KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 23, 2012

Upendo Kilahiro kufanya makubwa tamasha la Pasaka



MWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili mwenye sauti nyororo, Upendo Kilahiro amekuwa wa kwanza kuthibitisha kushiriki katika tamasha la Pasaka litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions, alisema mjini Dar es Salaam kuwa, Upendo amemthibitishia kwamba atashiriki tamasha hilo.

"Kilahiro tutakuwa naye kwenye tamasha na naamini kwamba mwaka huu tamasha hili litakuwa bora zaidi kutokana na kushirikisha waimbaji wengi wakali," alisema Msama.

Kwa mujibu wa Msama, tamasha hilo la aina yake, baada ya kufanyika Dar es Salaam, pia litarindima kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9.

Tamasha la mwaka huu malengo yake makubwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji wanawake wajane.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi kadhaa za Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia.

Akizungumza mjini Dar es Salaam, Upendo alisema amepania kufanya mambo makubwa katika tamasha la mwaka huu na atapanda jukwaani kuimba 'live' na bendi yake ya Upendo Kilahiro. "Natoa mwito kwa mashabiki wangu wasiwe na wasiwasi, watarajie kupata vitu vizuri na tofauti zaidi... watapata vitu vinono kwa vile tamasha hili linazidi kuwa bora zaidi. "

"Sikukuu ya Pasaka ni upatanisho kutokana na kifo cha Yesu Kristo aliyefia msalabani na kufufuka siku ya tatu... tutaienzi sikukuu hiyo kwa nderemo," alisema Upendo.

Mwanamuziki huyo anayeabudu katika Kanisa la BCIC lililoko Mbezi Beach, Dar es Salaam (Kwa Askofu Gamanywa), alisema amejiandaa vyema kukonga nyoyo za mashabiki wake na mbali na kufanya mazoezi, pia atafunga na kusali ili Mungu amfanyie miujiza.

Aliwaomba mashabiki wamiminike kwa wingi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 8 na Jamhuri Aprili 9 ili kuona mambo mazuri aliyowaandalia na kuongeza kuwa, kwa vile anamtukuza Mungu aliyemtoa kwenye shida na majaribu mengi ya Shetani, anaamini atawapa kile wanachotaka kutoka kwakwe.

Alisema anatarajia kuimba nyimbo mbalimbali zikiwemo zilizotamba za Zindonga (alioimba kwa Kizulu), Unajibu Maombi na Ni Salama Rohoni. Upendo hivi sasa anatamba na albamu yake mpya ya Ficho Langu aliyoirekodi nchini Canada.

No comments:

Post a Comment