KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 22, 2012

Zamalek yaikamia Yanga



Mshambuliaji Amr Zaki wa Zamalek akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la kusawazisha ilipomenyana na Yanga katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya michuano ya klabu bingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. (Na mpiga picha wetu).


KOCHA Mkuu wa Zamalek, Hassan Shehata amesema wapo tayari kurudiana na Yanga mahali popote, hata kama itakuwa nje ya Misri.
Shehata ameueleza mtandao wa cafoline wiki hii kuwa, wanachosubiri kwa sasa ni maelekezo kutoka Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Misri aliiongoza Zamalek kutoka sare ya bao 1-1 na Yanga katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya michuano ya klabu bingwa Afrika iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hizo zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo mjini Cairo, lakini upo uwezekano mkubwa kwa pambano hilo kuchezwa bila watazamaji ama kuhamishiwa katika nchi nyingine.
“Tunasubiri maamuzi ya CAF iwapo tutacheza Cairo au la, ‘ alisema Shehata.
Kocha huyo ameyaelezea matokeo ya sare kati yao na Yanga kwamba yalikuwa mazuri kwao na kuongeza kuwa walikuwa wakiyahitaji.
Aliisifu Yanga kuwa ni timu nzuri na yenye kocha mzuri, lakini alisisitiza kuwa, wana uhakika mkubwa wa kuitoa na kusonga mbele.
Kwa upande wake, mshambuliaji Amr Zaki wa Zamalek amesema hana uhakika kuhusu mahali itakapochezwa mechi yao ya marudiano dhidi ya Yanga.
Hata hivyo, Zaki amesema wamejiandaa vilivyo kwa ajili ya mechi hiyo na aliisifu Yanga kuwa ni timu nzuri. Zaki ndiye aliyeifungia Zamalek bao la kusawazisha.
CAF ndiyo yenye uamuzi wa mwisho iwapo pambano hilo la marudiano kati ya Yanga na Zamalek, lichezwe mjini Cairo bila watazamaji ama lihamishiwe katika nchi nyingine.
Hatua hiyo imekuja kufuatia vurugu zilizotokea hivi karibuni mjini Port Said na kusababisha vifo vya mashabiki 74 wakati wa mechi ya ligi kati ya Al-Ahly na Al-Masry.
Kufuatia vurugu hizo, Shirikisho la Soka la Misri liliamua kusimamisha mechi zote za ligi nchini humo ili kupisha uchunguzi. Hadi sasa, bado shirikisho hilo halijatoa uamuzi wa kuruhusu ligi hizo ziendelee.

No comments:

Post a Comment