KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 14, 2014

VAN VICKER: SIJACHUKIZWA NA KAULI YA GENEVIEVE



 

VAN Vicker ni mmoja wa wacheza filamu waliojipatia sifa na umaarufu mkubwa barani Afrika kutokana na mwonekano wake wenye mvuto. Mcheza filamu huyo raia wa Ghana, ameoa na ni baba wa watoto watatu. Mkewe anaitwa Adjoa. Aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wacheza filamu wa Kinigeria, Genevieve Nnaji na Chika Ike. Katika makala hii ya ana kwa ana ya gazeti la Tribune la Nigeria, Van Vicker anaelezea kuhusu maisha yake ya usanii.

SWALI: Umekuwa maarufu kutokana na kucheza filamu za mapenzi. Umeupataje mwonekano mzuri ulionao?

JIBU: Sielewi. Siwezi kusema hasa iwapo ni kutoka kwa mama yangu au baba yangu. Naweza kusema ni mchanganyiko wa wote wawili kwa sababu, iwapo mama yangu angeolewa na mwanaume mwingine au baba yangu angeoa mwanamke mwingine, matokeo yangekuwa tofauti.

SWALI : Licha ya kuwepo kwa joto kali nchini Ghana kutokana na ukali wa jua, bado ngozi yako inaonekana kuwa mororo. Je, unatumia mafuta yoyote kuifanya ibaki ilivyo?

JIBU: Ni kweli nimekuwa nikitumia mafuta ya kutunza ngozi, si Ghana pekee, hata ninapokuwa Nigeria. Inategemea na mahali ninapokwenda kupiga picha za filamu. Lakini nakunywa maji mengi na kula mara kwa mara. Ni hivyo tu.

SWALI: Tumesikia uvumi mwingi kuhusu wewe. Unajisikiaje unaposikia uvumi kuhusu wewe binafsi?

JIBU: Mara nyingi huwa sijali uvumi wa aina yoyote kwa sababu naelewa ni mambo ya kutengenezwa. Baadhi ya wakati ninaposikia kujibu, huwa nafanya hivyo kupitia mitandao ya kijamii. Lakini watu hawawezi kuacha kuzungumza mambo ya uvumi, wataendelea kufanya hivyo.

SWALI: Unawezaje kumudu kuwa baba, mume na mwigizaji?

JIBU: Sidhani kama ni jambo kubwa sana. Ninaishi maisha ya kawaida. Nacheza nafasi mbalimbali kwenye filamu kama sehemu ya kazi yangu. Ninapokuwa nyumbani, nakuwa nyumbani na ninapokuwa kazi, sitaki mzaha. Nafanya mambo kama ambavyo baba wa kawaida angefanya. Mtu yeyote aliyeoa, anayefanyakazi na mwenye watoto, atakwenda nyumbani baada ya kazi na kuwa pamoja na familia yake. Hivyo ndivyo ninavyofanya. Hakuna cha ziada kuhusu hilo. Ninapokuwa nyumbani, nacheza na watoto wangu kila ninapopaswa kufanya hivyo.

SWALI: Lakini unapotoka nyumbani kwa siku kadhaa na kwenda kupiga picha za filamu, hauhisi tofauti yoyote? Unafanya nini kwa siku zote hizo unapokuwa mbali na familia yako?

JIBU: Kwa kawaida, kila ninaporudi nyumbani, najaribu kutumia muda mwingi kuwa pamoja nao. Huwa tunakwenda kutembea kwenye fukwe za bahari au kwenye bwawa la kuogelea, kutaza filamu ama kusafiri umbali mrefu au tunabaki nyimbani na kucheza michezo mbalimbali. Huwa najaribu kufanya vitu vingi kwa ajili yao.

SWALI: Ni waigizaji gani wa kike na kiume wanaokuvutia Nigeria?

JIBU: (Kicheko). Huwezi kunitega kwa kuniuliza swali hilo. Nafurahia kufanyakazi na waigizaji wenzangu wote.

SWALI: Kuna wakati Genevieve aliwahi kusema wewe si mwigizaji mzuri. Ulichukua hatua gani kuhusu kauli yake hiyo?

JIBU: Nilisoma habari hiyo, lakini haikukisumbua kichwa changu kwa sababu hayo yalikuwa maoni yake na ana uwezo wa kusema hivyo. Kamwe sikujibu kitu na sifikirii kufanya hivyo. Sina hisia mbaya kuhusu yeye.

Kwa sasa, iwe mtazamo wake umebadilika ama uko vilevile, hauwezi kuleta tofauti yoyote kwangu kwa sababu mimi ni mwigizaji babu kubwa na ninafanya kile ninachopaswa kukifanya. Nafurahia kazi yangu na ninafanya kilicho bora kadri ya uwezo wangu.

Japokuwa amesema hivyo, kama nitapewa kazi ya kufanya ikimuhusisha yeye (Genevieve), nitafanya kazi hiyo. Siwezi kusema kwa sababu alisema maneno hayo, siwezi kufanya kazi hiyo.

SWALI: Iwapo utapata nafasi ya kukutana naye, utamuuliza jambo hilo?

JIBU: Iwapo nitakutana naye kwenye shughuli yoyote au kucheza naye filamu, nitamuuliza, lakini siwezi kufanya hivyo kupitia kwenye vyombo vya habari. Baadhi ya vitu hivi, ambavyo watu wanaviandika kwenye magazeti au blogu si vya kweli. Inawezekana walibadili maneno yake.

Siku zote wamekuwa wakifanya hivyo kwangu, hivyo inawezekana wamefanya hivyo kwake. Lakini nitakapokutana naye ana kwa ana, nitamuuliza iwapo alisema maneno hayo. Na kama ni kweli, majadiliano yataendelea kati yetu juu ya kwa nini alisema hivyo na alisema maneno gani.

SWALI: Asili yako hasa ni wapi?

JIBU: Mimi ni mchanganyiko wa Kidachi, Kiliberia na Kighana.

SWALI: Ulikulia wapi?

JIBU: Nimelelewa na wanawake wawili katika maisha yangu, mama na dada yangu na siku zote tulikuwa tukihama kutoka sehemu moja hadi nyingine. Baba yangu alifariki nikiwa na umri wa miaka sita, hivyo sikuwahi kuwa na baba yangu muda wote. Mama yangu alinifundisha jinsi ya kuwa imara, kufanya vitu sahihi na alihakikisha nakuwa mtu mzuri, tofauti na watu wengi wanavyosema kwa mtu aliyechanganya uzao kama mimi.

SWALI: Watu wanasema nini kuhusu waliochanganya uzao (machotara)?

JIBU: Unaelewa wanavyosema, sihitaji kukueleza.

SWALI: Sielewi wanavyosema. Mimi pia ni chotara, nieleze?

JIBU: Ok, siku zote watu wanasema machotara ni watu wabaya?

SWALI: Wewe si mtu mbaya?

JIBU: Hapana.

SWALI: Ulifunga ndoa ukiwa bado kijana. Unamudu vipi kupambana na majaribu kutoka kwa rafiki zako wa karibu wa kike na washirika wako?

JIBU: Kama nilivyosema awali, ni mtazamo wa akili yangu na kufanya mambo kwa umakini. Najaribu kuwa makini kadri inavyowezekana na unaelewa baadhi ya wakati, unapaswa kucheza filamu za mapenzi na waigizaji wa kike na bado ukaendelea kuwa makini kwa sababu huo ndio uzuri wa kazi. Unaweza kuigiza mapenzi na watazamaji wakadhani upo kwenye mapenzi ya dhati na mwigizaji unayecheza naye, lakini wakati huo huo baada ya filamu kumalizika, hauwi tena na hisia kuhusu yeye.

SWALI: Umewahi kuvutiwa na mwigizaji yeyote wa kike mkiwa kwenye harakati za kucheza naye filamu?

JIBU: Haijawahi kutokea hivyo. Mwanamke pekee, ambaye nilisoma habari zake ni wakati walipoandika kwamba nimevunja ndoa ya Chika Ike. Sioni iwapo habari hiyo ilikuwa na maana yoyote, lakini walisema nilisababisha ndoa yake kuvunjika.

SWALI: Vipi kuhusu mashabiki wako wa kike? Wamekuwa wakikusumbua?

JIBU: Unamaanisha nini kwa kusema kunisumbua?

SWALI: Umekuwa ukipokea mara ngapi simu, barua pepe na meseji kupitia twitter kutoka kwa mashabiki wako wa kike?

JIBU: Siwezi kuita huo ni usumbufu. Ni watu wanaoifurahia kazi yangu na wanataka kunifahamu mimi binafsi. Ni kweli, napokea simu mara kwa mara, lakini najaribu kutenga muda. Siwezi kuwasiliana nao muda wote, hivyo baadhi ya wakati nawapuuza, wakati mwingine najaribu kujibu maswali yao.

No comments:

Post a Comment