa Yanga, Ben Njovu, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamepokea nakala ya hukumu ya kesi hiyo iliyofungiwa na wachezaji hao ya kupinga kukatishiwa mikataba yao.

No comments:

Post a Comment