KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 17, 2012

AFC yashuka daraja



Timu ya AFC ya Arusha imeshindwa kutokea kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya 94 KJ iliyokuwa ichezwe jana (Februari 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 21 ya FDL timu yoyote inayoshindwa kufika kituoni na kusababisha mchezo husika kutochezwa itashushwa daraja hadi Ligi ya Taifa na matokeo ya michezo yake yote itafutwa ili kutoa uwiano sahihi kwa timu zilizobaki kwenye mashindano.

Si Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), msimamizi wa ligi hiyo Kituo cha Pwani wala Kamishna wa mechi hiyo Ramadhan Mahano waliokuwa na taarifa yoyote ya mapema juu ya AFC kushindwa kufika kituoni.

AFC ambayo mbali ya kushushwa daraja inatakiwa kulipa faini ya sh. milioni moja kabla ya kucheza Ligi ya Taifa msimu ujao. Sh. 500,000 kati ya hizo zitakwenda kwa timu ya 94 KJ iliyoingia gharama za kujiandaa kwa mechi hiyo ambapo wapinzani wao hawakufika uwanjani. Kundi C la ligi hiyo sasa linabakiwa na timu nne baada ya Manyoni FC ya Singida nayo kushuka daraja kwa kushindwa kucheza mechi yake dhidi ya Polisi Tabora iliyokuwa ifanyike Februari 12 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Timu zilizobaki katika kundi hilo ambalo baada ya mbili kujitoa hakuna itakayoshuka daraja ni 94 KJ ya Dar es Salaam, Polisi Tabora, Polisi Morogoro na Rhino FC ya Tabora.

No comments:

Post a Comment