KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 23, 2012

Stars, DRC kazi ipo leo



KIKOSI cha timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, leo kinashuka dimbani kumenyana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ni wa kujipima nguvu kwa timu zote mbili kabla ya kucheza mechi za michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Katika michuano hiyo, Taifa Stars imepangwa kumenyana na Msumbiji katika mechi itakayopigwa Februari 29 mwaka huu mjini Dar es Salaam wakati Congo itavaana na Shelisheli.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen na Kocha Msaidizi wa DRC, Mutubile Santos kila mmoja alitamba kuwa timu yake itaibuka na ushindi.
Poulsen alisema timu yake imejiandaa vyema kuikabili Congo na kuongeza kuwa, mchezo huo ni muhimu kwa kikosi chake kinachojiandaa kuvaana na Msumbiji.
Kocha huyo kutoka Denmark alisema, anatarajia mchezo huo utakuwa kipimo muhimu kwa timu yake kabla ya kuivaa Msumbiji na kuongeza kuwa, utamsaidia kubaini mapungufu ya timu yake.
Poulsen alisema ujio wa mchezaji Ali Badru anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Canal Suez ya Misri, utachangia kuongeza nguvu kwenye timu yake. Mchezaji huyo anatarajiwa kuwasili nchini leo asubuhi.
Katika mchezo huo, Taifa Stars itawategemea zaidi wachezaji wake wazoefu kama vile Shadrack Nsajigwa, Juma Nyoso, Abdi Kassim, Mrisho Ngassa na Stephano Mwasika.
Wachezaji wengine wanaounda timu hiyo ni Juma Kaseja, Shaaban Kado, Mwadini Ali, Nassor Said, Aggrey Morris, Kevin Yondan, Jonas Gerald, Shaban Nditi, Shomari Kapombe, Salum Aboubakar, Mwinyi Kazimoto, Juma Javu, John Bocco, Uhuru Selemani na Nsa Job.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Congo, Santos, alisema timu yake imejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo na kuongeza kuwa, wanatarajia utakuwa kipimo tosha kabla ya kuivaa Shelisheli.
Santos alisema wanaiheshimu Taifa Stars kuwa ni timu nzuri ndiyo sababu wamekubali kupambana nayo kwa lengo la kupima uwezo wa timu yake.

No comments:

Post a Comment