KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 22, 2012

NCHUNGA: Tutabadili kikosi chetu



MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Lloyd Nchunga amesema bado kikosi chao kina nafasi kubwa ya kusonga mbele katika michuano ya klabu bingwa Afrika licha ya kutoka sare ya bao 1-1 na Zamalek.
Nchunga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, ana imani kubwa kuwa, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic atafanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Zamalek ya Misri.
Kiongozi huyo wa Yanga alisema tayari wameshampatia maelekezo Papic ya kukifanyia marekebisho kikosi chake ili kiweze kuibuka na ushindi.
Licha ya kupata nafasi nyingi za kufunga mabao, Yanga ilishindwa kutamba mbele ya Zamalek baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya bao 1-1. Mechi hiyo ilichezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu mbili hizo zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo mjini Cairo na timu yoyote itakayoshinda mechi hiyo itasonga mbele.
Nchunga alisema wamepata uhakika wa ushindi katika mechi ya marudiano baada ya kupona kwa baadhi ya wachezaji wao nyota kama vile kiungo Nurdin Bakari na kipa Yaw Berko.
Mwenyekiti huyo alisema pia kuwa, baadhi ya wafadhili wa klabu hiyo wamejitokeza kuwapa motisha wachezaji kwa lengo la kuwaongezea ari ya kufanya vizuri, lakini hakutaja motisha hiyo.
Kuna habari kuwa, mechi hiyo huenda ikachezwa nchini Sudan, kufuatia vurugu zilizotokea hivi karibuni wakati wa mechi ya ligi kati ya Al- Ahly na Al-Masry na kusababisha vifo vya mashabiki 74.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amesema sare waliyoipata dhidi ya Zamalek katika mechi yao ya awalihaijawakatisha tamaa ya kusonga mbele.
“Najua mechi ya marudiano itakuwa ngumu mjini Cairo, lakini nitahakikisha nawaandaa vyema vijana wangu,”alisema.

No comments:

Post a Comment