KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 17, 2012

Simba, Yanga zaingia vitani kesho

Felix Sunzu

Emmanuel Okwi

Hamisi Kiiza



Haruna Niyonzima


Msimbazi waahidi mamilioni kwa wachezaji

Nurdin, Taita, Telela wamtesa Kocha Papic

Kuiona Zamalek sh. 50,000 na sh. 3,000

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya klabu za Afrika, Simba na Yanga mwishoni mwa wiki hii wanaanza kampeni zao kwa kumenyana na timu za Zamalek ya Misri na Kiyovu ya Rwanda.
Wakati Yanga itavaana na Zamalek katika mechi ya michuano ya klabu bingwa Afrika itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba watakuwa wageni wa Kiyovu katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa siku hiyo kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali.
Mechi zote mbili zinatarajiwa kuwa ngumu kwa vile Zamalek na Kiyovu ni timu nzuri, hivyo Simba na Yanga zitalazimika kufanyakazi ya ziada ili ziweze kuibuka na ushindi.
Simba inatarajiwa kuondoka nchini leo kwenda Rwanda ikiwa na msafara wa watu 40, wakiwemo wachezaji 18 na viongozi watano wakati Zamalek inawasili nchini kesho kwa ajili ya mechi yake na Yanga.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana kuwa, maandalizi yote kwa ajili ya safari hiyo yamekamilika na kwamba msafara huo utaondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda.
Kamwaga alisema Simba itakwenda Rwanda bila ya wachezaji wake wawili nyota, Haruna Moshi ‘Boban’ na Felix Sunzu kutokana na kuwa majeruhi. Alisema Sunzu anasumbuliwa na maumivu ya kichwa wakati Boban anasumbuliwa na nyama za paja.
Hata hivyo, Kamwaga alisema kikosi chao kipo imara na mapengo ya Boban na Sunzu hayawezi kuwaathiri katika mchezo huo kwa sababu wachezaji wengine wote wapo fiti.
Naye Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema wamepanga kuwazawadia wachezaji wa timu hiyo mamilioni ya pesa iwapo wataishinda Kiyovu na kusonga mbele katika michuano hiyo.
Rage alisema wametoa ahadi hiyo kwa wachezaji kwa lengo la kuwaongezea morari na kuwafanya wacheze kwa kujituma.
Wiki iliyopita, Simba iliwazawadia wachezaji wake sh. milioni 12 baada ya kuifunga Azam mabao 2-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Japokuwa Rage hakutaka kuweka wazi kiasi cha pesa watakachowazawadia wachezaji wao, kuna habari kuwa tayari baadhi ya matajiri wa Simba wameshachangia zaidi ya sh. milioni 25.
Rage alisema vijana wake wapo imara na wamejipanga vizuri kwa ajili ya vita yao dhidi ya Kiyovu. Alisisitiza kuwa, ushindi dhidi ya Wanyarwanda ni lazima.
Kwa upande wa Yanga, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa alisema maandalizi yote kwa ajili ya mechi hiyo yamekamilika.
Mwesigwa alisema Zamalek imepangiwa kukaa kwenye hoteli ya Hyant, lakini inaweza kuhamia hoteli nyingine kwa kuongeza malipo iwapo itaamua kufanya hivyo.
Kwa kawaida, timu za Misri hupenda kukaa hoteli ya Serena (zamani Movenpick) ama New Africa kila zinapokuja nchini kucheza mechi za kimataifa.
Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic alisema juzi kuwa, bado ana wasiwasi kuhusu hali za wachezaji, Nurdin Bakari, Godfrey Taita na Salum Telela, ambao ni majeruhi.
Papic amesema kuumia kwa wachezaji hao ni pigo kubwa kwa Yanga kwa sababu kila mmoja ana mchango wake katika timu.
Kwa mujibu wa Papic, Taita na Telela wameumia mguu na watakuwa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa wakati Nurdin amefunguliwa plasta ngumu (POP) baada ya kuumia kidole.
Hata hivyo, kocha huyo kutoka Serbia alisema kikosi chake kipo imara na kwamba atawatumia wachezaji wengine waliopo kwa ajili ya kuziba mapengo yao.
Wakati huo huo, kiingilio cha juu katika mechi kati ya Yanga na Zamalek kitakuwa sh. 50,000 kwa VIP A na sh. 30,000 kwa VIP B.
Viingilio vingine ni VIP C sh. 15,000, viti vya machungwa sh. 7,000, viti vya bluu sh. 5,000 na viti vya kijani sh. 3,000.

No comments:

Post a Comment