KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 1, 2012

Sina matatizo na TID-Dimpoz


MSANII anayechipukia katika fani ya muziki wa kizazi kipya nchini, Ommy Dimpoz amesema hana matatizo na kiongozi wa bendi ya Top, Khaleed Mohammed ‘TID’.
Dimpoz amesema, alipoamua kurekodi wimbo wake wa Nai Nai, alipata baraka zote kutoka kwa TID na si kweli kwamba alimzunguka.
Amesema siku zote msanii anapofanyakazi nzuri, ni kawaida ya watu kuzusha maneno mengi, lakini ukweli unabaki palepale kwamba bado yeye ni mwanamuziki wa bendi ya TOP.
Dimpoz ni mmoja wa wanamuziki wanaounda bendi hiyo, inayoongozwa na kumilikiwa na TID, akiwa ameshiriki nayo kurekodi nyimbo mbalimbali.
Hivi karibuni, msanii huyo aliibuka na kibao chake kipya cha Nai Nai, alichokirekodi kwa kushirikiana na Ali Kiba na kumpa sifa na umaarufu mkubwa.
Kibao hicho kimekuwa kikishika chati za juu katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini na kumfanya msanii huyo apate umaarufu katika kipindi kifupi.
“Nilipoamua kurekodi wimbo huu nje ya bendi yangu, TID alikuwa anafahamu. Lakini ni kawaida mtu anapofanya kazi nzuri, huwa yanasemwa maneno mengi,”alisema.
Kwa mujibu wa Dimpoz, anazo nyimbo nyingi za kwake binafsi na ataendelea kuzirekodi kila atakapopata nafasi kwa vile lengo lake ni kukamilisha albamu.
Alisema tayari ameshapata ofa ya kurekodi nyimbo zake sehemu nyingi na kuongeza kuwa, atakachokifanya ni kurekodi nyimbo moja baada ya nyingine.
“Sijarekodi wimbo huu kwa kubipu kama wanavyofanya wengine, ambapo wimbo wa kwanza unakuwa mkali, zinazofuata mbovu. Nyimbo zangu zote ni mawe,”alisema msanii huyo.
Dimpoz alijigamba kuwa, hata video ya wimbo huo ni kali na inapendwa na mashabiki wengi kwa sababu wote alioshirikiana nao ni wakali na waliifanya kazi hiyo kwa muda uliopangwa.

No comments:

Post a Comment