WAKATI akifungua michuano ya soka na netiboli ya kuwania Kombe la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka alipatwa na mshtuko mkubwa alipokuwa akitambulishwa kwa waamuzi waliopangwa kuchezesha mechi za soka.
Alipatwa na mshtuko huo baada ya kuwaona waamuzi hao, ambao ni wanafunzi wa shule ya sekondari ya Jitegemee na pia kituo cha kuendeleza soka cha Kambi ya Twalipo iliyopo Chang’ombe, Dar es Salaam.
“Hivi hawa vijana wataweza kweli kuchezesha soka?” Waziri Gaudencia alimtupia swali Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau.
“Hawa vijana ni wazoefu sana, wamekuwa wakichezesha mechi za michuano ya Copa Coca Cola na Kombe la Uhai kila mwaka,” alijibu Dk. Dau huku akitabasamu.
Kauli hiyo ya Dk. Dau ilimfanya Waziri Kabaka awe na hamu kubwa ya kuwashuhudia kwa macho vijana hao wakichezesha soka. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani alitazama mechi hiyo kati ya TBC na Jambo Leo kuanzia mwanzo hadi mwisho.
“Hawa vijana (waamuzi) peke yao ni burudani, ni vijana wadogo sana, lakini wanaifahamu vyema kazi yao, napongeza uamuzi wa kuwapa vijana hawa mafunzo ya uchezeshaji soka tangu wakiwa wadogo,”alisema Waziri Kabaka baada ya mechi hiyo kumalizika huku akionekana kuwa na furaha kubwa.
Waziri Kabaka aliwamwagia sifa waamuzi hao kwa kuonyesha umahiri mkubwa katika uchezeshaji wa mchezo huo na kukipongeza kituo cha Twalipo kwa kutoa mafunzo kwa vijana hao.
Mbali na vijana hao kupewa mafunzo ya uamuzi na wakufunzi wa kituo hicho, pia wamekuwa wakipata mafunzo mbalimbali yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Hivi karibuni, vijana 15 wa kituo hicho walishiriki katika mafunzo ya kuchezesha soka yaliyotolewa na TFF kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kufaulu vizuri mitihani yao.
Mkufunzi mkuu wa kituo hicho, Stafu Sajenti Abel Kitundu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kwa sasa vijana hao wameshaanza kufanya mitihani ya uamuzi kwa ajili ya kupangiwa madaraja.
“Mwanzo vijana hawa hawakuwa wakifanya mitihani ya uamuzi, lakini walikuwa wakitumika kuchezesha mechi za michuano mbalimbali kama vile Copa Coca Cola na Kombe la Uhai,”alisema Kitundu.
“Lakini hivi sasa wameshaanza kufanya mitihani hiyo na wamekuwa wakifanya vizuri. Lengo ni kuwapandisha madaraja kama ilivyo taratibu kwa waamuzi wa soka,”aliongeza.
Kitundu alisema pia kuwa, wamepokea mwaliko kutoka nchini Burundi, ambako waamuzi hao watoto wanatakiwa kwenda kuchezesha mechi za michuano ya Kombe la Rollingstone inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Bujumbura.
Alisema waandaaji wa michuano hiyo wametaka wapelekewe waamuzi 12 kutoka kituo hicho kwa vile hawataki ichezeshwe na waamuzi wengine.
Je, ni nani aliyetoa wazo la kuanzishwa kwa mafunzo ya uamuzi kwa vijana hao?
Kwa mujibu wa Kitundu, wazo hilo lilitolewa na mwamuzi mstaafu, Kanali Issaro Chacha na Meja Bakari mwaka 2007. Alisema kwa kuanzia, walianza kutoa mafunzo ya kucheza soka kwa vijana wadogo.
Lakini baada ya kituo kuanza kukua na vijana wengi zaidi kujitokeza kupata mafunzo hayo, waliona ni vyema pia kuanzisha mafunzo ya kuchezesha soka kwa vijana wengine.
“Tulikuwa na vijana wengi, lakini tulipata tabu katika uchezeshaji wa mechi, tukaona ni vyema tutafute vijana kwa ajili ya kuwapa mafunzo ya kuchezesha soka ili wasaidie katika kazi hiyo,”alisema.
Kwa sasa, kituo hicho kinao wanafunzi 36, kati ya hao waamuzi 32 ni wa kiume na wanne wa kike. Alisema kituo hicho kinafadhiliwa na kuendeshwa na kambi ya Twalipo.
Kitundu alisema awali wanafunzi wa kituo hicho walikuwa wakitoka katika shule mbalimbali za sekondari za mjini Dar es Salaam, lakini baada ya kufanya mazungumzo na uongozi wa shule ya sekondari ya Jitegemee, waliamua kuwahamishia katika shule hiyo.
“Tuliona ili iwe rahisi kuwapata kwa wakati mmoja, ni vyema wasome karibu na mahali ilipo kambi yetu ndio sababu kwa sasa wote wanasoka sekondari ya Jitegemee,”alisema.
Ameushukuru uongozi wa TFF kwa kutoa kipaumbele kwa vijana hao kimafunzo na kuongeza kuwa, anaamini ipo siku watakuwa waamuzi bora hapa nchini na kimataifa.
Je, vijana hao wanafaidika vipi kutokana na malipo yanayotolewa kutokana na kuchezesha mechi za michuano mbalimbali?
Kwa mujibu wa Kitundu, vijana hao wamekuwa wakipatiwa sehemu kubwa ya mgawo wa fedha za malipo hayo, ambazo wamekuwa wakizitumia kulipia ada na mahitaji mengine ya shule.
“Tumekuwa na utaratibu wa kuingia mikataba na wanaosimamia na kuendesha michuano mbalimbali, hivyo sehemu ya malipo wanayotoa kwa ajili ya kazi ya uamuzi, tunawapatia vijana hawa,”alisema.
Kitundu ametoa mwito kwa vijana wenye mapenzi na kazi ya uamuzi wa soka, kujitokeza kujiunga na chuo hicho kwa vile mafunzo hayo yanatolewa bure kwa vijana wote, hakuna malipo.