KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 16, 2012

Mwanamuziki wa Nigeria afunika tamasha la Busara


MWIMBAJI nguli wa muziki wa Nigeria, Nneka Egbuna mwishoni mwa wiki iliyopita alifanya shoo ya aina yake na ya kihistoria katika tamasha la tisa la Sauti za Busara.
Tamasha hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa Ngome Kongwe mjini hapa, lilihudhuriwa na mashabiki lukuki, ambao walivutiwa na muziki wa mwanadada huyo.
Kabla ya kutinga kwenye tamasha hilo, Nneka alifanya maonyesho katika nchi za Kenya, Rwanda na Uganda.
Katika onyesho la juzi, Nneka aliimba nyimbo kadhaa kutoka katika albamu yake mpya, aliyoiachia mwaka jana, iitwayo ‘ Soul is Heavy’.
Baadhi ya nyimbo hizo zilikuwa zikizungumzia mapenzi, machungu na alizipiga katika mahadhi ya reggae, hio hop, R&B na vintage soul.
Mwanadada huyo alikuwa akiimba huku akisaidiwa na Garry Sullivan kutoka Marekani (drums), Emmanuel Ngolle Pohossi kutoka Cameroon (besi), Jonas ‘Mo’ Da Silva Pinheiro kutoka Brazil (gita) na Nis Goetting kutoka Ujerumani (kinanda).
Akizungumza wakati wa onyesho hilo, Nneka alisema rushwa ni ugonjwa wa kijamii, ambao ulikuwa ukipigwa vita na marehemu Fela Anikulapo Kuti wa Nigeria. Alisema rushwa ina athari kubwa kwa bara la Afrika na kutolea mfano wa jimbo la Niger Delta, alikozaliwa na kukulia.
Mara baada ya kumaliza kupiga nyimbo zake, mashabiki waliohudhuria tamasha hilo hawakutaka ashuke jukwaani. Waliomba aendelee kuwaburudisha. Uimbaji wake na ujumbe alioubeba umedhihirisha kuwa muziki unatumia lugha, ambayo inaweza kufikisha ujumbe kirahisi zaidi.
Mwanamuziki huyo alirekodi albamu yake ya kwanza mwaka 2005 inayokwenda kwa jina la ‘Victim of truth’ na kufuatiwa na No Longer At Easy aliyoitoka mwaka 2008.
Tamasha hilo la tisa lilipambwa kwa burudani kutoka kwa wanamuziki mbalimbali maarufu kutoka nchi za Afrika na vikundi vya muziki tofauti vya Tanzania.
Wanamuziki kutoka nje waliopamba tamasha hilo ni Hanitra kutoka Madagascar, kikundi cha Camirata kutoka Sudan, Fredy Massamba kutoka Congo, Super Mazembe kutoka Kenya na Ogoya Nengo kutoka Japan.
Kikundi cha Mashauzi Classic kinachoongozwa na Isha Ramadhani nacho kilikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki kutokana na nyimbo zake maridhawa kama vile Mama nipe radhi na Tugawane ustaarabu.

No comments:

Post a Comment