KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 3, 2012

Mwamuzi mkongwe Gratian Matovu afariki dunia


MWAMUZI na kamisaa wa kimataifa wa zamani wa soka wa Tanzania, Gratian Matovu amefariki dunia.
Matovu (85) alifariki dunia jana saa sita mchana nyumbani kwake Mbezi Beach (Makonde), Dar es Salaam.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, mtoto wa marehemu, Stephen Matovu alisema baba yake alifariki kwa ugonjwa wa kiharusi.
Stephen alisema marehemu Matovu alipatwa na ugonjwa huo kwa nyakati mbili tofauti kabla ya kumkuta tena kwa mara ya tatu na kusababisha mauti yake.
Kwa mujibu wa Stephen, taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwa marehemu na leo wanatarajia kutoa taarifa kuhusu siku na mahali yatakapofanyika mazishi yake.
Matovu ni mmoja wa waamuzi waliojipatia sifa nyingi nchini miaka ya 1960 hadi 1970, akiwa na waamuzi wenzake marehemu Manyoto Ndimbo na marehemu Mohamed Nyama.
Alianza kuchezesha soka nchini mwaka 1964 hadi mwishoni mwa miaka ya 1970 alipoamua kustafu na kuanza kazi ya ukufunzi wa waamuzi na ukamisaa wa mechi za ligi na kimataifa.
Marehemu Matovu alikuwa mmoja wa waamuzi na makamisaa waliokuwa wakitambuliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, marehemu Matovu aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT- sasa TFF), katibu wake akiwa, Leodeger Tenga.
Kabla ya kuanza kuugua, marehemu Matovu alikuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya waamuzi ya TFF. Pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa chama cha waamuzi nchini (FRAT).
Marehemu Matovu, ambaye ni mzaliwa wa wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, alipata cheti cha uamuzi wa soka kwa mara ya kwanza mwaka 1956 na kupewa uamuzi wa daraja la kwanza mwaka 1961. Miaka mitatu baadaye, alipata beji ya FIFA.
Marehemu Matovu ameacha watoto 11 na wajukuu, ambao idadi yao haikuweza kufahamika mara moja.

No comments:

Post a Comment