KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 1, 2012

WEMA: Sitaki tena mpenzi sharobaro


MREMBO na msanii nyota wa kike wa Tanzania, Wema Sepetu sasa ameamua kuweka wazi kuwa, hatajihusisha tena kimapenzi na wanaume masharobaro.
Uamuzi huo wa Wema umekuja siku chache baada ya kupigwa kibuti na mpenzi wake wa muda mrefu, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Naasib Abdul ‘Diamond’.
Diamond alitangaza kumpiga kibuti Wema wiki iliyopita baada ya kumfumania akiwa na rafiki yake kwenye hoteli moja mjini Dar es Salaam.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Wema alisema alichobaini ni kwamba, wanaume masharobaro hawana mapenzi ya dhati kwa vile malengo yao ni kuchezeana.
Wema amemwelezea Diamond kuwa ni mmoja wa masharobaro anaowazungumzia na kuongeza kuwa, isingekuwa tabia yake hiyo, huenda mapenzi yao yangedumu kwa muda mrefu.
Wema, mrembo wa Tanzania wa mwaka 2006 amesema, kwa sasa anahitaji kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume anayemzidi umri kwa vile anaamini watu hao wanakuwa na mapenzi ya dhati.
Mbali ya kuwa na mapenzi ya dhati, Wema alisema wanaume wenye umri mkubwa hawana wivu kama masharobaro, ambao muda wote hupenda kuwa karibu na wapenzi wao badala ya kufanyakazi.
“Kila kitu kina mwisho wake. Mapenzi yangu mimi na Diamond yangeweza kudumu, lakini usharobaro alionao ndiyo uliosababisha yote yaliyotokea, “alisema Wema.
“Na ndiyo maana nasema kwamba, ni bora uwe na mpenzi aliyekuzidi umri, mnaweza kufika mbali, lakini hawa masharobaro hakuna kitu kabisa,” aliongeza.
Hata hivyo, Wema alisema ni afadhali aamue kufunga ndoa na mwanaume atakayempata kuliko kuendelea na kadhia inayompata hivi sasa.
Alisema amedhamiria kwa dhati kutafuta mwanaume anayejua mapenzi kuliko kuwa na uhusiano na wanaume wenye umri mdogo, ambao amedai hawajui maana ya mapenzi na kuyathamini na pia hawana mwelekeo wa maisha.
Wema, ambaye kwa sasa anatamba katika fani ya filamu Bongo, amekuwa akijihusisha kimapenzi na wasanii wa fani mbalimbali, lakini hakuna aliyeweza kudumu naye muda mrefu.
Awali, binti huyo aliyejaliwa kuwa na sura na umbo lenye mvuto, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mcheza filamu, Steven Kanumba, lakini wakapigana kibuti baada ya muda si mrefu.
Mbaya zaidi, Kanumba alimfungulia Wema kesi ya madai katika mahakama ya hakimu mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam, akimtuhumu kuvunja kioo cha gari lake.
Hata hivyo, kesi hiyo ilifutwa baada ya pande hizo mbili kufikia makubaliano ya kulimaliza suala hilo nje ya mahakama. Tayari Wema ameshalala rumande zaidi ya mara mbili.
Baadaye Wema alijitosa kimapenzi kwa mwanamuziki Chalz Baba, aliyekuwa bendi ya Twanga Pepeta International na sasa yupo Mashujaa, lakini penzi hilo nalo halikudumu.
Ndipo mwanadada huyo akajitoma kimapenzi kwa Diamond, ikiwa ni pamoja na kuvishwa pete ya uchumba na kwenda kuvinjari naye nchini Afrika Kusini, lakini penzi hilo nalo limepukutika.
Je, tatizo lipo kwa wanaume, ambao Wema ameamua kuwaita masharobaro wa mapenzi ama ni yeye ndiye mwenye gundu?
Kazi kwenu wasomaji kujiuliza na kupata majibu.

No comments:

Post a Comment