KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 16, 2012

Sizitaki tuzo zenu-Dully Sykes


MSANII machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Dully Sykes amewataka waandaaji wa tuzo za muziki wa Kilimanjaro, waondoe jina lake kwenye orodha ya washindani wa tuzo za mwaka 2011.
Dully alisema mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, alishatangaza kujitoa kwenye tuzo hizo tangu mwaka juzi hivyo anashangaa kuona waandaaji wameendelea kuorodhesha jina lake.
“Nilishawaambia, sitaki kuwemo tena katika tuzo zao, lakini nashangaa kuona wanaendelea kuniweka tu. Kwani wananiona mimi ndio msanii pekee?” Alihoji msanii huyo.
“Wakati ule wa hits kama nyambizi na zinginezo mbona hawakunipa tuzo? Au walidhani mimi ni msanii, ambaye ningeishia kati tu,” aliendelea kulalamika msanii huyo.
Alisema uamuzi wa waandaaji wa tuzo hizo kuendelea kumshirikisha kuziwania, umetokana na kubaini ukweli kwamba yeye bado ni mkali katika fani.
“Nimeshasema sitaki, sizitaji tuzo zenu,” alisisitiza msanii huyo, ambaye amewahi kutamba na vibao kadhaa kama vile Shekide.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo wa Dully, mratibu wa tuzo hizo kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Angelo Ruhala alisema hawana taarifa.
“Kama msanii ameamua kujitoa, basi aandike barua BASATA ya kujitoa, sio kuzungumza kwa maneno mitaani,”alisema.

No comments:

Post a Comment